NINAVYOJUA : Zahera anatimiza kazi nyingi za kocha wa soka

Muktasari:

  • Pia kama kawaida waandishi wa habari walitaka wasikie lolote kutoka kwa Jerry Muro ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Arumeru kuhusiana na yanayoendelea kwenye soka la nchi yetu.

Juzi Jumanne Arusha baada ya mchezo wa Ligi Kuu uliozikutanisha African Lyon dhidi ya Simba iliyoibuka na ushindi wa mabaoa 3-0 kulikuwa na matukio mengi sana achana na tukio la Haji Manara kumvarisha Jezi ya timu ya Simba, Jerry Muro ambaye bila shaka ni mpenzi na mwanachama wa klabu ya Yanga.

Pia kama kawaida waandishi wa habari walitaka wasikie lolote kutoka kwa Jerry Muro ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Arumeru kuhusiana na yanayoendelea kwenye soka la nchi yetu.

Muro aliongelea mambo mengi sana yaliyotokana na yeye kukubali kuvalishwa jezi, lakini akaenda mbali hadi kuiongelea timu ya Yanga, akawaongelea baadhi ya wachezaji nguli waliocheza kwa muda soka waliopo Yanga msimu huu akianza na Mrisho Ngassa kuwa sasa mpira mguuni hakuna kwa hiyo akatafute kazi ya kufanya.

Pia kwa Haruna Moshi vile vile, akaenda mbali zaidi na kumfananisha au kumuona Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera kuwa si Kocha hasa bali ni Mhamasishaji.

Inawezekana kwa mtazamo ikawa ni mtazamo wake na akawa sahihi kwa upande wake. Majibu anayopata kupitia mitandao ya kijamii mengi ya majibu hayo yameelekezwa kwake kwa jazba sana badala ya kumuelewesha kwa ufundi zaidi kuhusu kauli yake hiyo kuanzia kwa wachezaji hadi kwa kocha mwenyewe.

Kwanza Jerry aelewe uwepo wa wachezaji kama Ngassa na Haruna Moshi ndani ya klabu ya Yanga kwa sasa kumetokana na kundi lililopo pale la wachezaji wa Yanga kutofanya kazi zao ipasavyo, kuna kundi la wachezaji wengi waliokuwapo pale pamoja na ujana wao halikuwa likidhi mahitaji ya timu ya Yanga, Vijana wengi wapo pale kama wanavuta muda tu lakini hawana mchango wowote.

Hata hivyo kuingia kwao Yanga hakukuja kirahisi tu bali kulitokana na kazi nzuri walioionyesha huko walikokuwa Ndanda kwa Ngasa na African Lyon kwa Haruna Moshi.

Pamoja na umri wao huo ambao Jerry amewataka wakatafute kazi nyingine bado Kwa Ngasa imekuwa tofauti kwani hadi sasa ameshaifungia timu yake goli nne na kutoa usaidizi mara mbili wa kupatikana kwa mabao, Jerry anatakiwa aione tofauti hii na wachezaji vijana kama kina Matheo Anthony ,Juma Mahadhi, Saidi Makapu na wengineo ambao hawana hata baa moja hadi sasa, hata hivyo mahitaji ya kikosi cha sasa cha Yanga kilihitaji wachezaji wachache waliocheza huko nyuma kuja kumsaidia kocha katika kujenga saikolojia ya wachezaji wanaoishi kidogo kwa tabu ili waendane na mfumo wa sasa.

Huku kwa Kocha ndiko hasa bwana Muro amekosea na inawezekana ikawa si makosa yake sababu hajawahi kusoma kozi za Ualimu wa Mpira wa miguu na kujua majukumu ya kocha zaidi.

Muro ameshindwa kutofautisha kati ya Kocha Mhamasishaji na Kocha mfundishaji wa mpira wa miguu na Mwinyi Zahera akiwa mmoja wao, sasa ni vizuri tukatoa somo la kitabuni kuliko kukasirika na kumjibu kwa hasira hasa kama jinsi mashabiki wa Yanga wanavyomjibu huku wakiwa wamekasirika sababu kocha kipenzi chao ameguswa.

Muro anatakiwa kujua yafuatayo kwa Mwalimu wa mpira wa miguu kuwa ;

Kocha ni Kiongozi, kwa maana Kocha anaongoza kundi la watu fulani wachezaji zaidi ya 30 na benchi lake la ufundi hivyo anahitaji kujua nini anakifanya mbele ya kundi hilo ili liweze fika kule anakokutaka.

Pili ajue kuwa Kocha ni Mzazi; Kocha anaishi na kundi la wachezaji wanaoishi kama wanafunzi wanaoishi kama watoto wadogo hivyo ajipambanue kama mzazi ili mafunzo yake yaweze kupokelewa vizuri na kufanyiwa Kazi.

Tatu Kocha ni daktari, kocha mara nyingi huweza kujua magonjwa ya wachezaji hata yale ya ndani na kisha idara ya utibabu hufanya kazi yake, kocha ni lazima ajue kila ugonjwa wa mchezaji ili apange programu zake kulingana na idadi kamili ya wachezaji walio vizuri.

Nne Kocha ni mwana Saikolojia; ni lazima ajue kuweka sawa akili za vijana wake pale wanapokuwa na msongo wa mawazo mmoja mmoja au kwa timu nzima, ndio maana kwenye kozi za ualimu wa mpira wa miguu haya yote hufundishwa.

Tano Kocha ni Mhamasishaji; hakuna namna Kocha anaweza kukwepa hali hii, ni lazima kocha awe mbunifu kila mara kujua wapi wanapokwama na wanatoka je, lazima kocha acheze na akili ya wachezaji na hata wapenzi na mashabiki wa timu yake ili kujua ni aina gani ya motisha wachezaji wanatakiwa kupewa. Sababu nyingi ambazo kocha huwajibika kuzifanya hivyo basi kwa Jerry Muro hakuna kosa kumuona kocha kama Mhamasishaji.