Stars kanyaga twende, mbona hao The Cranes wanapigika tu

KIKOSI cha timu ya Taifa (Taifa Stars) kinaondoka nchini leo kwenda Kampala, Uganda kuvaana na wenyeji wao, The Cranes kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya kufuzu kwa fainali za Mataifa Afrika (Afcon 2019) zitakazofanyika kule Cameroon.

Taifa Stars ambayo kwa sasa iko chini ya kocha mpya, staa wa zamani wa Nigeria, Emmanuel Amunike itawafuata The Cranes baada ya kujifua kwa siku kadhaa, ikiwa na kikosi kilichosheheni wachezaji wenye uwezo na vipaji vya soka.

Wachezaji wa kimataifa wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi wakiongozwa na Nahodha wao Mbwana Samatta anayekipiga Genk ya Ubelgiji, wote walitua nchini kwa wakati na kuungana na wenzao katika programu zilizoandaliwa na mwalimu na wasaidizi wake kwenye benchi la ufundi.

Mwanaspoti linafahamu kuwa, Stars inakwenda Uganda ikiwa na kiu na ari ya ushindi ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kufuzu kwenye fainali hizo kwani, hata mazingira ya kambi ya timu hiyo wamekuwa yenye utulivu mkubwa ili kuweka sawa saikolojia za wachezaji.

Wachezaji wote waliochaguliwa kuunda kikosi cha Taifa Stars wana uwezo mkubwa wa kupambana uwanjani kwa ajili ya kupata matokeo mazuri. Taifa Stars iko Kundi L ikiwa na timu za Lesotho, Cape Verde na Uganda ambalo linatajwa kuwa miongoni mwa makundi magumu kwenye michuano hiyo. Kwa sasa Taifa Stars ina alama moja tu baada ya kutoka sare na Lesotho kwenye mchezo wa nyumbani hivyo, ushindi dhidi ya The Cranes ni faraja kubwa sio kwa wachezaji tu, bali hata kwa mashabiki wa soka nchini ambao wamekuwa na shauku kubwa ya kuiona timu hiyo inafanya vizuri kwenye anga za kimataifa. Hata hivyo, matokeo mazuri uwanjani hayawezi kuja bila wachezaji kujituma na kufuata maelekezo ya mwalimu.

Pia, suala la nidhamu ndani na nje ya uwanja ndio kichocheo cha matokeo mazuri kwa timu yoyote uwanjani hivyo, tuna imani kubwa wachezaji watakwenda Uganda na kufanya kile walichoelekezwa na mwalimu. Amunike mwenyewe wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mchezo huo, alisema ushindi ni lazima kwani wanahitaji kupata pointi tatu muhimu ama alama yoyote lakini, sio kupoteza.

Akasema ili kupata matokeo hayo ni lazima wachezaji waweke uzalendo na moyo wa kupambana kwa ajili ya nchi yao mbele.

Pia, alisema timu ya Taifa ni kwa ajili ya wachezaji wote na kwamba, aliowateua ana imani watakwenda kufanya kile kilichotarajiwa na Watanzania wengi, kupata ushindi kwa ajili ya Tanzania.

Ni imani yetu kuwa, wachezaji walioitwa kwenda kuwakilisha Tanzania watatambua wajibu na hatima waliyoibeba kwa ajili ya taifa lao. Wakumbuke kuwa matokeo mazuri ni ya Watanzania wote na hata mabaya pia ni ya Watanzania wote hivyo, wakapambane vilivyo kwa maslahi ya taifa letu.

Pamoja na mapambano ambayo Watanzania wanataka kuona timu ikifika mbali, wachezaji wanatakiwa kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu.

Mfano ulalamishi na mwamuzi, suala hilo anatakiwa kulimaliza Samatta kama kiongozi wa uwanjani, lakini pia wachezaji kutopiga mpira au kuonyesha ishara yoyote ya kupingana na mwamuzi. Lakini, kwa mashabiki hasa wala watakaosafiri kwanda kuishangilia timu yetu na wale Watanzania waishio nchini Uganda, wakajitokeze kwa wingi kuwapa mzuka wachezaji wetu. Watanzania wanapaswa kutambua kwamba, katika soka shabiki ni mchezaji wa 12 japo haingii uwanjani kucheza lakini, ile hamasa ya kushangilia imekuwa ikiwapa hamasa kubwa wachezaji uwanjani.

Taifa Stars imeshacheza na The Cranes mara nyingi na imekuwa ikipata matokeo mazuri hivyo, mchezo huu wa Jumamosi suala la kupata ushindi sio msamiati mkubwa kwani, Waganda wanapigika kiulaini tu.

Mungu ibariki Tanzania.

Mungu ibariki Taifa Stars.