Shoo ya Hazard Russia ni darasa kwa mastaa Bongo

Sunday July 8 2018

 

By BADRU KIMWAGA

KATIKA soka kuna wakati wachezaji wanapaswa kujitoa kwa sababu ya timu. Kama hakuna mchezaji anayejitoa, ni ngumu timu kufikia mafanikio. Tulishuhudia msimu uliopita kwa nyota wa Simba kujitoa kindakindaki na kubeba taji la Ligi Kuu.

Taji ambalo Simba imelisotea kwa miaka sita tangu ilipolibeba mara ya mwisho 2012. Emmanuel Okwi alijitoa. Jonas Mkude alijitoa. Aishi Manula langoni alijitoa. John Bocco kule mbele naye hakubaki nyuma, sawa na akina James Kotei, Asante Kwasi, Yusuf Mlipili na nyota wengine wa Msimbazi walioibeba Simba msimu uliopita.

Kule Azam vijana chipukizi, Shaaban Idd Chilunda, Paul Peter, Yahya Zayd, Himid Mao, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Razak Abarola walijitoa kwelikweli, hadi Azam inakamaliza ya tatu katika msimamo bila kutarajiwa. Ndio, kabla ya kuanza msimu Azam ilifanya mabadiliko fulani kikosini, ikiachana na kuruhusu mastaa wao wa muda mrefu

kuondoka kwenda Simba. Watu wakajua timi inaelekea kuzimu na mabosi wakajihami mapema kwamba wangetaka kushiriki tu ligi na sio kuwania ubingwa. Kilichotokea kilikuwa tofauti kadri msimu ulivyokuwa ukielekea ukingoni. Kina Chilunda na wenzake walikaza na kuishusha Yanga hadi nafasi ya tatu.

Kama umekiangalia kikosi cha Ubelgiji kilichotinga nusu fainali ya michuano ya Kombe la Dunia inayoelekea ukingoni kule Russia utagundua kitu.

Nahodha Eden Hazard amekuwa mhimili wa timu, anajitoa kiasi cha kushangaza. Ni tofauti na anavyocheza Chelsea, ni sawa Romelu Lukaku na Marouane Fellaini- Bakkioui. Lukaku na Fellaini wa kule Russia wakiwa na Ubelgiji sio wale wa Manchester United.

Hazard anajituma, anajitoa na kuisaidia timu ya nchi yake kiasi cha kuzitetemesha timu nyingine zilizopo Kombe la Dunia. Fuatilia mechi zao tangu hatua ya makundi mpaka hapa ilipofikia utajua namaanisha nini.

Hata katika mechi ya juzi dhidi ya Brazili, Hazard alikuwa wa daraja la mbali. Alikuwa anashuka chini kuchukua mipira na kuipeleka mbele, alikuwa akitoa pasi za kiwango cha kina Iniesta, alikuwa akipiga chenga na mashuti ya kina Lionel Messi na Cristiano Ronaldo na alikuwa akijituma kama N’Golo Kante wa Chelsea na Ufaransa yake.

Kwa namna alivyokuwa akicheza inamfanya kila shabiki kuwa na hamu ya kuona fainali iliyowahishwa ya Ufaransa na Ubelgiji zitakazokutana katika nusu fainali Jumanne hii.

Jinsi Hazard na nyota wenzake wa Ubelgiji na hata wa nchi nyingine wanavyojituma kuzibeba timu zao ni wazi kuna darasa linatolewa kwa wachezaji wa klabu zetu za Ligi Kuu na hasa zile kubwa zinazotumia mamilioni kuwasajili na kuwalipa.

Uliiona Yanga ya msimu uliopita? Ilikuwa na wachezaji wa kuhesabika waliojitoa uwanjani kuipigania timu. Ukimuondoa Papy Kabamba Tshishimbi, Andrew Vincent

‘Dante’, Hassan Kessy na Kelvin Yondani, waliosalia walikuwa wapo wapo tu!

Huwezi kuwalaumu sana, kutokana na hali halisi iliyopo ndani ya klabu hiyo kiuchumi na hasa tangu Bilionea Yusuf Manji kujiuzulu Uenyekiti, lakini wakati mwingine ni kama wachezaji wengi wa klabu hiyo hawakujitambua wapo Yanga kwa sababu ipi.

Obrey Chirwa hakuonyesha kama ni straika wa kimataifa, Ibrahim Ajibu na wengine walijitoa mwanzoni mwa msimu baada ya hapo walipoteza ramani na timu kutiririka toka kileleni kwenda chini na ni bahati tu ilimaliza nafasi ya tatu. Ingeweza hata kushuka daraja, kwa sababu ilipoteza dira kwelikweli kwavile mastaa wao walikausha.

Ndio maana nasema kile anachokifanya Hazard kule Russia kama mastaa wa timu zetu za Ligi Kuu wamemfuatilia, wanaweza kuiga kitu ili msimu ujao tushuhudie nyota wa klabu hizo wakizibeba timu zao badala ya kuridhika kulipwa mamilioni ya fedha tu.

Haiwezekani mchezaji anayetumainiwa na timu na kulipwa fedha nyingi kucheza mechi kama yupo kwenye bonanza, hajali wala kuumia na matokeo mabaya ya timu yake.

Hata kama Neymar wa Brazili amezingua kule Russia kwa kujiangusha na kushindwa kung’arisha nyota yake baada ya Messi na Ronaldo kuondoka mapema katika fainali hizo za Dunia, lakini huwezi kumbeza kwani bado alionyesha kitu fulani kwa timu yake.

Ndivyo nyota wetu wa VPL wanatakiwa kufanya wanapopewa nafasi katika vikosi vya kwanza kwa kujituma, kujitoa ili kuzipa timu zao matokeo, kama Hazard na wenzake walivyofanya makubwa kwa Ubelgiji na kuipeleka The Red Devils nusu fainali. Sio kitu cha ajabu tukisikia Jumapili ijayo wanaume hao wakabeba ndoo kama watavuka salama mbele ya Ufaransa.

Advertisement