MTAA WA KATI : Sababu milioni za Los Blancos kuanza kujiunga upya

Muktasari:

  • Real Madrid hii haina kuleta sababu za VAR. Wala sababu za kulaumu mfumo. Sijui kulaumu uchovu na mambo mengine. Kwa maneno machache tu yenye usahihi. Real Madrid hali ni mbaya na wachezaji ndio shida.

REAL Madrid inatafuta pa kuegamia. Vichapo sita kwenye mechi 18 ilizocheza kwenye La Liga si habari nyepesi.

Haiwezi kuwa ile Real Madrid inayofahamika na wengi. Luka Modric amejaribu kuwa mkweli.

Real Madrid hii haina kuleta sababu za VAR. Wala sababu za kulaumu mfumo. Sijui kulaumu uchovu na mambo mengine. Kwa maneno machache tu yenye usahihi. Real Madrid hali ni mbaya na wachezaji ndio shida.

Kocha Solari anajaribu kurahisisha mambo akidai shida ni kufunga. Nahodha Sergio Ramos analiondoa tatizo kwa wachezaji na kuwalaumu marefa. Kila mmoja anajaribu kusema analoona linafaa.

Lakini jambo moja tu, kipigo cha kutoka kwa Real Sociedad kinafichua shida nyingi kwenye kikosi hicho cha Los Blancos. Kwa sasa imeshuka zaidi kwenye msimamo hadi nafasi ya tano na imeachwa pointi 10 na mahasimu wao, Barcelona. Utashangaa, Real Madrid imezidiwa hadi na Alaves. Nani alaumiwe? Wenye hoja dhaifu, watakwambia kisa Cristianno Ronaldo.

Kweli sababu za Madrid kufanya vibaya ni Ronaldo? Sitaki kuamini hilo. Shida wachezaji wengi wa Madrid wamevimbiwa mafanikio. Mataji matatu mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, michuano yenye hadhi kubwa kabisa kwa ngazi ya klabu huko Ulaya, inatosha kuwafanya wachezaji hao wajiona hawana sababu tena kupigania kitu cha zaidi.

Wachezaji wana vipaji vikubwa tu, lakini shida hakuna tena kupambana. Julen Lopetegui alionekana hafai, lakini Solari naye hafai pia. Wachezaji wamepoteza ile njaa. Ramos hana kitu kingine cha kutafuta na sasa anacheza tu kusubiria mafao yake. Nini sababu, Zinedine Zidane? La, haiwezi kuwa shida. Kwa ilipofikia Real Madrid, Zidane asingekuwa na kitu cha ajabu kufanya kwenye timu hiyo tena.

Jambo ambalo Madrid inapaswa kulifanya kwa sasa. Kitu ambacho Florentina Perez anapaswa kufanya kwa wakati huu ni kufungua milango ya kundi kubwa la wachezaji waliopo waondoke. Anahitaji kubaki na watoto kama Vinicius Junior, Dani Ceballos na wengine. Anahitaji kuleta mastaa wengine wapya wasiopungua wanne, ili kuja na dhana tofauti katika kuhakikisha timu inarudisha njaa yake ya mafanikio. Anahitaji kuwa na beki wa kati mpya wa kiwango cha dunia. Viungo wawili wa maana na washambuliaji wawili matata. Anamhitaji Eden Hazard, anamhitaji Kylian Mbappe, anamhitaji Neymar. Anamhitaji Paul Pogba, anamhitaji John Stones.

Nawataja wachezaji hao kama mfano, kwa sababu ni wazi ni aina ya wachezaji ambao watahitaji kufanya kitu kikubwa watakapokuwa na jezi za Los Blancos kwenye miili yao.

Hazard atahitaji kuwa na Tuzo ya Ballon atakapotua Bernabeu. Neymar na Mbappe ni hivyo pia.

Hamu ya kufanya vizuri, ndiko kunakoleta faida kwa timu kwa ujumla wake. Ronaldo alikuwa mnyama kwenye kikosi hicho cha Bernabeu. Lakini, kubwa ni ule upinzani wake kutoka kwa Lionel Messi.

Kila kilichobora alichofanya Messi huko Barcelona, basi Ronaldo alihitaji kufanya vizuri zaidi. Haukuwa upinzani wa wazi, lakini ulikuwa ukileta afya kwenye vikosi hivyo viwili.

Vita yake binafsi na Messi, ilimfanya Ronaldo awe mtu muhimu kwenye kikosi cha Madrid. Lakini, kwa sasa hakuna kitu kama hivyo. Isco, Bale na Asensio wanacheza tu na hawaonekani kuwa na uchu wa kufanya jambo la kushindana.

Lakini, hao ni watu waliopo kwenye orodha ya wachezaji unaoweza kusema wameshiba mafanikio. Real Madrid inahitaji kuanza upya na waungwana husema, kuanza upya si ujinga.