JAMVI LA KISPOTI : Simba, Yanga ni wakati wakutengeneza timu bora

Thursday May 16 2019

 

By Khatimu Naheka

MWISHO wa mwezi Mei, Ligi Kuu Bara itamalizika na timu itakayoliwakilisha taifa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayoanza mwezi Agosti itajulikana.

Pia timu tatu zitakazoshuka daraja zitafahamika huku African Lyon tayari imeshatangulia zikiipisha Namungo ya Lindi na Polisi Tanzania ya Moshi ambazo zimeshapanda daraja na msimu ujao zitacheza Ligi Kuu Bara.

Kumalizika kwa ligi pia kutatoa fursa ya timu kufanya usajili kuongeza nguvu kwenye vikosi vyao huku pia zikiachana na baadhi ya wachezaji walioonekana hawana mchango wowote.

Hata hivyo, kabla ya dirisha la usajili kufunguliwa timu kubwa za Simba, Yanga na Azam zimeshaanza makeke ya kutaka kufanya usajili kulingana na wachezaji ambao wameonyesha dhamira ya kuwahitaji ingawa mpaka sasa bado hawajafanya hivyo.

Azam, wao kabla ya kuanza makeke ya usajili kwa kuwataka wachezaji kutoka timu nyingine wameanza kuboresha mikataba ya wachezaji wao wa kikosi cha kwanza ambao wamekuwa wakitumika mara kwa mara.

Azam wamewaongezea mikataba mabeki Yakub Mohammed, ambaye alikuwa akiwindwa na Simba kutokana mkataba wake ulikuwa unamalizika mwezi Desemba mwaka huu, wengine Bruce Kangwa na Abdallah Kheri ‘Sebo’ ambaye kwa sasa ni majeruhi.

Advertisement

Kwa upande wa Simba na Yanga wao wameshaanza makeke yao ya usajili kutokana wakihusishwa kuwataka wachezaji fulani kutoka hapa ndani na nje ya nchi.

Simba wao wameonyesha nia ya kuwataka Ibrahim Ajibu wa Yanga, Yakub Mohammed, Azam ambaye alimeshaongeza mkataba mpya wa miaka miwili, Jacques Tuyisenge wa Gor Mahia ya Kenya na Lazadius Kambole wa Zesco United ya Zambia.

Wengine ni Yacouba Songne wa Asante Kotoko ya Ghana, Walter Bwalya wa Zesco ya Zambia na Juan Makusu wa AS Vita lakini Simba wana kila dalili ya kuwakosa kutokana nyota hao kuna ambao wamesajiliwa na timu nyingine na wengine kuongeza mikataba katika timu zao.

Kwa upande wa Yanga nao hawapo kimya kwani tayari wameshaonesha nia ya kuwanasa nyota kadhaa kama Juuko Murshid na Nicholas Gyana kutokea Simba, Hassan Kabunda kutoka KMC, Faruk Shikhalo wa Bandari ya Kenya na wengine wengi.

Simba kama wataweza kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu na kutwaa ubingwa kwa maana hiyo watarudu tena Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao kwa maana hiyo hawatakiwi tena kufanya usajili ya miemko kama walivyokuwa wakifanya misimu ya nyuma.

Uongozi wa Simba unatakiwa kukaa chini na kocha wao Patrick Aussems kumsikiliza anataka wachezaji wa aina gani ili kuwasajili kwa msimu ujao kulingana na mapungufu ambayo waliyaonyesha msimu huu ili kuweza kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita.

Uongozi wa Simba kama utatulia na kumsikiliza Aussems kutokana na mapungufu ambayo waliyaonesha katika mashindano yote hayo watasajili wachezaji imara ambao watakuja kufikia malengo yao ambayo wamejiwekea msimu huu kama ambavyo amekuwa akikaliliwa mdhamini wao Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’.

Yanga nao wameanza vizuri msimu ujao baada ya kufanya uchaguzi wa viongozi makini ambao kabla ya msimu huu kumalizika wameanza kuonesha mipango yao ya kuhakikisha wanatafuta pesa ili kufanya usajili wa maana kulingana na mipango ya kocha wao Mwinyi Zahera.

Uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti wake Dk Mshindo Msolla unatakiwa kukaa na Mwinyi Zahera kumsikiliza mahitaji ya wachezaji ambao anawataka ili kuongeza nguvu katika kikosi hiko msimu ujao kwani msimu huu haukuwa mzuri kwao.

Zahera alishakaririwa ameshaanza kufanya mazungumzo na wachezaji wa maana ambao anaamini kama wataweza kuwapata hao, Yanga itakuwa kali zaidi ya msimu huu ambao licha yab kuonekana wamekuwa na matatizo mengi ya kiuchumi laini wapo katika nafasi ya kwanza au ya pili kwenye msimamo wa ligi.

Kwa maana hiyo msimu ujao hawatakuwa katika mashindano yoyote ya Kimataifa, hivyo wanatakiwa kuisuka timu kuwa imara ili kufanya vizuri katika mashindano yote ambayo watashiriki na kufikia malengo yao ya kufanya vizuri kuliko msimu huu ikiwemo kucheza mashindano ya Kimataifa.

Wakati huu uongozi wa Simba na Yanga wakishirikiana na benchi la ufundi wanatakiwa kutulia na kufanya usajili wa maana kulingana na mapungufu ya vikosi vyao ili kila timu kuweza kufikia malengo yake ambayo wamejiwekea.

Advertisement