MTAA WA KATI : Ramsey na kisa cha mrembo anayejipodoa

Muktasari:

  • Arsenal usiku wa jana Jumatatu walitarajia kumenyana na Watford. Ni mechi ngumu hasa ukizingatia rekodi zao wanapocheza ugenini msimu huu.

LIVERPOOL wamerudi kileleni tena kwenye Ligi Kuu England baada ya kuwaachia Man City kwa muda tu. Ushindi wao dhidi ya Chelsea umeondosha maana yote ya ushindi wa Man City kwa Crystal Palace.

Pengo lilelile la pointi mbili limeendelea kuzitofautisha timu hiyo kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Chelsea sasa ameweka rehani nafasi yao kwenye Nne Bora kwa sababu Arsenal kama watakuwa ameboresha matokeo yao ya ugenini na kushinda, basi watawaondoa kwenye hizo nafasi nne za juu.

Arsenal usiku wa jana Jumatatu walitarajia kumenyana na Watford. Ni mechi ngumu hasa ukizingatia rekodi zao wanapocheza ugenini msimu huu.

Arsenal kwenye mechi zao 15 walizocheza ugenini msimu huu, wameshinda tano tu. Wamefungwa sita na wametoka sare mara nne.

Kocha Unai Emery amekuwa aking’ang’ania fomesheni yake ya 3-4-2-1, ambayo wanapocheza nyumbani imekuwa na msaada mkubwa ila wanapokuwa ugenini mambo yanakuwa tofauti. Bila shaka Emery atalifanyia kazi hilo na kubadilika.

Tuachane na hilo, tuje kwenye mjadala wetu wa leo kijiweni kwetu. Mjadala ni kuhusu Aaron Ramsey. Ukweli Ramsey anatushanga.

Anatushangaza kwa kiwango chake. Hana tofauti na mrembo anayejipamba zaidi akiwa anaelekea kwenye sherehe ambayo atakutana na mpenzi wake wa zamani. Hivi ndivyo Ramsey anavyowafanyia Arsenal kwa sasa.

Hivi ni kweli angekuwa kwenye kiwango hicho cha sasa kama asingekuwa na mpango wa kuachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu? Ramsey anataka kuwaonyesha Arsenal kwamba wanaachana na chuma.

Anawafanya Arsenal wajutie uamuzi wao wa kutombakiza. Ukweli kiungo huyo kwa sasa anacheza soka la ubora wake. Msimu ujao hatakuwa kwenye kikosi hicho.

Anakwenda zake Juventus, ambako amesaini dili la maana kabisa. Ramsey ana mambo mawili. Jambo la kwanza anataka kuwafanya Arsenal wajutie kumuacha. Hakika wanajutia kwa sasa. Lakini, jambo la pili kuwafanya Juventus kuwa na hamu ya kumpokea mchezaji wao haraka.

Anawapa hamu wababe hao wa Italia aende haraka akakipige kwenye kikosi chao na wasianze kufikiria dili lake la mapema walilosaini kumfanya awe mmoja wa wachezaji wanaolipwa mshahara mkubwa huko kwenye Serie A.

Hivi ndivyo maisha yanavyohitaji kuwa mjanjamjanja. Amemfanya kocha Emery asithubutu kumwondoa kwenye kikosi licha ya kwamba ana miezi miwili tu iliyobaki ya kucheza kwenye kikosi chake.

Anawachongea mabosi wake waliomruhusu aondoke. Pengine mabosi hao kwa sasa watakuwa wanamlaumu Emery kwa kumpa nafasi ya kucheza.

Lakini, Mhispaniola huyo atathubutu vipi kumweka benchi mchezaji ambaye anamletea matokeo mazuri ndani ya uwanja?

Emery anafahamu wazi usalama wa kibarua chake upo kwenye matokeo ya uwanjani. Kutokana na hilo atafanya kila kitu katika kuhakikisha anapata matokeo chanya uwanjani hata kama kwa kumtumia mchezaji ambaye bila ya shaka atakuwa anawachongea wengi kama vile Ramsey. Staa huyo wa Wales anafanya makusudi.

Kwa nini hakuwa kwenye ubora wake huo wakati alipokuwa kwenye meza ya mazungumzo na Arsenal kuhusu mkataba mpya?

Kwa nini wakati ule hakuwa kwenye ubora mkubwa kuwashawishi mabosi wake kutokuwa na hofu juu ya mshahara aliokuwa akitaka kulipwa?

Amesubiri hadi hapo alipomalizana na Juventus, akaanza kuonyesha ubora wa soka lake. Juve wao wala hawakuona ugumu wa kumpa mshahara mkubwa kwa sababu kwanza wanampata bure.

Hawajalipia chochote, hivyo ni gharama yao ni kumlipa mshahara tu. Na hakika kwa Ramsey huyu wa sasa Juventus wamenasa bonge la mchezaji kama atakwenda kucheza soka lake la kiwango hicho huko Turin.

Ramsey anaonekana kuufahamu vyema mfumo wa Emery na hakika atamwaacha kocha huyo kwenye matatizo makubwa ya kuziba pengo lake huko Emirates.