NJE YA BOKSI: Kazi ya refa kiapo ni muhimu

Tuesday November 14 2017Peter Kisaranga

Peter Kisaranga 

By Peter Kisiranga

MWAMUZI katika mchezo wowote ule huwa mtu wa kutumainiwa na kuaminiwa ili aweze kutenda haki na kutoa uamuzi usio na mizengwe.

Katika soka neno rasmi ambalo hutumiwa kwa mwamuzi wa katikati ya uwanja ni refa (referee). Refa katika ngazi za juu anatakiwa kuhitimu mafunzo na kupata leseni kutoka katika shirikisho la mpira wa miguu linalotambuliwa na Fifa au mchezo wowote.

Refa hukimbia kwa njia ya hanamu (diagonal) akitokea Kaskazini Magharibi na kurudi Kusini Mashariki mwa uwanja kadiri pambano linavyoendelea, huku washika vibendera (linesman) wakikimbia pande mbili za uwanja kuanzia kwenye kona mpaka katikati ya uwanja.

Kazi za washika vibendera huwa ni kumshauri tu refa inapotokea uvunjwaji wa sheria za mchezo, ila uamuzi wa mwisho hubaki kuwa ya refa mwenyewe.

Mastori ya leo yanaturudisha hadi mwaka 1987 katika michuano ya Littlewoods Cup, wakati Nottingham Forest na Brighton zilipokutana. Katika pambano hilo mshika kibendera Ray Pearce alikuwa ni kaka wa mchezaji wa England na nahodha wa Nottingham Forest, Stuart Perce.

Stuart Pearce alijulikana akicheza kama beki wa kushoto alicheza dakika zote 90 huku mshika kibendera akiwa ndugu yake. mchezo huo uliendeshwa kwa haki na matokeo ya suluhu ya 0-0 hayakuwa na malalamiko licha ya watu wengi kutofahamu kuwa wawili hao ni ndugu wa damu.

Huko Scotland, beki wa timu ya taifa, Brian Mclean ambaye pia ni mdogo wa refa anayetambulika na Fifa, Steve Mclean, wao pia wamewahi kukutana kazini kwenye mechi kadhaa.

Steve Mclean kama refa huwa haoni tabu kutoa kadi za njano ama nyekundu endapo mdogo wake Brian atakwenda kinyume na sheria za mchezo. Kwenye moja ya mahojiano yake, Steve Mclean alisema kwa mzaha “Kuna wakati namuonya kwamba nitampa kadi na kwamba nitakwenda kumsemea kwa mama kama atarudia tena kucheza rafu.” Maisha ya refa yanapaswa kuwa ya uadilifu na umakini. Wafuatiliaji wazuri wa mpira wa Ulaya wanaweza kuwa wanamjua refa maarufu huko Pierluigi Collina wa Italia, licha ya kuwa na utumishi uliotukuka katika kazi yake alilazimika kujiuzulu baada ya kuingia mkataba wa biashara na kampuni ya Opel iliyokuwa ikidhamini pia A.C Milan na hivyo kuepusha mgongano wa kimaslahi. Wakati mwingine tusiwalaumu sana waamuzi kwani wao ni binandamu.