WINO MWEUSI : Simba msirudie makosa yale yale, yatawagharimu

Wednesday March 6 2019

 

By Thobias Sebastian

KIKOSI cha Simba kiliondoka jana saa 10:40 jioni na Shirika la ndege la Emirates hadi nchini Algeria na walipitia kwanza Dubai ili kuunga ndege ya kwenda Algers ambako watakaa kwa siku mbili kabla ya kuchukua tena ndege nyengine mpaka Saoura.

Simba ndio wawakilishi pekee wa Ligi ya Mabingwa Afrika kutoka ukanda wa Afrika Mashariki wakiwa katika hatua ya makundi sambamba na Al Ahly kutoka Misri, AS Vita ya Kongo na JS Saoura ya Algeria.

Iko kundi ‘D’ na imeshacheza mechi nne kati ya sita ambazo inatakiwa acheze ili kufahamu timu mbili zitakazosonga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.

Imeshinda mechi mbili dhidi ya JS Saoura kwa mabao 3-0, na ile dhidi ya Al Ahly kwa bao 1-0, lakini walipoteza mechi mbili dhidi ya Al Ahly na AS Vita zote akifungwa mabao matano.

Baada ya kupata matokeo hayo Simba wapo katika nafasi ya pili wakiwa na pointi sita, Al Ahly ndio vinara wakiwa na pointi saba, nafasi ya tatu AS Vita ambao wamevuna pointi tano huku JS Saoura ambao watacheza na Simba Jumamosi wanaburuza mkia wakiwa na pointi nne.

Kwa kundi ‘D’ lilivyo kila timu imebakiwa na michezo miwili kila mmoja atacheza nyumbani moja na ugenini moja na kutokana na pointi za kila timu yoyote ambaye anaweza kufanya vizuri katika mechi zilizobaki atakuwa na nafasi ya kusonga hatua ya robo fainali.

Wiki hii wino mweusi inatazamia mchezo wa Simba ambao watakuwa ugenini ambao kama wakishinda kwa maana ya kupata pointi tatu na Vita kufungwa dhidi ya Al Ahly pale Kongo ni wazi wawakilishi hao kutoka Tanzania watakuwa wameshafuzu.

Hata kama Simba wakishindwa kupata ushindi hata sare ya aina yoyote kwao itakuwa nzuri kwani watafikisha pointi saba, ambazo zitawafanya kuwa katika mazingira mazuri ya kusonga mbele huku wakiwa na mchezo mmoja nyumbani na wamekuwa na rekodi nzuri ya kushinda mechi za nyumbani.

Ili Simba wafanikiwe kwa kupata hayo matokeo ya ushindi au sare kama malengo yao yalivyo ni kutokufanya makosa yale ambayo waliyafanya katika mechi mbili zilizopita ambazo walicheza ugenini kwa kupoteza kwa jumla ya mabao kumi.

Katika mechi zote mbili kosa la kwanza ambalo liliwagharimu ni kutokuwa na umakini mkubwa wa kukaba hasa ile mipira ya kona ambayo walifungwa mabao ya aina moja licha ya kwamba walilifanyia kazi hilo wakiwa mazoezini.

Makosa hayo ya kukaba kwa macho yalionekana si kwa safu ya ulinzi tu bali ni timu nzima walikuwa na uwezo mdogo wa kukaba na ambao ulichangia kufanya makosa mengi ambayo wachezaji wa timu pinzani walionekana kucheza kwa uhuru.

Tatizo lingine ni kupoteza mipira mara kwa mara ambayo muda mwingine ilikwenda kuzaa bao, mfano katika mechi na Al Ahly ugenini beki wa kati Pascal Wawa aliokoa mpira nyuma na alitaka kupiga chenga kabla ya mpira kunaswa na kwenda kufungwa bao.

Kosa lingine ni faulo nyingi ambazo zilikuwa hazina ulazima, kwani moja ya mabao waliyofungwa Simba ni kucheza faulo ndani ya boksi ambayo ilikuwa haina ulazima na wapinzani wakapata penalti.

Simba wanatakiwa kuingia katika mchezo huo wakifahamu wanacheza ugenini kwa maana hiyo wanatakiwa kuwa na nidhamu kubwa ya mchezo na kutokutaka kushambulia mara kwa mara kama walivyofanya katika mechi mbili za ugenini kwani wakitamani kufanya hivyo itawagharimu

Pia Kocha wa Simba, Patrick Aussems nae anatakiwa kubadilika katika upangaji wake wa kikosi kwa maana hata kama alikuwa na malengo ya kupata ushindi na mambo yakaonekana kuwa magumu ili kupunguza idadi kubwa ya mabao ya kufungwa anatakiwa kumpumzisha mchezaji mwenye asili ya kukaba na kumuingiza mwenye uwezo katika kushambulia.

Katika mechi za AS Vita na Al Ahly Simba walionekana kuzidiwa na hata wasingekuwa na uwezo wa kufanya lolote kwa maana ya kupindua matokeo lakini Aussems alionekana kutoa wachezaji washambuliaji na kuingiza washambuliaji jambo ambalo lilifanya kikosi chake kuendelea kuwa eneo hatarishi zaidi.

Katika mechi zote mbili za ugenini Simba walionekana kushindwa kutengeneza nafasi za kufunga kama wanavyo fanyaga katika mechi za hapa Dar es Salaam, lakini katika hili kosa ambalo walifanya ni zile nafasi chache ambazo zinatokea kwa nadra na kushindwa kuzitumia. Katika mechi na Vita mwanzoni mwa mchezo Simba walipata nafasi ya wazi kupitia kwa Meddie Kagere ambaye alishindwa kufunga na kipa Vita akapangua mpira huo.

Wino mweusi inawakumbusha Simba ili kufanya vizuri katika mchezo huo wanatakiwa kuyaboresha haya ili kutimiza malengo yao, lakini kama wakiyarudia tena halitakuwa jambo la kushangaza kuona wanacheza kipigo kingine ugenini kwa mara ya tatu.

Advertisement