Namuona Neymar katika jezi nyeupe Hispania

Saturday December 2 2017

 

Nitajie vitu ambavyo haviwezekani. Lionel Messi kucheza Real Madrid haiwezekani. Mario Balotelli kutuliza kichwa chake haiwezekani. Cristiano Ronaldo kwenda Barcelona, Haiwezekani. Waisrael na Wapalestina kupatana. Haiwezekani.

Kuna vitu vingi haviwezekani duniani. Lakini Neymar kwenda Real Madrid inawezekana sana. Tena sana. Nasikia chokochoko nyingi kutoka Santiago Bernabeu. Nauona moshi mwingi kutoka Santiago Bernabeu. Nahisi moto unaweza kuwepo.

Ukiunganisha nukta nyingi katika suala la Neymar kwenda Real Madrid basi unaweza kupata kitu kamili. kwa sasa inaonekana kama masikhara kwa sababu ndio kwanza Neymar ametua PSG kwa rekodi ya uhamisho wa dunia. Hata hivyo muda mchache ujao kuna kitu kinaweza kutokea.

Tofauti na Lionel Messi, Neymar hajawahi kuwa Mcatalunya. Neymar ni Mbrazil aliyetua uwanja wa Ndege wa Barcelona kusaini Barcelona akiwa na miaka 20 tu. Messi alitua uwanja wa Ndege wa Barcelona akiwa na miaka 13.

Kuanzia hapo balehe yake aliipata Barcelona, utu uzima wake ulimkuta Barcelona, watoto wake aliwapatia Barcelona. Messi ni kama Mcatalunya. Anapotembea katika viunga vya Barcelona, Messi ni kama Gerard Pique au Cesc Fabregas. Ni mtoto wa Catalunya mwenye damu ya Argentina.

Kwa Neymar sio hivyo. Ndio maana hakupata tabu kuihama Barcelona katika dirisha kubwa lililopita. Hakuona kama Barcelona ilikuwa ni damu nzito kwake. Amekaa pale Miaka minne tu. Messi amekaa Barcelona miaka 17.

Hii ni kama hadithi ya Luis Figo. Alikaa Barcelona kwa miaka mitano tu akitokea kwao Ureno. Damu haikuwa nzito sana na ndio maana ilipokuja ofa ya kwenda Madrid hakujiona kama mtoto wa Catalunya. Alijiona kama mkazi tu ambaye anaweza kuhama jiji. Catalunya haikuwa rohoni. Ndivyo ilivyo kwa Neymar.

Lakini pia sijawahi kumuamini baba yake Neymar. Neymar Snr ni mpiga dili mzuri. Huyu kuna siku nitamuelezea vizuri zaidi. Juzi nimesikia akisema hajaondoa uwezekano wa mwanae kucheza Real Madrid. Neymar Snr anajua anachokifanya.

Mawakala na Mameneja maarufu duniani siku zote kazi yao ni kuhakikisha wanasapoti uvumi. Wanajua uvumi ndio chanzo cha pesa zao. Amefanikiwa kutengeneza mafungu mawili makubwa ya pesa kupitia kwa kampuni yake ambayo inamsimamia mwanae Neymar.

Alipata pesa nyingi zilizoleta kesi wakati Neymar alipohama kutoka Santos kwenda Barcelona. Na majuzi amepata pesa nyingi wakati Neymar alipohama kutoka Barcelona kwenda PSG. Unadhani ataingiza kiasi gani akifanikisha uhamisho wa Neymar kutoka PSG kwenda Real Madrid?

Ndio maana kaacha milango wazi. Ana akili timamu huyu. Na ndio maana makocha maarufu wanachukia mawakala na Mameneja kwa sababu siku zote akili zao wamezielekeza mchezaji ahame ili wapate pesa. Mchezaji akitulia katika klabu moja hawapati pesa nyingi.

Lakini pia uhamisho wa Neymar kutoka PSG kwenda Madrid unawezekana kwa sababu ya ukweli kwamba kama Neymar akiichoka PSG atarudi wapi katika timu kubwa yenye hadhi kubwa kama ya Barcelona.

Kule Barcelona hawezi kurudi kwa sababu Neymar alijenga ukuta na kuchoma daraja la mahusiano dhidi ya mabosi wa Barcelona na mashabiki wake ambao walichoma jezi yake wakati anaondoka. Uhusiano wao umekufa. Na umekufa kirahisi kwa sababu ile ile niliyoisema awali. Neymar hajioni kama Mcatalunya na hata mashabiki hawamuoni kama mwenzao.

Wabrazil na Waargentina wana timu mbili kubwa Ulaya. Real Madrid na Barcelona. Zamani ilikuwa AC Milan au Inter. Neymar kwa sasa hawezi kwenda Inter wala AC Milan. Sio timu za hadhi yake. Imebakia timu gani hapo? Real Madrid. Timu za Waingereza hazipo kwa ajili ya Waamerika Kusini walio katika kiwango cha juu. Haishangazi kuona Ronaldinho, Rivaldo, Ronaldo na Kaka ambao ndani ya miaka 20 hii walichukua tuzo ya mwanasoka bora wa dunia lakini hakuna hata mmoja ambaye aliwahi kugusa Ligi Kuu ya England. simuoni Neymar akienda tofauti na hawa. Ataenda wapi? Real Madrid tu.

Kama Ligi Kuu ya Ufaransa ikimchosha akaiona nyepesi, kama maisha ya Paris yakimchoka, kama kila kitu kuhusu PSG kikimkinai kama ilivyoanza kutokea kwa sasa, Neymar atakwenda Real Madrid.