Sina uhakika kama Karia amemwelewa vyema JPM

Rais wa TFF, Wallace Karia

Muktasari:

Katika halfa hiyo, Rais Magufuli alizungumza mambo mengi mno mno huku akisisitiza kuwa na uongozi bora ndani ya TFF wenye kujua matumizi mazuri ya madaraka na fedha kwa ujumla, akipinga vikali matumizi mabaya ya fedha kwamba hilo jambo anapingana nalo katika sekta yoyote.

WIKI iliyopita, Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli aliialika timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ Ikulu na alipata chakula cha mchana na wachezaji wa timu hiyo, makocha na viongozi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF).

Katika halfa hiyo, Rais Magufuli alizungumza mambo mengi mno mno huku akisisitiza kuwa na uongozi bora ndani ya TFF wenye kujua matumizi mazuri ya madaraka na fedha kwa ujumla, akipinga vikali matumizi mabaya ya fedha kwamba hilo jambo anapingana nalo katika sekta yoyote.

Katika hotuba ya Rais Magufuli, alimtaka Rais wa TFF, Wallace Karia kuwa na viongozi waadilifu kwenye uongozi wake ingawa maana kubwa ya Rais Magufuli ilikuwa pana ambayo inaonekana inachukuliwa juu juu na baadhi ya watendaji wa shirikisho hilo.

Karia ni kiongozi ambaye alichaguliwa na wanachama wengi ikiwa na maana alipita kwa kura nyingi ambazo hakuna mgombea yoyote aliyeweza kumkaribia kwa kura zake, yote hayo ni kutokana na wapigakura kuwa na imani kubwa juu yake kwamba atawaletea mabadiliko ndani ya TFF ambayo yana maendeleo makubwa.

Amekaa mwaka mmoja na miezi kadhaa tu akiwa Rais wa Shirikisho hilo lakini amekuwa ni kiongozi ambaye analalamikiwa kwa asilimia kubwa na wapiga kura wake.

Malalamiko hayo ni kutokana na utendaji kazi wa watu ambao amewaamini kumsaidia baadhi ya majukumu ambao wameonekana kushindwa kufanyakazi kwa uweledi.

Mfano mdogo tu ni hizi chaguzi ambazo zinaendelea na kusimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho hilo, ulianza uchaguzi wa klabu ya Simba na kikanuni ni lazima usimamiwe na kamati ya TFF na sio kuwa wao ndiyo wanakuwa mbele bali kuangalia kama kila kitu kinakwenda swa kwenye mchakato huo.

Kamati ya uchaguzi ya Simba ni kama iliteleza katika mchakato wao wa uchaguzi ndipo kamati ya uchaguzi ya TFF iliingilia na kuwataka wafanye mabadiliko ya kanuni ili ziendane na kanuni za uchaguzi za TFF pasipo kuathiri tarehe ya uchaguzi huo.

Cha ajabu baadaye Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao aliibuka na kumwandikia barua aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Wakili Revocatus Kuuli ili ajielezea kwanini amesimamisha uchaguzi wa Simba, ila ukweli uchaguzi haukusimamishwa na kilichotamkwa ni kufanya marekebisho ya kanuni za uchaguzi. Hapo walikurupuka na sababu wanazifahamu wao.

Hilo likapita, kuna uchaguzi unaendelea wa Bodi ya Ligi (PTBL) wa kuziba nafasi iliyoachwa wazi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi hiyo Clement Sanga pamoja na nafasi tatu za wajumbe wa bodi.

Uchaguzi huu unaendeshwa kwa siri kubwa mno mno, ingawa kuna tetesi kwamba tayari ameandaliwa mtu wa kuongoza nafasi hiyo. Ni kichekesho.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilimuondoa mgombea mmoja kati ya watatu waliojitokeza kuchukuwa fomu ambaye ni Mkurugenzi wa Alliance, James Bwire, bila kufanyiwa usaili yaani alikatwa juu kwa ju. Hiyo haijalishi pengine ni mahaba ya kuwa na kiongozi wanayemtaka ama kanuni kweli hazimruhusu kiongozi huyo.

Wamebaki wagombea wawili, Steven Mguto ambaye ni Mwenyekiti wa Coastal Union ya Tanga na Emmanuel Kimbe ambaye ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa klabu ya Mbeya City baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo Musa Mapunda kustaafu.

Kituko ni, Mguto alimwekea pingamizi Kimbe kwamba haruhusiwi kikanuni kugombea kwani yeye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mbeya City.

Inafahamika uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya ambayo ndiyo wamiliki wa timu hiyo, ilimtambulisha Kimbe kuwa Mwenyekiti wa Mbeya City tangu Januari Mosi, 2018 ambapo kwa mujibu wa pingamizi ya Mguto iliyopelekwa Oktoba 16, 2018, haina mashiko labda kuwe na sababu nyingine.

Mguto na wale waliopokea pingamizi hiyo bila kuitupilia mbali wanapaswa kujipima kwanza na kujiridhisha na pingamizi yao kabla ya kutoa maamuzi.

Pingamizi hilo linaleta taswira mbaya kwa wadau wa soka nchini hasa ambapo kuna tetesi za kutaka kumpigania Mguto kuwa Mwenyekiti wa bodi hiyo na mgombea huyo kupeleka pingamizi yenye mapungufu mengi.

Karia kaa ufahamu kwamba kauli za Rasi Magufuli zilikuwa hazilengi matumizi mabaya ya fedha pekee bali hata matumizi mabaya ya madaraka, maana inaonekana ndani ya TFF kwa baadhi ya watendaji wako wanatumia vibaya ofisi ya umma. Kaa ulitafakari hilo halafu uchukuwe hatua.