TIMUA VUMBI : Nini kimeushika uwanja wa Simba Bunju?

Thursday March 14 2019

 

By Mwanahiba Richard

NI miaka mingi sasa tunaendelea kusoma na kuisikia historia ya uwanja wa Simba uliopo Bunju B nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, ukubwa wa eneo hilo ni zaidi ya ekari 20, upo sehemu nzuri ambayo ni tambalale huku ukizungukwa na makazi ya watu.
Uwanja huo ulinunuliwa tangu uongozi wa kina Hassan Dalali ingawa kuna historia nyingi juu ya ununuzi wa uwanja huo kwani baadhi hudai ulinunuliwa na Ismail Aden Rage lakini yote kwa yote unatambulika ni eneo la klabu ya Simba.
Washukuriwe viongozi waliopita na wale wote waliohusika kwenye mawazo ya ununuzi wa eneo hilo kwa klabu hiyo kongwe kuwa na eneo la kujenga uwanja wao, pengine hadi sasa hata eneo la kuzungumzia historia hii isingekuwepo.
Dalali na mwenzake Rage ambao waliongoza Simba kwa nyakati tofauti wakiwa Wenyeviti kabla ya Katiba kubadilishwa na kumtambua Mwenyekiti kama Rais ambayo pia imedumu kwa miaka minne pekee na sasa Katiba inamtambua Mwenyekiti baada ya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo.
Uongozi wa Simba ulianza harakati za  kujenga uwanja wa mazoezi kuanzia uongozi wa Rage wakati huo wanaelekea mwishoni kumalizia kuongozi kwa kipindi cha miaka minne waliajiri mkandarasi na nyasi zilipandwa na umwagiliaji uliendelea lakini ghafla uongozi mwingine ulipoingia madarakani ukasitisha kuendelea kuujenga uwanja huo ambao tayari ulianza kutumia pesa.
Sio pesa ndogo iliyomwagwa chini kwenye hatua hiyo ila nadhani viongozi wapya walijiamini kutengeneza kilicho bora zaidi ya kile cha awali ambacho sasa kinatumika na vijana wa mtaani kufanyia mazoezi.
Kabla ya hapo Simba ikiwa chini ya Rage, wanachama walijitolea kwenda kuufyeka uwanja huo hadi wakabatizwa jina la Kilimo Kwanza na Ezekiel Kamwaga wakati huo akiwa katibu aliongoza msafara huo wa wanachama wakiwa na majembe, mapanga na mafyekeo.
Simba ilianza mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji na sasa utaendeshwa kwa mfumo wa hisa baada ya mwekezaji Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’ kupita huku Katiba nayo ikibadilishwa kulingana na mahitaji ya klabu hiyo kwasasa.
Mo Dewji moja ya vipaumbele vyake ni kujenga uwanja wa kisasa wa mazoezi ambao ulianza kujengwa tangu mwaka jana na matarajio ya mkandarasi kuukabidhi ilikuwa ni Februari 15 mwaka huu, yaani mwezi uliopita.
Kabla ya tarehe husika kufika, Mo Dewji alitangaza sababu zinazowakwamisha hadi sasa kuwa ni nyasi zao kuzuiwa hivyo wanasubiri hatima itakayofuata.
Hata hivyo, kitu pekee cha kujiuliza ni Simba inakwama wapi kuendelea na mambo mengine ambayo yamepangwa kufanyika kwenye uwanja huo kama kujenga vyumba vya kubadilishia nguo, vyoo na mabafu yaani vile vitu muhimu vinavyopaswa kuwepo kwenye eneo hilo.
Ni kweli Mo Dewji alipata matatizo makubwa lakini kwa taarifa za awali ambazo ziliwekwa wazi na mkandarasi, kila kitu kilikuwa kimeandaliwa na  kazi ilibaki kwao tu ingawa baadaye suala la nyasi limeibuka.
Uwanja huo tayari umewekwa mabomba ya kunyonya maji mvua ikinyesha na miundo mbinu mingine inayohitajika kwenye hatua ya awali lakini sasa umeanza kugeuka kama kichaka kama ilivyokuwa hapo awali.
Ni gharama zingine ambazo Simba watapaswa kuzitumia siku watakapopata nyasi zao ambapo haijafahamika kwamba itakuwa lini kwani hivi sasa wanaonekana kuwa ‘bize’ sana na mechi za makundi Ligi ya Mabingwa Afrika hivyo mambo mengine ya nje ya uwanja huenda yamewekwa kando.
Hata wakimaliza hatua hiyo ambapo watacheza mechi ya mwisho keshokutwa Jumamosi dhidi ya Vita napo watakuwa ‘bize’ kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu yaani mambo yanapandana tu ndani ya Simba.
Ila kwa umoja wao pasipokutegemea nguvu ya mtu mmoja, wangeweza kujikusanya japo kupata pesa ya kununua nyasi nyingine kama hizo za awali zinazodaiwa kuzuia bandarini kwani haieleweki watapewa lini.
Kama wataendelea kusubiri hizo nyasi basi uwanja huo utasahaulika kabisa ama tutaendelea kuandika histori ya uwanja usiokalimika kila mwaka mwaka ama miaka na itaonekana kuna jambo lililoshikilia uwanja huo usikamilike kila hatua nje ya kuzuiwa kwa nyasi zao.

Advertisement