TASWIRA YA MLANGABOY : Phiri alisema Samatta ni dhahabu, kuna mtu ana swali!

Muktasari:

Nakumbuka baada ya mazoezi nilikwenda hotelini ilipofikia Simba na kuzungumza na kocha Phiri, kubwa ni kujua kipi amekiona kwa Samatta na Gumbo kiasi cha kuwapa nafasi mbele ya wakongwe.

MWAKA 2010, nilipata bahati ya kusafiri na kikosi cha Simba wakati huo kilikuwa kinakwenda mjini Songea kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Majimaji.

Wakati huo Simba ilikuwa chini ya kocha Mzambia Patrick Phiri aliyefanikiwa kutengeza kikosi chake bora, na kulikuwa na vijana wawili waliokuwa wanaibukia.

Vijana hao waliokuwa wanaibukia na kutishia namba za wakongwe wa wakati huo Nico Nyagawa na Mussa Mgosi, walikuwa kiungo Rashid Gumbo na mshambuliaji Mbwana Samatta.

Samatta ndiyo alikuwa amejiunga na kikosi baada ya kumaliza mgomo wake wa kushinikiza apewe gari aliloahidiwa na viongozi wake wakati akisaini mkataba wa kujiunga na Wekundu wa Msimbazi akitokea katika klabu ya African Lyon, ili achezee timu hiyo.

Wadau wengi na mashabiki walimshangaa mchezaji chipukizi ambaye ndiyo kwanza anaibukia anagoma kucheza Simba akishindikiza kupewa kwanza hitaji la mkataba wake.

Jambo hilo lilinifanya nitamani kumfahamu zaidi kwa sababu ni vigumu kwa mchezaji anayeibukia akiwa ndiyo kwanza amesajiliwa na klabu kubwa kama Simba anagoma kucheza na uongozi wake unatetemeka, nikajua kuna kitu cha zaida.

Hata hivyo, nakumbuka kwamba Samatta ndiye mchezaji aliyeweka rekodi ya kufunga mabao 14, katika msimu moja wa Ligi Daraja la Kwanza akiwa na Mbagala Market.

Nikasema kama mchezaji amefunga mabao 14, Ligi Daraja la Kwanza basi Simba wanayo haki ya kupambana kutaka huduma yake, pia mchezaji anayo haki ya kuringa kwa sababu miguu yake inaongea yenyewe.

Nakumbuka baada ya mazoezi nilikwenda hotelini ilipofikia Simba na kuzungumza na kocha Phiri, kubwa ni kujua kipi amekiona kwa Samatta na Gumbo kiasi cha kuwapa nafasi mbele ya wakongwe.

Mzambia Phiri aliniambia Samatta na Gumbo kwake ni sawa na mtu aliyeokota dhahabu chafu anayohitaji kuisafisha na kuiweka sokoni kusubiri kupiga pesa ndefu.

Phiri alitimiza wajibu wake wa kuisafisha dhahabu hiyo kwa kuhakikisha anawatumia vijana wake Samatta na Gumbo kwa kuwapa nafasi ya kucheza katika kikosi chake.

Siku zote maisha hayawezi kuwa sawa, Gumbo bahati mbaya maisha yake ya soka yamekatika mapema, alikwenda Yanga, baadaye nikasikia ametafuta timu nje ya nchi, lakini kwa ufupi maisha yake ya soka yamemalizika mapema.

Gumbo ameshindwa kuishi ndoto za Phiri, lakini wakati yeye akipotea Samatta amethibitisha kweli alikuwa ni dhahabu chafu iliyohitaji kusafishwa kufikia malengo.

Samatta alitua TP Mazembe alimkuta mfalme pale Tressor Mputu Mabi na nyota wengine kibao, lakini alikubali kujiunga na miamba hiyo na kukataa kubaki Msimbazi.

Hakuna ubishi kwamba Samatta alionyesha kwamba yeye ametumwa kufanya kazi. Akitaka kuthibisha kwamba yeye ni dhahabu aliendelea kupita katika moto ili kuwa bora na kuongeza thamani yake ndani na nje ya uwanja.

Pamoja na kuonyeshwa mapenzi makubwa kutoka kwa bilionea Moses Katumbi, lakini Samatta alikataa kuuzwa asipotaka na tajiri huyo aliyekuwa na lengo la kumpeleka Ufaransa.

Samatta aligoma kuondoka kwenda Ufaransa kwa sababu alijua yeye ni dhahabu inayoweza kuuzika kokote pale, ndipo akasubiri mkataba wake ulipokwisha akaondoka na kujiunga na Genk ya Ubelgiji.

Ubelgiji Samatta alianza chini akifunga mabao matano tu katika mechi 18 za mwanzo ndani ya klabu ya Genk. Aliendelea kujituma na kuonyesha thamani yake kiasi cha kupewa jezi namba 10.

Ametimiza ndoto yake ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu amechukua mpunga wake wa kutosha kwa kushiriki mashindano hayo, amechukua ubingwa wa Ligi Kuu Ubelgiji na amekuwa mchezaji bora.

Vyote ambavyo mchezaji anatamani kupata amepata, miaka inakwenda kasi, ndoto kubwa zaidi ni kucheza Ligi Kuu England ameitimiza japokuwa Aston Villa haipo katika nafasi nzuri.

Hakuna ubishi Samatta ni dhahabu. Ataonyesha hilo kwa kuhakikisha anaisaidia Aston Villa kufika katika fainali ya Kombe la Ligi endapo ataisaidi kushinda kesho Jumamosi dhidi Leicester City.

Kama Aston Villa atatwaa ubingwa huo itapata tiketi ya kucheza Europa Ligi. Katika mpira hakuna linashindikana, lakini kubwa ni kuishi kwa kauli ya Phiri kwamba Samatta ni dhahabu.

Naamini uwezo wake kwa kushirikiana vema na wenzake Aston Villa inaweza kujiepusha na janga la kushuka daraja, lakini pia kiwango chake kinaweza kumfanya apate timu nyingine ya Ligi Kuu England hata kama Villa itashuka daraja.

Hongera Samatta umeonyesha inawezekana kwenye nia, naamini kinda wetu amayekuja vyema katika soka la Tanzania, Kelvin John akijituma na nidhamu atafikia ulipofika.

Na si kwa Kelvin John peke yake. Vijana wengine wanaofuata nyayo za Samatta wanapaswa kuutumia mfano wa ‘Champion Boy’ huyo katika kuzifikia ndoto zao.