JAMVI LA KISPOTI : Samatta anapoutamani umri wa Chilunda, Mbappe

Muktasari:

Samatta anafikiri kama angewahi kwenda Ulaya kwa kasi anayoionyesha sasa ukizingatia ni msimu uliopita tu aliibuka kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Ubelgiji, basi wakati huu angekuwa katika soko kubwa kwa kuwindwa na hata klabu kubwa kama Real Madrid na nyingine za Ligi Kuu England.

MUDA ni kitu muhimu sana katika maisha hasa kama unatafuta mafanikio. Ukishindwa kuuheshimu muda hakuna malengo utakayoweza kufikia katika maisha yako.

Ili uweze kufanikiwa ni lazima utambue nafasi ya muda katika kila unalolipanga, unawezaje kuyafikia malengo yako na je, utawezaje kutumia muda vyema katika kuhangaika na unachotaka kukifanya.

Kwenye soka nako muda bado unahusika kwa wachezaji, makocha, viongozi na wakati mwingine hata mashabiki ambao wanasubiri kuona mafanikio ya makundi hayo matatu.

Jana Watanzania wengi macho yao yalikuwa katika televisheni wakimuangalia raia mwenzao, Mbwana Sammata akiendelea kuandika historia kwa kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika wakati klabu yake ya Genk ilipoialika Napoli ya Italia.

Licha ya Sammata kuandika historia hiyo baada ya kucheza mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Samatta aliandika kitu akijutia juu ya suala la muda. Anajiona kama alichelewa kwenda Ulaya na pengine hata safari yake ya kutoka katika mipaka ya Tanzania kwenda kucheza soka la kulipwa. Ukifuatilia alichoandika Samatta unaweza kumsikitikia kwani ni dhahiri majuto yake yako sahihi kwa kasi ambayo anaionyesha sasa hakuna shaka angekuwa katika ubora mkubwa kama angewahi kwenda Ulaya.

Samatta anafikiri kama angewahi kwenda Ulaya kwa kasi anayoionyesha sasa ukizingatia ni msimu uliopita tu aliibuka kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Ubelgiji, basi wakati huu angekuwa katika soko kubwa kwa kuwindwa na hata klabu kubwa kama Real Madrid na nyingine za Ligi Kuu England.

Wakati Sammata akijutia muda unakutana na taarifa kuwa mshambuliaji mwingine wa Tanzania, Shabani Idd Chilunda anarejea nchini akitokea Hispania alikokwenda kucheza soka la kulipwa. Chilunda yuko nchini akipigiwa filimbi za offside na kina Hamisi Chang’walu baada ya kurudi katika klabu yake ya zamani ya Azam FC.

Unaweza kujiuliza nini kilichomfanya Chilunda arudi Bongo, ukakosa jibu la maana. Ni kama ilivyokuwa kwa Athuman Abdallah China wa Yanga alivyoenda kucheza Ligi Daraja la Nne England. Ni kama ilivyokuwa kwa Haruna Moshi ‘Boban’ alivyoenda Sweden. Nafurahi nikimuona Farid Mussa akiendelea kukomaa pale Hispania. Samatta akiuangalia umri wa Chilunda anatamani kulia zaidi, kwani hicho ndio kitu kinachouumiza moyo wake kwa kuona amechelewa kwenda kusaka maisha Ulaya.

Elimu hii inaweza pia kuwa sahihikwa kinda kama Kelvin John ‘Mbape’ ambaye sasa yupo pale Genk akijaribu maisha yake.

John anatakiwa kutambua kilio cha Samatta ni mtaji mkubwa kwake ni umri alionao na kuhakikisha anajituma zaidi akiwa huko na asiamini kama kuna safari nyepesi katika maisha.

Milima ambayo John amaeonyeshwa na Sammata anayoitumia katika kujiweka sawa, ndiyo inatakiwa kuwa elimu yake kubwa akiwa huko na ikiwezekana kila anapokumbuka nyumbani, basi arudi katika milima hiyo na kujifua.

Chilunda ni mmoja tu kati ya wachezaji wetu wengi wanaopaswa kutumia umri wao vizuri. Wasidhani safari ya kuwika ukiwa Ulaya ni nyepesi kama ambavyo maisha yalivyo hapa Bongo. Maisha ya kufanya vyema Ulaya yana mapito mengi ambayo ili ufanikiwe lazima uvumilivu sambamba na kujituma katika jukumu lako.

Sifa hizi wengi wanazikosa na wakikikutana na changamoto kidogo tu hukumbuka kurejea nyumbani na sio kupambana kama ambavyo wachezaji wengi wa Afrika Magharibi wanavyofanya.

Samatta anatakiwa kugeuzwa kama elimu kwa wachezaji wetu wanaochipukia kuhakikisha wakipata nafasi ya kwenda nje, basi juhudi kubwa zinahitajika katika kupata kile walichokifuata huko hasa wakati huu ambao tumeanza kuona matunda kupitia kwa wachezaji wetu wanaocheza nje.

Vijana wanatakiwa kufanya uamuzi sahihi sasa. Umri ni kitu ambacho hakirudi nyuma hili ndio linalomtesa Samatta sasa anatamani angekuwa na umri kama John au Chilunda ili aweze kujituma zaidi na kuwa katika soko bora zaidi ya ilivyosasa.

Ikumbukwe katika soko lolote bora la Ulaya ukiondoa ubora husika wa mchezaji lakini jambo lingine muhimu linalopanga bei nzuri ya mchezaji basi ni umri wake.

Pengine hili linaweza kuwa kikwazo kwa Sammata kwani analazimika kupata ofa za kawaida kwani nafasi yake kiumri ingeweza kumpa fedha nyingi na kuhitajika katika klabu kubwa zaidi kama angekuwa na umri kama wa Chilunda na Mbappe kuliko sasa ambapo ana miaka 26 akibakiza miaka michache kuingia katika daraja gumu la kibiashara.