Si Ajibu na Erasto tu, hata Ambokile hajaitwa Stars

Monday October 1 2018

 MCL

By EDO KUMWEMBE

NYAKATI za maswali kutoka kwa Watanzania kuelekea kwa Taifa Stars. Nyakati hizi zinakuja wakati mwanga unapoanza kuchomoza kwa Taifa Stars. Kama ilivyo sasa hivi wakati inapoanza kuzungumzwa kuwa Stars inaweza kufuzu kwenda Afcon 2019 pale Cameroon.

Mashabiki na mabosi wa klabu za Simba na Yanga wanaanza kunong’ona. Kwanini Ibrahim Ajib hajaitwa katika kikosi cha Taifa Stars? Wengine wanauliza kwanini Erasto Nyoni hajaitwa? Wanamuhoji kocha, Emmanuel Amunike.

Jibu la kwanza, Amunike ana maamuzi ya mwisho. Ni mwendelezo uleule wa makocha waliopita. Majibu mengine naanza kukisia mwenyewe. Naanzia kwa Ibrahim Ajibu Migomba. Ni fundi wa mpira.

Ajibu amechipuka katika mechi tatu zilizopita. Amepika mabao mazuri kwa Yanga. Kabla ya hapo aliamua kutong’ara. Hii ni kwa sababu Ajibu anacheza kwa kujisikia. Sijui kwanini ameamua kucheza vema nyakati hizi. Labda mkataba wake unakaribia mwisho. Hauwezi kujua.

Mchezaji wa aina hii anatufanya tumuachie kocha mwenyewe aamue. Mara nyingi wachezaji wanahitaji mwendelezo wa ubora katika kuitwa kikosi cha Stars na sio ubora wa mechi tatu. Hasa katika timu ambayo haujawahi kuifanyia makubwa.

Kwa mfano, wote tunajua Thomas Ulimwengu hajafikia ubora wake, wakati ule Taifa Stars ikiichapa Morocco 3-0 pale Taifa. Baadaye alikuja kuumia goti lake. Akakosa dili la Ulaya lakini sasa anarudisha ubora wake taratibu pale Sudan.

Anastahili kuwepo Stars kutokana na uzoefu wake (exposure) katika mechi za kimataifa. Lakini pia kuna kitu aliwahi kukifanya. Inawezekana Kocha Amunike aliwahi kuiona mikanda yake au anajua faida ya kuwa naye kikosini kwa sababu kabla ya hapo Amunike alikuwa Sudan.

Vitu alivyofanya Ajibu mechi tatu zilisopita inabidi avifanye wiki hadi wiki kuweza kupata uhalali wa kujihakikishia nafasi katika kikosi cha Taifa Stars. Mbona mashabiki hawajiulizi kwanini Eliud Ambokile wa Mbeya City hajaitwa Taifa Stars wakati yeye na Meddie Kagere wanaongoza kwa kufunga mabao Ligi Kuu?

Erasto Nyoni, kwangu ni fundi wa mpira. Huwa nawaambia watu, Nyoni ndiye mchezaji anayejua kuuchezea mpira kuliko wote hapa nchini. Kwanini Amunike hajamuita katika kikosi? Sijui lakini nina mawazo yangu binafsi.

Kama Erasto anaitwa katika kikosi kama beki wa kati, basi ana kazi kubwa ya kumshawishi kocha kutokana na shoka lililopigwa na Aggrey Morris na David Mwantika katika mechi dhidi ya Uganda. Wanaonekana kucheza kwa kutumia nguvu zaidi (aggressiveness) na wanatawala mipira mingi ya hewani.

Kocha aliamua kuchagua nani mwenye vurugu zaidi kati ya Kevin Yondani na Erasto akaamua kwenda na Kevin. Kwa walichoonyesha Mwantika na Morris dhidi ya Uganda dhidi Amunike ataamua kubadili kikosi chake. Wataungana na Abdi Banda kucheza mabeki watatu katika eneo la katikati.

Erasto atakuwa mzuri zaidi katika mechi ambazo tutatawala mechi. Nadhani Amunike anaamini aina ya mechi ya Cape Verde itakuwa vilevile kama ya Uganda. Unahitaji wachezaji wababe zaidi uwanjani.

Shiza Kichuya utata wake ni mdogo kwa sababu hata mashabiki wa klabu yake wanajua hajakuja vizuri sana msimu huu kuliko msimu uliopita.

Tukiachana na haya pengine ni wakati wa kujiuliza, mbona wachezaji walioitwa ni wazuri? Wakati mwingine napata shida sana kukubali kikosi cha mwalimu kama amewaita wachezaji wa kawaida halafu akawaacha wachezaji wazuri.

Lakini ukitazama kikosi cha Stars cha sasa kimesheheni wachezaji wengi wenye uwezo. Mchezaji shoka kama Himid Mao alianzia benchi pambano la Uganda. Na ni mchezaji anayecheza soka la kulipwa panga pangua katika kikosi cha Petrojet Ligi Kuu ya Misri.

Kama unamrudisha Jonas Mkude kikosini halafu Mudathir Yahaya na Frank Domayo bado wapo kikosini sidhani kama tuna viungo wengi wa maana walioachwa nje ya kikosi. Tatizo bado tutalalamika kwa sababu ya Usimba na Uyanga.

Lakini pia tukumbuke wachezaji wetu nao wanahitaji bahati kuwepo kikosini. Ukipewa nafasi yako unapaswa kuitumia. Kuna wachezaji wengi wazuri nchini. Sio lazima wawe wanatoka Simba na Yanga. Bahati nzuri kwao waliitwa kwa ajili ya kuchukua nafasi za wachezaji wa Simba na Amunike anaonekana kuwapenda kwelikweli.

Hawa kina Kevin Sabato, Mwantika, Salum Kimenya, Paul Ngalema na wengineo wote wamerudi. Ni wachezaji wazuri. Na pia tukumbuke kocha ni mpya na bado yupo katika mchakato wa kupata wachezaji wake anaowapenda yeye kwa mfumo wake.

Lingekuwa jambo zuri kama angemkuta Ajibu akiwa ameitwa kikosini kwa sababu alipofika hakumjua Ajibu wala Mbwana Samatta. Hilo lingemsaidia kumjua Ajibu mazoezini. Lakini pia angewakuta kina Nyoni katika mazoezi ya Stars si ajabu asingemjua Mwantika mpaka baadaye. Kwa sasa tuheshimu mawazo ya kocha.

Advertisement