STRAIKA WA MWANASPOTI : Simba na Gor Mahia kazi bado mbichi ugenini

Tuesday April 9 2019

 

By Boniface Ambani

Wahenga walisema kupanda mchongoma, kushuka ndio ngoma.

Haya ndugu zanguni tumekutana tena kwa mara nyingine kuangazia soka letu la ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Wengi wanashindwa kuelewa ni nini kimezikumba timu zetu mbili za Simba ya Tanzania na Gor Mahia ya Kenya kwenye michezo yao ya kwanza ya michuano ya kimataifa na kushindwa kupata matokeo chanya ya kurahisihsa kazi kwenye michezo yao ya marudiano.

Kazi ipo ya kufanya kwa klabu zetu hizi mbili kwenye michuano hiyo mikubwa Afrika.

Wakati tunaposubiria droo ya kujua timu zetu za kimataifa zinapangwa katika makundi yapi katika mashindano ya Kombe la Mataifa barani Afrika (Afcon), droo itakayofanyika Misri katika yale maeneo ya ma pyramids, tayari klabu zetu kanda hili zimeanza mashindano ya robo fainali kwa njia zisizo za kueleweka.

Simba Sports Club, vijana wa Msimbazi walianza mashindano hayo kwa kupiga sare ya 0-0 jijini Dar na TP Mazembe kutoka Congo kwenye Klabu Bingwa Afrika.

Ni mechi ambayo wangeshinda vizuri tu lakini nahodha wao John Bocco alipaisha penalti kipindi cha pili baada ya beki wa TP Mazembe kuunawa mpira ndani ya kijisanduku akizuia krosi iliyopigwa na Meddie Kagere.

Ni mechi ambayo kwa mtazamo wangu wa karibu ilikuwa moto sana kwa pande zote mbili.

Simba walipoteza nafasi zao nyingi tu, kama ilivyokuwa kwa TP Mazembe na mwishowe kuondoka bila bao lolote.

Ni ishara kuwa mechi ya marudiano nchini Congo inaenda kuwa moto zaidi, Si9mba ikihitajika kujipanga zaidi ili wawafunge TP Mazembe kwao japo ni wazi kuna ule msemo wa mcheza kwao hutunzwa na Mazembe ni hatari zaidi wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani. Kazi ipo kwa Simba.

Simba wafahamu kuwa TP Mazembe ni wazoefu wakubwa katika mechi hizi za kimataifa. TP Mazembe wamelishinda taji hilo zaidi ya mara mbili.

Wapo katika robo fainali na ukweli inaenda kuwa kazi Kubwa sana kwa Simba mechi ya marudiano.

Wakati huo huo, Gor Mahia kwa mara ya kwanza walicheza vibaya sana mechi yao nyumbani Nairobi Uwanja wa Kasarani.

Walipoteza mechi kwa kichapo cha mabao 2-0. RS Berkane walifunga mabao hayo katika kipindi cha kwanza na cha pili kupitia kwa beki Dayo na mshambuliaji Helali ambaye alimpokonya beki wa Gor Mahia ndani ya kijisanduku na kumwacha kipa wa Gor Mahia akitazama tu bila kujua afanye nini.

Ukosefu wa Shafik Batambuze kwenye beki la kushoto, beki wa kati, Haron Shakava na mshambuliaji Jacques Tuyisenge kwa kweli kuliathiri kikosi cha Gor Mahia pakubwa.

Ni aibu kwa sababu ndani ya dakika 90 hakuna hata shuti moja lilipigwa langoni mwa klabu ya RS Berkane.

Mabao 2-0 nyumbani ndugu zangu mechi za marudiano kutakuwa na kazi Kubwa sana ya Gor Mahia kufanya nchini Morocco. Ipo Kazi.

Kazi Kubwa saana. Nasema hivyo kwa sababu gani, kulingana na mchezo Gor Mahia walicheza hapa, sijui mabao matatu watayatoa wapi huko Morocco.

Shughuli ipo na ni kubwa sana. Gor Mahia wamekuwa wazoefu katika mashindano hayo lakini hata hivyo kamgomo baridi walikuwa nako basi kalichangia kidogo katika uchezaji wao.

Ni vyema wachezaji na viongozi kuelewana na kusiwe na mshikemshike wakati wachezaji wanapojiandaa katika mashindano haya makubwa ya kimataifa.

Gor Mahia wanasafiri ndani ya siku tatu zijazo kwa mechi ya marudiano. Ni Tuyisenge pekee yake ambaye nadhania atakuwepo katika wachezaji ambao wapo nje.

Amemaliza kifungo chake. Swali ni ataweza? Ukosefu wa Shakava na beki wa kupanda na kushuka Shafik Batambuze kumeathiri kikosi hicho pakubwa.

Acha tutazame kutaendaje. Kocha Oktay sko na kazi ya kufanya. Washambulizi wake Mustafa na Oliech Denis na Bonface Omondi kwa kweli hawakutendea haki kikosi hicho juzi. Lazima wachangamke.

Simba vile vile wako na kazi. Yangu ni kuwaombea baraka zangu. Kazi kwao. Sisi ni kuweka macho tu. Kivumbi kinatimka wikendi ijayo.

Advertisement