Nilipenda Bocco awe mbabe lakini sio vile

Muktasari:

Bocco ameweka rekodi ya kufunga bao lake la 100 katika Ligi Kuu Bara tangu aanze kucheza 2007

Dar es Salaam. JOHN Bocco ni mshambuliaji hatari na mnyonge kwa mabeki. Ni mnyonge kwa sababu ni mpole kwa asili, ndani na nje ya uwanja. Hana maneno mengi na anazingatia anachofanya uwanjani na hata nje ya uwanja sio mtu wa maneno.
Walinzi wengi wanamuonea Bocco na kuna wakati niliandika hapa kwamba Bocco anahitaji kuwa mbabe. Wengi wanauchukulia upole wake kama unyonge. Wanamfanya watakalo na wakati mwingine tumeona picha za kumdhalilisha zaidi.
Hawa akina Kevin Yondan, Juma Nyosso, Kassim Chona na wengineo huwa wanamtembezea Bocco ubabe usio na maana. Bocco anawakera kwa sababu anajua kufunga na ana urefu ambao unamfanya awamudu kwa mipira ya hewani.
Zamani tulikuwa na washambuliaji ambao wangeweza kushughulika na walinzi wa aina ya Nyosso, siku hizi hatuna washambuliaji wa hivyo, ndio maana nilimtaka Bocco awe mbabe kwa walinzi wa aina hii. Hata hivyo katika tukio la kumpiga mlinzi wa Mwadui, Revocatus Mgunga nadhani Bocco ameniangusha.
Amempiga wazi wazi mbele ya kamera huku kukiwa hakuna mpira. Nimesikia mahala kwamba Mgunga ndiye mchezaji aliyemuumiza Bocco katika msimu uliopita kiasi kilichopelekea Bocco kukaa nje kwa muda mrefu akiumiza majeraha.
Hii ina maana lilikuwa tukio la kisasi. Hata hivyo lilikuwa tukio la kisasi ambalo halikuwa na maana. Kitu cha msingi kwa Mgunga ni kwamba atacheza mechi inayofuata na Bocco atakuwa nje kwa kadi nyekundu na hapo hapo hakuweza kumsababishia Mgunga ambayo yangemuweka nje kwa muda mrefu.
Bocco anatakiwa kuwa mbabe wakati anawania mpira au akiwa na mpira. Hivi ndivyo washambuliaji wababe wa zamani waliweza kumudu walinzi watukutu wa aina ya Nyosso. Mchunga Bakari, Ildephonce Amlima, Said Mwamba Kizota, Zuberi Katwila na wengineo niliwahi kuwaona wakitembeza ubabe kwa namna hii.
Walinzi wengi walikuwa wanawakimbia washambuliaji wa namna hii, zamani kulikuwa na walinzi watukutu kuliko hawa akina Nyosso na bado walipata washambuliaji wakorofi zaidi. Na ndio maana nilimtaka Bocco aongeze ubabe zaidi katika aina yake ya mchezo kwa sababu ingeweza kumpa nafasi ya kufunga zaidi.
Wakati fulani akina Said Mwamba walikuwa wanapata nafasi nzuri za kufunga kwa sababu ya kuhofiwa wakati wa kuruka au kupambana kuwania mpira kwa namna nyingine yoyote. Hata hivyo ilikuwa nadra kwa akina Mwamba kutembeza ubabe wakati wakiwa hawana mpira.
Kwa alichofanya Bocco, kwanza kabisa kinampa mwamuzi kazi rahisi kama ambavyo mwamuzi alivyofanya. Akina Said walikuwa wanawapa waamuzi kazi ngumu ya kujua kama wamefanya matukio kwa kudhamiria au kwa bahati mbaya.
Lakini katika hali ya kawaida, kama Simba inaendeshwa kwa misingi ya soka la kisasa basi Bocco anastahili kukatwa mshahara bila ya kujali kwamba ni nahodha na ni mchezaji muhimu klabuni. Hapaswi kupokea mshahara wa Mwezi huu au anaweza kupewa nusu.
Katika hali nyingine Bocco anapaswa kujua kuwa mchezaji wa kulipwa hawezi kufanya vile, haijalishi kama Mgunga alimtembezea ubabe kwa kiasi gani lakini mwisho wa siku mchezaji wa kulipwa anapaswa kuwa mvumilivu na kupanga visasi vyake kwa akili.
Tunaishi katika dunia ambayo maisha ya ndani ya soka yametawaliwa na kamera za Televisheni kama ambavyo watu wa Azam walinasa tukio lile. Nje ya soka tunatawaliwa na dunia ya mitandao ya kijamii. Hata kama mwamuzi wa mechi asingeona bado kamera za Azam zingemuumbua Bocco. Hapa ndipo mwanasoka wa kulipwa anapotakiwa kuwa mjanja zaidi.
Bocco anapaswa kujichunga zaidi kwa tabia kama zile wakati huu akiwa anavaa jezi ya Simba. Unaweza kujikuta unaondoka katika njia zako za maisha kama unaziweka kichwani zaidi tabia za Simba na Yanga. Ni klabu ambazo zinadekezwa sana na mashabiki na viongozi wake kiasi kwamba unaweza kujikuta unafanya matukio mengi bila ya kushutumiwa na ukapotea njia.
Katika jezi ya Azam tukio kama lile linaweza kushutumiwa maradufu kuliko ukiwa Simba ambapo utapata watetezi wengi hadi Waandishi wa habari. Tabia hii imelemaza mastaa wetu wengi. Hata wachezaji wengi waliotamba katika klabu hizi baadae walikuja kuishi maisha mabovu kwa sababu ya kudekezwa kulikopitiliza na mashabiki wa timu hizi.
Wengine waligoma kwenda nje katika malisho mema pindi walipotakiwa kufanya hivyo kwa sababu ya kudekezwa kulikopitiliza. Bocco asijitie doa katika maisha yake ya sasa ya Simba kwa sababu pale Azam hatukuwahi kumuona akifanya alichofanya dhidi ya Mgunga. Wote tunafahamu kwamba Bocco ni mtu muungwana.