Simba ikibadilisha mambo ugenini, itatoboa kwa TP Mazembe

Muktasari:

  • Kabla ya mchezo huo wa jana hakuna Mtanzania aliyekuwa shaka na Simba inapocheza nyumbani imejiwekea rekodi nzuri ya kupata ushindi inapokuwa nyumbani..

MAMBO yanakwenda kasi sana na kuna mambo mengi, lakini shida ni muda mchache. Baada ya droo ya mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ghafla wikiendi hii Simba imekutana na TP Mazembe ya DR Congo.

TP Mazembe iliyowasili nchini Jumatano iliyopita, imecheza na Simba jana Jumamosi na kulazimisha sare 0-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa hatua hiyo.

Kabla ya mchezo huo wa jana hakuna Mtanzania aliyekuwa shaka na Simba inapocheza nyumbani imejiwekea rekodi nzuri ya kupata ushindi inapokuwa nyumbani.

Simba inapokuwa nyumbani msimu huu katika Ligi ya Mabingwa hakuna aliyefanikiwa hata kupata sare, timu zote zilizotia mguu Uwanja wa Taifa zilitoka patupu. Isipokuwa Mazembe pekee waliofanikiwa kuondoka na pointi moja Dar es Salaam.

Wakati Simba ikiweka rekodi hiyo nyumbani hatua mbaya kwake ni pale inapotoka bila ya ushindi wowote inapocheza ugenini. Haijawahi hata kupata sare ukianzia mechi za hatua ya makundi na mechi pekee iliyoshinda ugenini ni katika ile ya hatua ya mtoano ilipofunga 4-0 Mbabane Swallows ya e-Swatin. Hapa ilifanya kweli tena kwa idadi kubwa ya mabao huku ikicheza soka safi na wenyeji walitulia.

Hapa mambo sasa yanabadilika na kuanza kugeuka changamoto kwa Simba kutokana na hatua iliyofikia kama inashinda nyumbani inatakiwa kufanya makubwa ili isipate ugumu inapokwenda ugenini.

Changamoto ya Simba iko hapo na ubora wake utathibitika hapo kutokana na sasa Wekundu wa Msimbazi hawako tena eneo la kuhesabu pointi wako katika eneo la ulivuna kipi nyumbani na utavuna kipi ugenini, biashara imeisha.

Kama Simba ina malengo ya kufika nusu fainali na hata fainali kuanzia inapocheza dhidi ya TP Mazembe inatakiwa kubadilika na kuwa na uthubutu inapokuwa ugenini.

Shida inaweza kuwa mfumo wake na kama hilo ndiyo Kocha wa Simba, Patrick Aussems anatakiwa kubadilika haraka kuhakikisha wachezaji wake wanakuwa na mabadiliko katika kucheza ugenini. Tishio la Simba ni rekodi ya TP Mazembe ambayo msimu huu haina ushindi ugenini lakini ina rekodi mbaya ya kumfunga mpinzani wake mabao 8-0 katika uwanja wake wa nyumbani.

Simba sio timu ya kufungwa mabao manane lakini ikumbukwe tayari msimu huu imeshapoteza mara mbili ugenini kwa vipigo vya mabao 5-0 hapa ndiyo kwenye shida.

Simba ikitaka kujihakikishia kufika nusu fainali inatakiwa kuendelea kufanya vizuri nyumbani tena zaidi kuliko ilivyofanya katika mechi zilizopita.

Wanasimba wengi watafarijika zaidi kama Simba ikipata hata sare ugenini kwani wataanza kunusa harufu ya timu yao kuwa na ubora mkubwa lakini kama itaendelea kupoteza itazidi kuwatesa.

Inawezekana kwa Simba kuizuia TP Mazembe nyumbani lakini pia haitakuwa kazi rahisi endapo hakutakuwa na mabadiliko ya mbinu inapokuwa inacheza ugenini.

Kocha Aussems anatakiwa kuiongoza Simba kwa kutangulia kuwabadilisha wachezaji wake akili ya msemo walioubeba katika hatua ya makundi kwamba kila mtu ashinde kwake.

Simba ina uwezo wa kufanya mabadiliko na kupata ushindi ugenini, lakini kinachotakiwa ni kubadilika kimbinu zaidi kuliko kitu kingine.

Nilikuwepo pale Uwanja wa Mashujaa jijini Kinshasa wakati Simba ikipoteza dhidi ya AS Vita. Niliiona Simba ambayo inacheza mechi ya ugenini kama inavyocheza mechi za nyumbani.

Lakini, pia safu ya ulinzi ya timu hiyo ilikuwa na makosa mengi ambayo yaliipa nafasi sana AS Vita. Pia, wakati tunamwangalia Aussems ni wakati wa wachezaji kubadilika kwa kutofanya makosa hasa wanayokatazwa na makocha.

Nakumbuka Aussems aliwaambia juu ya makosa ya kutokaba vyema mipira ya krosi, lakini makosa hayohayo ndiyo yalikujua kufanyika katika mechi ile. Udhaifu huo wa kucheza mipira ya kona na krosi pia, ulionekana kwenye mchezo wa ugenini dhidi ya Al Ahly, ambapo Simba iliruhusu idadi kubwa ya mabao kama ilivyokuwa kwa AS vita.

Suala hili linaleta haka na sasa wachezaji wanatakiwa kubadilika na kufuata kile wanachofundishwa na mwalimu ili kuhakikisha Simba inafanya kweli.

Kama kasumba hiyo itaendelea tutaweka mashaka juu ya ubora wa wachezaji hao kwa kutokuwa na mabadiliko katika ubora wao.