STRAIKA WA MWANASPOTI : Sawa Gor Mahia ilifungwa, ila tumejifunza nini kwa Everton?

Muktasari:

Safari hii ilianza baada ya Gor Mahia kutwaa kombe la SportPesa ambalo hushirikisha timu zote zinazodhaminiwa na kampuni hiyo ya michezo ya kubahatisha ikiwamo Everton ambao ni mara nyingine wanacheza na Gor Mahia. Awali walicheza pale Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Juzi Gor Mahia ilipata nafasi murua kabisa ya kusafiri hadi Uingereza kupiga mechi ya kirafiki na klabu ya Everton inayoshiriki Ligi Kuu England. Ni safari itakayobaki vinywani mwa wachezaji wa Gor Mahia.

Safari hii ilianza baada ya Gor Mahia kutwaa kombe la SportPesa ambalo hushirikisha timu zote zinazodhaminiwa na kampuni hiyo ya michezo ya kubahatisha ikiwamo Everton ambao ni mara nyingine wanacheza na Gor Mahia. Awali walicheza pale Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Timu nyingine zinazodhaminiwa na kampuni hii ni Yanga, Simba na Singida United za Tanzania na AFC Leopards, Kakamega Home Boys na Gor Mahia za Kenya. Ni utaratibu uliowekwa na wadhamini ya kwamba, timu itakayoshinda michuano hii, atacheza na timu hiyo ya Ligi Kuu England na bahati hiyo imeiangukia Gor kwa mara ya pili mfululizo.

Hatimaye wachezaji wa Gor wakasafiri hadi Liverpool na kujifunzaq mengi kwa upande wa soka.

Kubwa walilojifunza ni soka hapa Afrika Mashariki tunacheza tu na tuko mbali sana kuweza kufikia hatua ilizofikia nchi za Ulaya kisoka

Nilibahatika kufanya mahojiano na mmoja wa wachezaji wa Kogalo juu ya safari yao hiyo na anavyoiona Everton.

Kwanza alicheka kisha akasema, ikiwa Everyone wako vile akiwa na maana ya kiwango cha soka, vipi hao Manchester United, Liverpool, Chelsea, Arsenal, Real Madrid, Barca na nyinginezo? Wako wapi kimaendeleo ya soka. Anasema hivyo kutokana na kuiona Everton ilivyo na maendeleo makubwa akiilinganisha na timu ambazo ni kubwa zaidi yake, hizo alizozitaja.

Everton ina viwanja zaidi ya kumi vya mazoezi, ina hospitali yake binafsi, eneo kwa ajili ya chakula ambapo wachezaji wote hukutana hapo baada ya mazoezi kwa ajili ya chakula.

Kuna madaktari wa kutosha na vyumba vya kupumzikia na kila kitu kinafanyika kwa utaratibu maalumu.

Hayo yote walijionea ambayo ni tofauti sana na huku kwetu. Pia kuingia uwanja wa Everton, sio rahisi kama huku kwetu. Ni lazima uwe na ruhusa maalumu kutoka kwa viongozi wa klabu na uwanja huo wa Goodson Park unatumika kwa mechi pekee.

Hata hivyo, wachezaji wa Gor walipata ruhusa ya kucheza mle kwa sababu wikiendi iliyofuata Everton ilikuwa inasafiri kwenda kukipiga na Chelsea, jijini London. Hili ni somo tosha kwa klabu zetu za Afrika Mashariki kutamani wapate nafasi ya kujiunga na timu hiyo au moja ya timu za ligi hiyo kubwa duniani.

Ni wazi wachezaji wa Gor walitamani kiusalia huko, sio wao tu hata wanasoka wengine wa ukanda huu wakienda huko, watatamani sana kuendelea kucheza huko.

Hoteli waliyofikia ni ya hadhi, uwanja waliofanyia mazoezi ni zaidi ya hivi vya kwetu vya mechi kubwa. Ni aibu tupu kwa ukanda huu na Afrika kwa jumla.

Ndio maana mara nyingi huwa nasema, inatakiwa tuanzie chini kutengeneza viwanja vyetu hasa vya mazoezi.

Naamini ukanda huu una vipaji vingi, tatizo ni ubinafsi umewajaa viongozi wetu na nyoyo zao zio za kuangalia maendeleo ya soka letu.

Wengi wao hawafahamu umuhimu wa soka na michezo kwa jumla. Hii ni aibu tupu kwa ukanda wetu huu.

Embu tujiulize, ni nani wa kumlilia ili angalau tuweze kufikia asilimia kumi tu za kile kilichofanyika pale Goodson Park? Hela zipo. Lakini shida Kubwa viongozi ndio hatuna. Waliopo wote hawafahamu lolote kuhusu michezo.

Ni juzi tu waziri wa michezo wa Kenya alifikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kufyonza hela za wanariadha. Sasa Kama waziri mwenyewe anakula hizo hela nani ataacha. Ni vigumu.

Hata hivyo, nawashukuru Sportpesa kwa kuwapa wachezaji wa Gor Mahia nafasi ya kueza kutembelea klabu ya Everton na kujifunza mengi ikiwa pia ndio klabu ya kwanza kutoka Afrika kutembelea Everton. Ni historia nzuri na changamoto kwao hasa wachezaji kujituma ili kuweza kufikia hatua waliyofikia wachezaji wa Everton.

Ndio maana nasema, kufungwa kwa Gor mabao 4-0 na Everton, kwangu sio hoja sana, kikubwa ni kipi wamejifunza? Hata hao viongozi wa klabu waliosafiri nao ni yapi wamejifunza?

Niwatakie siku nzema.