Breaking News
 

ROHO NYEUPE: Pesa za Singida, Azam zilivyotuletea mechi kali

Friday January 12 2018Gift  Macha

Gift  Macha 

By GIFT MACHA

HADI kufikia Jumatatu ya wiki hii Simba ilikuwa imeshatupwa nje ya Kombe la Mapinduzi. Juzi Jumatano kabla ya jua kuzama, Yanga nayo ilitolewa kwenye mashindano hayo. Inashangaza sana.

Kinachochekesha ni kwamba aliyeitoa Simba ndiye aliyeitoa Yanga. Ni URA kutoka Uganda, moja ya timu zinazocheza kwa nidhamu katika mashindano haya mwaka huu. URA haichezi soka safi sana, ila ina mbinu sahihi na utulivu mkubwa.

Kwa soka la Tanzania, Simba na Yanga zikitolewa kwenye mashindano tu, huwa ndiyo mwisho wa mashindano. Kama ingekuwa miaka ya nyuma, basi kwa matokeo ya Jumatano jioni, ingekuwa ndiyo mwisho wa msisimko wa Kombe la Mapinduzi. Kama Simba na Yanga zimeshatolewa, ungetulia sebuleni kwako kutazama mechi gani tena? Tanzania hakukuwa na mechi kali ambayo Simba na Yanga hazichezi. Ndiyo imekuwa hivyo kwa miaka nenda rudi. Lakini juzi ilikuwa tofauti. Baada ya Yanga kucheza soka la hovyo jioni, usiku wake pesa zilitupatia soka safi na la kusisimua. Kulikuwa na mechi kali ya Singida United na Azam. Nani alitamani kuacha kuitazama mechi ile?

Pesa zimeongeza msisimko katika soka la Bongo. Kwa sasa sio lazima tena utulie na kuzitazama Simba na Yanga ili upate burudani. Singida na Azam zinakupa mechi kali zaidi. Inatia moyo sana.

Kwa waliotazama michezo ya Mapinduzi, watakubali baada ya ile mechi ya Simba na Azam, mechi nyingine kali ilikuwa juzi Jumatano usiku kati ya Singida United na Azam. Lilichezwa soka la kuvutia mno.

Singida ilikuwa bora zaidi japo ilipoteza mchezo. Ilishambulia, ilitengeneza nafasi nyingi zaidi na ilipiga mashuti mengi zaidi. Tatizo washambuliaji wake; Danny Lyanga, Lubinda Mbia na Papy Kambale hawakuwa siriazi na kazi yao ya kufunga. Deus Kaseke naye alikuwa mchoyo.

Singida ingeweza kushinda mapema zaidi, kabla hata Shaban Iddi aliyekwenda kuifungia Azam bao pekee la ushindi hajaingia. Bahati mbaya mambo hayakuwa hivyo.

Hata hivyo, Azam nayo ilikuwa vizuri. Ilikuwa makini katika kujilinda. ilifahamu inacheza na Singida yenye washambuliaji bora. Ilijua kabisa Singida ingepata bao muda wowote.

Nidhamu ya kukaba ya Azam na mbinu yao ya kushambulia kwa nafasi ndiyo iliwabeba. Mwisho wa mechi, Singida ilikuwa imecheza soka safi, ila Azam ikashinda. Mpira wa miguu ndivyo ulivyo, muda mwingine hauna heshima.

Tukirejea kwenye hoja ya pili, soka la Tanzania sasa linapiga hatua. Ukiona mamilioni ya Watanzania wametulia sebuleni mwao na kutazama mechi ambayo haikuwa na timu za Simba na Yanga, ni hatua kubwa. Siku zote tulihitaji kufika hapa. Tulitahitaji kuwa na timu nyingine bora nchini. Tulihitaji kutazama mechi nyingine bomba ambayo Simba na Yanga hazihusiki.

Soka la kisasa linahitaji pesa na Azam na Singida zimewekeza pesa. Timu hizo zina mastaa wa nje wenye viwango vya maana. Ulimtazama kwa makini kipa wa Azam, Razack Abalora katika mchezo huo na mingine ya Mapinduzi? Anakupa maana halisi ya mchezaji wa kulipwa.

Uliwatazama Michele Rusheshangoga na Shafiq Batambuze wa Singida United? Ni wachezaji mahiri. Ni wachezaji wanaokupa maana halisi ya soka la kulipwa. Haya ndiyo matumizi sahihi ya fedha.

Ilipoanzishwa Azam miaka 10 iliyopita na kulishika soka la Tanzania miaka minne tu baadaye, tuliona mkombozi mpya amekuja. Hakuna kificho, tangu Azam imeshika hatamu Ligi Kuu, Simba na Yanga zimetia adabu.

Baada ya Azam kuweka mizizi, tulihitaji tena timu nyingine ya maana. Ikaja Mbeya City na kupotea ghafla. Angalau sasa imekuja Singida United. Pesa imeutendea haki mpira wetu.

Natamani sasa kuona Singida inaanza kuzungumzia uwekezaji wa miundombinu kwani uwanjani sasa imekuwa tamu. Natamani kusikia inajenga hosteli na uwanja wake. Timu bora inahitaji kuwa na nyumbani kwake, Namfua siyo kwa Singida.

Azam inatupa matumaini ya kuishi miaka mingi kwa kuwa imejiwekeza katika miundombinu. Ina uwanja wake wa mechi na mazoezi. Ina hosteli zake, gym, bwawa la kuogelea na vitu vingine vya maana kwenye soka.

Singida inahitaji kuwa na uwekezaji wa aina hii, vinginevyo itapotea bila kuacha alama yoyote. Kipindi cha nyuma zilikuja timu kali kama Singida na zikafa. Kulikuwa na Kajumulo, Twiga, Palsons, Moro United na nyinginezo, lakini zilikufa kifo cha mende. Timu zote hizo zilikuwa na jeuri ya fedha, lakini hazikujiwekeza na sasa zimepotea na hakuna hata anayezikumbuka.