STRAIKA WA MWANASPOTI : Simba, Gor Mahia zimeing’arisha Afrika Mashariki

Muktasari:

  • Mabao ya Simba yalifungwa na beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Chama yalitosha kuizika AS Vita Club. na Wana Msimbazi wakaanza kusheherekea ushindi huo.

MBWEMBWE, vifijo na nderemo vilisikika kote Afrika Mashariki baada ya klabu ya Gor Mahia na Simba kufuzu kwenye robo fainali za mashindano ya makombe ya Washindi Caf na Confederation Cup Afrika.

Simba Sports Club ilikuwa ya kwanza kufuzu kwa hatua ya robo fainali Jumamosi baada ya kuilaza As Vita ya Congo mabao 2-1 jijini Dar Es Salaam.

Jiji la Dar lilisimama na Tanzania kwa jumla shughuli za kila siku zilisimama kupisha shamrashamra za kila kona. Ilikuwa raha isiyo na kifani baada ya mchezaji mwenye asili ya Zambia, Clatous Chama kupachika bao la ushindi bao ambalo liliwezesha Simba kufuzu robo fainali,nyuma ya Al Ahly ya Misri.

Al Ahly ilimaliza katika nafasi ya kwanza katika kundi hilo baada ya kuidhibu JS Soura mabao 3-0 katika kundi hilo.

Mabao ya Simba yalifungwa na beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Chama yalitosha kuizika AS Vita Club. na Wana Msimbazi wakaanza kusheherekea ushindi huo.

Katika upande wa pili, kulikuwa na presha kubwa jijini Nairobi, wakati Gor Mahia FC iliposhuka dimbani kumenyana na Petro De Luanda ya Angola katika Michuano ya Kombe la Shirikisho yanayojulikana Kama Total Caf Confederation Cup.

Kipindi cha kwanza kiliambulia patupu kwa timu hizo kwenda sare tasa.

Kipindi cha pili, Gor Mahia iliongeza kasi na kuweza kupata penalti ambayo ilitiwa kimyani na mchezaji Jacques Tuyisenge raia kutoka Rwanda.

Ni mechi ambayo Gor Mahia ilimaliza wakiwa na wachezaji tisa uwanjani baada ya wachezaji wake wawili kulimwa kadi nyekundu.

Ndani ya dakika 15 za mwisho, Gor Mahia ilistahimili mafuriko kutoka kwa Pedro hadi mwisho. Kumbuka lilikuwa ni kundi ambalo kila klabu ilikuwa ina uwezo wa kufuzu.

Kundi hilo lilikuwa na klabu za Zamalek iliyokuwa na alama nane, Hussain Dey (saba), Petro (saba) na Gor Mahia iliyokuwa na alama sita.

Kwa alama hizo ilimaanisha timu yoyote ingepata ushindi tu siku hiyo basi ilikuwa inafuzu.

Zamalek katika mechi yake ya mwisho ikatoa sare na Hussain Dey. Sare ambayo iliwaezesha kufikisha alama tisa. Gor Mahia nayo ikiwa katika nafasi ya mwisho ikatoa na ushindi dhidi ya Petro ikasonga mbele na kushika nafasi ya pili ikiwa na alama tisa. Baada ya ushindi na kufuzu kwa robo fainali, jiji la kuu la Kenya, Nairobi kwa kweli halikukalika.

Zilikuwa ni shangwe za kila kona. watu walishangilia kwa nguvu zao zote kwa hatua hiyo ambayo ni ngumu kwelikweli.

Binafsi nazitakia klabu hizo mbili za Afrika Mashariki kila la kheri kati mechi zifuatazo za robo fainali.

Simb ana Gor Mahia zimeiweka kanda yetu hii katika chati ya Afrika kwa kufikia hatua hiyo za robo fainali katika mashindano hayo ya barani. Inaonyesha iwapo Afrika Mashariki tutapanga mikakati yetu vizuri tu muda sio mrefu tutakuwa tunatikisa kama sio kutawala soka la Afrika.

Ni suala la muda na mikakati tu. Tukijipanga vizuri mbona pia sisi tutasisikika duniani nzima. Mbona tutakuwa na wachezaji wengi tu wa kulipwa wengi tu huko nje?

Suala lililobaki kwa sasa ni kuangalia timu hizo zitacheza na timu gani katika hatua inayofuata.

Droo ya robo fainali inafanyika kesho Jumatano, hapo ndipo tutajua timu zetu hizo zitachuana na timu gani katika hatua hiyo.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika wapinzani wa Simba wanaweza kuwa Esperance ya Tunisia, Wydad AC Morocco, Cs Constantine Algeria, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Horoya na TP Mazembe Congo.

Kumbuka Simba haiwezi kupangwa na timu ya Al Ahly ya Misri kwasababu zote zimetoka kundi moja katika hatua ya makundi.

Katika Kombe la Shirikisho (Total CAFCC,) wapinzani wa Gor Mahia ni Rs Berkane Morocco, Cs Sfaxien Tunisia, Al Hilal Club Sudan, Hassania Agadir Morocco, Etoile Du Sahel Tunisia, Nkana ya Nigeria, Na Gor Mahia kutoka Kenya ndizo klabu ambazo zilifuzu robo fainali. Pia, Gor Mahia haitaweza kupangwa na Zamalek ya Misri kwa sababu kama zile za Simba.

Kikubwa kwetu ni kuhakikisha klabu za Simba na Gor mahia zinapata maandalizi mazuri katika mashindano hayo. Tunajua Mashirikisho ya Soka ya Tanzania na Kenya, TFF na FKF yataendelea kuhairisha mechi za timu hizo la Ligi Kuu. Jambo lingine pia ni kuwapongeza mashabiki wa Simba Sports Club kwa kazi nzuri ya kufurika kiwanjuani kila timu yao ilipocheza. Mashabiki waliujaza Uwanja wa Taifa kwelikweli.

Hakuna budi kwa Wakenya kuwaiga mashabiki hao kwa kuwapa hamasa wachezaji wetu. Ni aibu mechi ipo Nairobi na hatuwezi kuujaza Uwanja wa Kasarana kuzipa sapoti klabu zetu zinapocheza mechi za kimataifa. Katika mchezo wa mwisho wa Gor Mahia, nilitarajia uanja ufurike lakini haikuwa hivyo. Lazima tuwaige wenzetu wa Tanzania kupanda soka letu. Lazima turudi viwanjani. Wachezaji wetu wanatutarajia viwanjani. Ni lazima. Popote ulipo unapisoma makala haya ujifikirie.

Utapata jibu. Tumekuwa na ushabiki wa mdomoni tu na Facebook na Twitter. hatufiki uwanjani. Aibu tupu. Tuache chocha. Watanzania nawavulia kofia ndugu zangu za Tanzania. Hongereni. Kando na hayo nawatakia mashabiki wote na timu ambazo zimefuzu kila la kheri.