TASWIRA YA MLANGABOY : Wanamuziki wetu wengi hawawaimbii watu

Friday December 20 2019

By Andrew Kingamkono

HADITHI ileile. Ndiyo hadithi ileile timu ya Taifa ya Tanzania Bara pamoja na Zanzibar zimeshindwa kutamba katika mashindano ya Chalenji yanayoelekea mwishoni Uganda.

Zanzibar ilitolewa katika hatua ya awali ndugu zao Kilimanjaro Stars wenyewe wakafuata kwa kufungwa na Uganda katika mchezo wa nusu fainali.

Ni jambo linalotia aibu kwa kweli hasa kwa ikizinganitiwa kwamba siku zote tunajidanganya ligi yetu ni bora zaidi katika Ukanda wa Cecafa, lakini mara ya mwisho kuchukua ubingwa ilikuwa ni 2010 miaka tisa iliyopita tena fainali hizo zilipofanyika hapa Dar es Salaam, Tanzania.

Pia, hii si ishara njema kwa Tanzania hasa katika kipindi hiki ambacho wachezaji waliounda Kilimanjaro Stars na Zanzibar ndio hao tunawategemea kuunda kikosi cha Stars kitakachoshiriki mashindano ya CHAN2020 Cameroon Aprili mwakani.

Tuyaache hayo ya soka wiki hii Taswira inazungumzia muziki japo kwa uchache kwa sababu hali ya mambo inavyokwenda kwa sasa hapa nchini.

Hivi karibuni tumeshuhudia matamasha mawili makubwa ya muziki yakifanyika katika Jiji la Dar es Salaam tulianza na Tamasha la Wasafi tukamaliza na Tamasha la Fiesta, baada ya matamasha haya watu waliacha kujadili viwango na uwezo wa wanamuziki kutawala jukwaa na kukonga nyoyo za watu.

Advertisement

Watu mitandaoni walikuwa bize kuulizana nani amejaza watu wengi katika tamasha lake bila ya kuangalia mazingira yaliyofanyika matamasha hayo yalikuwa na tofauti kubwa Uwanja wa Chuo cha Posta na Uwanja wa Uhuru ni viwanja vyenye uwezo tofauti wa kuchukua watu.

Tumefika huko kwa kujadili idadi ya watu kwa sababu wanamuziki wetu wameshindwa kutupa kile kilichokuwa bora wawapo jukwaani, ndiyo maana tunakimbilia kuulizana nani amejaza uwanja.

Muziki wa siku hizi umekuwa mzuri kusikiliza katika redio au kuangalia katika TV tu, lakini unapokwenda kutazama jukwaani unakuchosha kwa sababu wanamuziki wetu wamekuwa na uwezo mdogo kutumbuiza jukwaani.

Lakini kama haitoshi tungo za muziki siku hizi zimekuwa nyepesi wengi wanakimbilia kuimba matusi, kusifu kunywa pombe na mapenzi ya watoto wa shule.

Hapo ndipo nikakumbuka kauli ya marehemu babu yangu Waziri Mbena aliniambia kuna wanamuziki wanaimbia watu.

Kauli hiyo ya Mzee Mbena ilitoka baada ya kusikiliza wimbo wa maheremu Dokta Remmy Ongala unaoitwa ‘Niseme nini’ kuna ubeti moja unasema hivi:

“Walipewa madaraka wakashindwa kuwajibika ooh, tembo wanateketea jamani, uchumi wa taifa unatopea, wengine wanalialia hivi sasa wamenyang’anywa madaraka wapo hoi, lakini wamesahau madhambi yao walipewa madaraka wakashindwa kuwajibika mmh, tazama sasa barabara mashimo matupu, hospitalini wagonjwa wanalala chini, mbunge anauza pembe. Nahuko Mtwara padri anauza sabuni za misaada, shekhe anauza bangi, huko Shimo la Udongo polisi anauza gongo vurugu mechi daktari kabaka mgongwa, mwalimu anauza maandazi eeh tutasoma kweli… saa mbili asubuhi foleni kwenye supu ofisi ipo nani...” Hii ni moja ya beti katika wimbo huo.

Pamoja na kusikia ujumbe wa wimbo huo bado nilikuwa sijaelewa aliposema kuna wanamuziki wanaimbia watu, je wengine wanaimbia n akina nani.

Alinijibu wanamuziki wote wanaimba, lakini wengine wanaimba kwa kuzungumza matatizo ya watu hasa yanayokabiri jamii zao.

Ndipo nilipoelewa maana ya muziki mzuri ni inayosema ‘Unaposema unapokuwa na furaha unafurahi muziki, lakini unapokuwa katika matatizo unaelewa mashairi ya wimbo.’

Ukisikiliza Wimbo wa Baba Lao, Uno na nyingine nyingi kuanzia mwanzo hadi mwisho hakuna ujumbe wowote wa maana au hata mstari mmoja unaweza kukupa elimu.

Najua muziki unaburudisha, unaelimisha, lakini muziki mzuri ni ule unaokupa elimu huku unakuburudisha unatakufanya udumu kwa muda mrefu kichwani mwa msikilizaji.

Ukiimba nyimbo za kuburudisha tu kuanzia mwanzo hadi mwisho bila ya kuweka japo mstari mmoja wa kumuelimisha msikilizaji unaondoa sifa za kuufanya muziki wao kuwa muziki mzuri na unakosa sifa ya kuimbia watu.

Watu hadi miaka 100 ijayo wataendelea kusikiliza nyimbo za Bob Marley, Remmy Ongala, Tupac, Michael Jackson, Marijani Rajabu, Mbaraka Mwinshehe, Banza Stone yote kwa sababu waliwaimbia watu.

Ni lazima wanamuziki wetu wa kizazi cha sasa pamoja na kutuimbia nyingi za stahere wajue wanawajibu wa kuhakikisha wanaimba kwa ajili ya watu kwa kuonyesha changamoto ambazo jamii inapitia ziwe za kiuchumi, matatizo ya kuvunjika kwa ndoa, elimu, siasa na mikasa.

Advertisement