MAONI YA MHARIRI: Simba, Yanga zijitathimini na kujipanga kikamilifu kimataifa

Friday January 12 2018

 

By MWANASPOTI

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya klabu barani Afrika; Simba na Yanga, tayari wameondoshwa kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayofikia tamati kesho Jumamosi kisiwani Unguja, Zanzibar.

Simba ndiyo ilikuwa ya kwanza kuondolewa katika michuano hiyo baada ya kupoteza mchezo wa mwisho wa makundi mbele ya URA. Simba ilifungwa bao 1-0 na Waganda hao huku baadhi ya mastaa wa Msimbazi wakionyesha utovu wa nidhamu wa kupindukia.

Kombe la Mapinduzi la mwaka huu limekuwa gumu kwa Simba kwani, hadi mechi za makundi zinamalizika, ilikuwa imeshinda mchezo mmoja tu kati ya minne. Ilipoteza miwili na kutoa sare moja.

Yanga nayo licha ya kuonyesha kiwango bora katika mechi za makundi, ilifia pia kwa URA juzi Jumatano ilipotolewa kwa penalti 5-4 kwenye mechi ya nusu fainali. Mechi hiyo ilikwenda hatua hiyo baada ya kumaliza dakika 90 bila ya timu hizo kufungana.

Kutolewa kwa Yanga kumeendeleza maumivu kwao katika suala la upigaji wa penalti kwani, ndani ya miaka miwili, wanakuwa wameondoshwa katika mashindano manne kwa mikwaju hiyo.

Yanga ilipoteza mapambano mawili ya Ngao ya Hisani mwaka 2016 kwa Azam na mwaka jana kwa Simba, yote kwa mikwaju ya penalti. Mwaka jana iliondoshwa pia kwenye nusu fainali ya Mapinduzi na Simba kwa mikwaju hiyo hiyo ya penalti.

Ni wazi sasa tatizo la penalti limeanza kuwa sugu ndani ya klabu hiyo, hivyo benchi la ufundi linatakiwa kutuliza akili na kulifanyia kazi ili kulipatia ufumbuzi wa kudumu.

Haiingii akilini kwamba Yanga imekuwa na udhaifu mkubwa kiasi hicho kwenye kupiga penalti. Imefikia hatua sasa timu hiyo inapoingia kwenye hatua hiyo ya penalti, hata mashabiki wake wanakosa imani na wakati mwingine huamua kuondoka uwanjani.

Inahitajika nguvu ya ziada kwa makocha wa Yanga kuwanoa wachezaji wao vilivyo ili kuwaondoa kwenye unyonge huo wa kupoteza penalti ambazo kwenye mchezo wa soka huwa haziepukiki.

Upande wa pili, kutolewa kwa Simba na Yanga katika mashindano ya Mapinduzi japo kwenye hatua tofauti, kunapaswa kuwa fundisho kwa timu hizo ambazo mwezi mmoja baadaye zitaanza kucheza mechi za kimataifa.

Simba na Yanga zinapaswa kutulia chini na kufanya tathmini ya mashindano hayo ya Mapinduzi, ili ziweze kufahamu pale zilipokosea ni wapi na kufanyia marekebisho.

Kumekuwa na changamoto kubwa kwa timu hizo hasa pindi zinapokutana na timu zenye uwezo wa juu. Simba na Yanga zimekuwa zikipata shida pindi zinapokutana na Azam, Singida United na URA ambazo zina ushindani wa hali ya juu.

Ni wazi kwamba ili timu iweze kuwa bora, inahitaji kuzifunga timu kubwa na bora zaidi, lakini kwa klabu hizi msimu huu hilo limekuwa mtihani kwao. Timu hizo bado hazijawa na nguvu kubwa katika kucheza mechi za daraja la juu. Tuliona hata Yanga walipokutana na Singida United walipata wakati mgumu kushinda na hata sare yenyewe waliipata dakika za mwishoni.

Simba ilifungwa bao 1-0 na Azam ambayo msimu huu imekuwa na mabadiliko makubwa. Kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo walikutana mapema mwezi Septemba, Simba iliyokuwa na mastaa wengi haikuweza pia kupata ushindi.

Ni imani yetu kwamba mabenchi ya ufundi ya timu hizo mbili yatakaa na kutathimini ili kufanya vizuri kwenye mechi kubwa.

Hakuna ubishi kwamba, mechi za kimataifa ni kubwa na ngumu, hivyo Simba na Yanga zinapopata wakati mgumu kushinda mechi kubwa hapa nchini, ni wazi zinaacha maswali mengi juu ya uwezekano wa kufanya vizuri kwenye michuano mikubwa.

Ni matumini yetu kwamba, tathimini itakayofanyika kwa timu zote mbili italeta mageuzi makubwa katika mechi zao zinazokuja pamoja na kutengeneza msingi imara wa kushiriki michuano ya kimataifa.

Tunahitaji kuona timu zetu hizo zikitutoa kimasomaso mwaka huu kwa kuwa na ushiriki mzuri na wenye matokeo bora na sio kusindikiza na kutolewa mapema.

Pia, ni matarajio ya wadau wengi wa soka hapa nchini kuona timu hizo zikifika angalau hatua ya makundi ambayo ndiyo msingi halisi wa michuano hiyo ya Afrika.