JAMVI LA KISPOTI : Natamani Aiyee awakatae kwanza vigogo

Thursday March 14 2019

 

By Khatimu Naheka

PALE juu kwenye msimamo wa wafungaji wa Ligi Kuu Bara kuna majina yalikuwa yamesimama kwa muda mrefu na kila mmoja aliamini kwenye ushindani wa kuwania kiatu cha dhahabu cha ufungaji bora ndio yatakayochuana.
Hata hivyo, kwa sasa mtu amekuja kwa kasi ya kufunga na anawakimbiza kweli wenye majina hayo.
Huyo si mwingine ni Salim Aiyee, kijana flani hivi msumbufu kwenye suala la kufunga anawatesa sana makipa. Wakati wote anawaza kufunga tu na ndicho anachokifanya kwenye klabu yake ya Mwadui ya pale Shinyanga.
Majina makubwa yanayokimbizwa na Ayee ni Meddie Kagere na Heritier Makambo ambao hadi sasa wana mabao 12 kila mmoja huku wakiachwa nyuma na Ayee anayeongoza akiwa na mabao 15.
Kinachovutia zaidi Aiyee ni mshambuliaji mzawa ambaye kasi yake imekuwa mwiba kwa wafungaji wenzake ambao wengi wanaomfuatia ni wageni kutoka mataifa ya nje.
Kwa muda sasa nafasi hiyo ya ufungaji bora imekuwa ikitua kwa wachezaji wa kigeni tangu afanye hivyo mshambuliaji wa sasa Simba John Bocco wakati huo akiwa Azam FC.
Kasi ya Aiyee sasa sitashangaa kama wale jamaa wanaojua kupiga hesabu za fedha kupitia sajili za wachezaji wakianza kumvisha jezi za Simba, Yanga na hata Azam katika hesabu za akili zao.
Soka letu mara nyingi limekuwa na mhemko mkubwa kwa tathimini ya kina kutopigwa katika kufanya usajili na hili ni kosa ambalo klabu kubwa zimekuwa zikipoteza fedha.
Huu ni msimu wa kwanza kwa Aiyee kufikia mafanikio hayo ya kufunga idadi ya mabao 15 mpaka sasa wakati ligi ikiwa inaencdelea.
Katika akili ya utulivu kuvutiwa na Aiyee hilo halipingiki klabu mbalimbali zinaweza kuanza kumfikiria.
Nionavyo bado Aiyee alipaswa kubakia katika klabu kama Mwadui kujijenga zaidi kuliko akichukuliwa kwa haraka na kupelekwa timu kubwa.
Kuna kina Aiyee wengi ambao walivuma kama huyu kisha waliponyakuliwa na vigogo wakapotea kwa haraka na kuinyima wachezaji bora nchi yetu.
Dua yangu ni kuomba Aiyee awakimbie zaidi kina Kagere na kupiga hata mabao 25 mpaka mwisho wa msimu kisha baada ya hapo abakie Mwadui kwa msimu ujao afanye kazi nyingine bora kama hiyo ya hata kufikisha mabao 24 kwa msimu unaofuata.
Akifanya hivyo ataonekana ni mshambulaiji ambaye amekomaa na kuthibitisha ubora wake hakubahatisha kile alichofanya katika msimu uliopita.
Angalia mtu kama Adam Salamba alivuma katika mechi chache tu akiwa na Stand United kisha Lipuli na kufunga mabao ambayo hayakuzidi hata tisa lakini haraka akanyakuliwa na kupelekwa timu kubwa kisha akapotea akitua Simba.
Sina maana kama Salamba alibahatisha lakini klabu aliyokwenda kwa ubora wake hawezi kupambana kwa kuwaweka nje watu kama Meddie Kagere, John Bocco au hata Emanuel Okwi.
Kumbe kama Salamba angesalia Lipuli angeweza kuonyesha kasi kubwa kwa klabu yake kumpa nafasi zaidi na kuzidi kuonyesha ubora wake na kukomaa zaidi katika kufumania nyavu.
Kosa kama hili pia linaweza kufanyika kwa Aiyee kama atatanguliza tamaa ya pesa kisha kutimkia timu kubwa ambazo zitamsajili kwa nia ya kukomoana na klabu zingine kisha juu yake wakaongezwa mastraika wakubwa ambao watammeza.
Wakati mwingine kinachowakwamisha ni presha kubwa zilizopo katika timu hizi mashabiki wao wanaamini anayesajiliwa katika timu yao ni mtu hatari na anapofuika na kukumbana na presha hiyo kupotea ni jambo la kawaida.
Natamani kuona Aiyee akibaki Mwadui kwanza chini ya Kocha Ally Bizimungu ambaye ana uzoefu mkubwa katika kutengeneza wachezaji bora kama alichofanya kule kwao Burundi ili mfungaji bora huyu awe n a tija kubwa kwa taifa huko baadaye.

Advertisement