Nusu fainali Kombe la Dunia, patawaka moto

Muktasari:

  • Mara ya kwanza kabisa miamba hii kukutana ilikuwa mwaka 1938 katika mchezo wa nusu fainali pia, fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Ufaransa na Ufaransa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, kwa mabao ya Emile Veinante, Jean Nicolas aliyepiga mawili, huku lile la Ubelgiji likifungwa na Rik Isemborghs.

FAINALI za Kombe la Dunia zimeingia hatua ya nusu fainali na sasa zimesalia timu nne tu kati ya timu 32 zilizokuwa zikiwania ubingwa wa michuano hii mikubwa tangu hatua ya makundi ilipoanza mwezi uliopita.

Baadhi ya miamba ya soka tayari imeshabanduliwa kuanzia hatua ya makundi ilipoanza Ujerumani mabingwa watetezi, zikafuatia Argentina, Ureno na Hispania huku wakiwaacha wenyeji Russia wakifika hatua ya robo fainali kabla ya kubanduliwa na Croatia. Uingereza, Ufaransa na Ubelgiji na Croatia ndio timu vigogo zilizobaki, Ufaransa ikimpiga Uruguay 2-0 katika mchezo wa kwanza wa robo fainali. Sasa inaenda kukutana na Ubelgiji katika nusu fainali.

Mara ya kwanza kabisa miamba hii kukutana ilikuwa mwaka 1938 katika mchezo wa nusu fainali pia, fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Ufaransa na Ufaransa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, kwa mabao ya Emile Veinante, Jean Nicolas aliyepiga mawili, huku lile la Ubelgiji likifungwa na Rik Isemborghs.

Hata hivyo, Ufaransa ilipoteza kwenye fainali dhidi ya Italia.

Mwaka 1986, timu hizi zilikutana tena kwenye Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Mexico na Ufaransa iliibuka na ushindi wa mabao 4-2 katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu kwenye Uwanja wa Estadio Cuauhtemoc Puebla.

Swali ambalo linabakia kwa vinywa vya watazamaji na mashabiki kote duniani. Je? Ufaransa wataendeleza huo mziki dhidi ya Ubelgiji?

Nikitazama kwa undani tu, timu zote zimejipanga vilivyo. Sioni mnyonge yoyote hapa ndugu zanguni. Ukitazama Ubeljiji ipo na nyota wengi sana ambao wanasakata soka kote duniani.

Thibaut Courtois anakipiga Chelsea, TobyAlderweireld (Tottenham), Vincent Kompany (Manchester City), Thomas Vermaelen (Barcelona), Nacer Chadli (West Brom), Romelu Lukaku (Manchester United), Eden Hazard (Chelsea) na kadhalika.

Ufaransa nao wana kikosi ambacho kila kocha duniani anakimezea mate. Hugo Iloris, Paul Pogba, Umtiti, Griezman, kinda Kylian Mbape, Olivier Giroud na kadhalika, wamo katika kikosi hicho. Ni wazi kila mtu anaisubiria kwa hamu mechi hii ya kibabe itakayopigwa Jumanne usiku.

Makocha Didier Deschamp, kocha wa Ufaransa na Thierry Henry, kocha msaidizi wa Ubelgiji walikipiga katika kikosi kimoja cha Ufaransa Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1998.

Sasa wanakutana uso kwa uso. Kazi iliyopo ndugu zanguni. Sisi watazamaji ni kubaki kushangilia tu.

Wakati huo huo, timu yangu ninayoshabikia ya The Three Lions nayo ilifuzu nusu fainali baada ya kuinyuka Sweden mabao 2-0, mabao ya Harry Maguire na Dele Alii.

Sasa England inaenda kukutana na Croatia iliyofuzu baada kuwanyamazisha wenyeji kwa mikwaju mitano mitano ya matuta wakipata mikwaju 4-3. England itakuwa na kibarua kigumu sana kwa Croatia ambao tangu michuano hii ianze wamekuwa wagumu sana. Gareth Southgate anajivunia mshambuliaji hodari, Harry Kane anayeongoza kwa kupasia nyavu huko Russia akiwa na mabao sita hadi sasa. Pia ana watu kama Raheem Sterling ambaye pamoja na Kane wataisaidia sana England katika mchezo huo wa Jumatano.

Hata hivyo, kazi kubwa kwa kikosi hicho cha Southgate itakuwa ni kumdhibiti kiungo matata wa Croatia, Luka Modric ambaye katika michuano hii ametesa sana

Croatia nao wana kazi ngumu ya kuwakaba wachezaji wa England hasa kuepuka mipira ya adhabu ‘hikabu’. Hapa England ni wazuri zaidi hivyo, tahadhari kwa Croatia wasisababishe England ikapata mipira hiyo, itakuwa hasara kwao.

Kati ya mabao 11 ambayo England yameifunga, mabao manane yanatokana na mipira ya hikabu. Swali ni je? Croatia itaweza kukabiliana na England katika mchezo huo.

Wakati huo huo, England haitakiwi isahau Croatia ni hatari, hasa kwa uwepo wa nyota wake kama Mario Mandzukic anayekipiga Juventus ya Italia, Ivan Perisic (Inter Milan), Ivan Rakitic (Barcelona) na Luka Modric (Real Madrid).

Hawa ni baadhi tu ya wachezaji wa kikosi hicho ambao England lazima kiwatolee macho bila hivyo safari yaoitakuwa imefikia mwisho.

Cha kujiuliza hapa ni, ni timu zipi kati ya hizi nne zitaingia fainali na ipi itanyakua taji hilo la dunia mwaka huu.

Bingwa mtetezi, Ujerumani kashaliacha kombe hilo, ni wazi bingwa atakuwa mpya.

Kati ya timu hizi nne, ni England na Ufaransa ndizo zilizowahi kulibeba mwaka 1966 na 1998 mtawalia.

Croatia na Ubelgiji hazijawahi na zinaonekana zimelipania hasa. Ufaransa na England zenyewe zinataka kuongeza hesabu na kuheshimika zaidi.

Nusu fainali hii, kitawaka unaambiwa. Tusubiri tuone.