SIO ZENGWE: Watu wa soka wasisubiri kudra za Mola

Monday April 27 2020
SOKA PIC

Kwa kuangalia uamuzi wa Serikali kuzuia shughuli za mikusanyiko kwa muda usiojulikana, unaona kabisa kuwa hakuna uwezekano wa Ligi Kuu ya soka na hata mashindano mengine kuendelea katika siku chache zinazokuja.

Michezo, kama zilivyo shughuli nyingine zinazokusanya watu wengi, imezuiwa kwa muda usiojulikana katika jitihada za kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19 ambao ushaua zaidi ya watu 200,000 kote duniani na kuambukiza zaidi ya watu milioni 2.8.

Mikusanyiko ni kati ya vitu vinavyowezesha maambukizi kusambaa kwa kasi na hivyo uamuzi wa kuizuia ni sahihi kabisa katika kuliokoa taifa na ugonjwa huo ambao hadi sasa haujapata tiba wala chanjo.

Lakini hatuwezi kutulia na kuachia mambo yaendelee kama yalivyo eti kwa sababu tunasubiri mwongozo wa Serikali ndipo tuamue nini cha kufanya. Lazima tuwe tunachukua hatua kwa sasa kujiweka tayari kwa suala lolote linaloweza kutokea.

Tayari Ligi Kuu ya England imeshakutana na kuweka taswira tofauti kusubiri uamuzi wa serikali yao. Yaani kama serikali ya Uingereza itaamua kulegeza masharti ya kuzuia watu kutembea, basi Ligi Kuu ya England inaweza kuendelea mwezi Juni kwa kushirikisha viwanja vichache na bila kuruhusu mashabiki uwanjani.

Taswira nyingine inaweza kuangalia kama makatazo hayo yataisha mwezi Juni au Julai, ili ijulikane kwamba iwapo makatazo yatakaribia muda wa msimu ujao kuanza, basi msimu wa mwaka huu ufutwe bila ya kuwepo na timu inayotwaa ubingwa wala kushuka daraja.

Advertisement

Hivi ndivyo ambavyo Bodi ya Ligi na klabu wanatakiwa kukutana na kujadili taswira tofauti kulingana na mazingira ya mafanikio ya kudhibiti Covid-19 mapema au kwa kuchelewa sana.

Yaani hadi sasa Shirikisho la Soka (TFF) limesema iwapo Serikali italegeza masharti, basi Ligi Kuu itaendelea bila ya mashabiki. Lakini hiyo ilikuwa wakati Serikali ilipozuia mikusanyiko kwa muda wa siku 30, hivi sasa ni kwa muda usiojulikana. Nini kinafanyika?

Ni kikao cha pamoja baina ya TPLB, TFF na wadau wengine kufanya uamuzi mapema ili Serikali ikitoa tamko inakuwa inajulikana kuwa kwa tamko kama hili, hiki ndio kinafanyika na hivyo hata klabu, waamuzi, makamisaa wanaanza kujipanga kulingana na mikakati iliyowekwa.

Pia kuna mdau muhimu, mdhamini, ambaye ili apange mikakati yake vizuri ni lazima ajue wenye mpira wamejipangaje kulingana na hali iliyopo. Je, aandae watu wake kwa ajili ya kuendelea na shughuli za kusisimua udhamini wake mara mechi zitakapoanza au aondoe kabisa katika shughuli anazopanga kufanya wakati mwaka utakapogeuka.

Mwingine muhimu ni mtangazaji wa mechi hizo, yaani Azam TV. Akae anasubiri tamko la Serikali au ajiandae kumalizia ligi kulingana na mikakati ambayo wenye mpira wameiweka. Na maandalizi yana mambo mengi, hasa fedha za kufanikisha mipango yote.

Hata klabu zinatakiwa zijue ili makocha wabadilishe program za mazoezi kulingana na muda wa kuendelea na ligi unavyokaribia au unavyochelewa.

Kwa hiyo ni muhimu sasa TFF, TPLB na wadau wengine kuweka mikakati, yaani Plan A kama makatazo ya Serikali yataisha Mei, au Plan B kama makatazo ya Serikali yataisha Juni na Plan C kama makatazo yatakwenda hadi kipindi ambacho msimu mpya unatakiwa kuanza.

Huu si wakati wa kutulia na kusubiri kudra, bali kuanza kujipanga kulingana na kudra hizo zitakavyokuja. Kama Mola akiziwahisha, basi tuwe tayari na kama akizichelewesha, basi tujue tutatumiaje kipindi hicho kirefu kabla ya michezo kuendelea.

Advertisement