NINAVYOJUA : Kakolanya akumbushwe kilichofanywa na Samatta

Muktasari:

  • Kakolanya ni moja kati ya watu waliochangia kuifanya Yanga kuwa hapa na hakuna anayeweza kusahau kazi aliyoifanya kwenye michezo dhidi ya Mtibwa, Stand United na Simba ambayo Yanga iliibuka na ushindi michezo miwili na suluhu mchezo mmoja dhidi ya Simba. Ni Beno ndiye aliyekuwa anaibuka shujaa kwenye michezo hiyo.

KWA muda mrefu kipa wa Yanga, ambaye kwa sasa amerudisha furaha ya mashabiki mahali pake, Beno Kakolanya, amekuwa akiisaidia timu yake kupata ushindi zinazoifanya kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara. Yanga inashika rekodi ya kutopoteza mchezo hata mmoja kwa sasa, lakini mambo yake hayajaa sawa.

Kakolanya ni moja kati ya watu waliochangia kuifanya Yanga kuwa hapa na hakuna anayeweza kusahau kazi aliyoifanya kwenye michezo dhidi ya Mtibwa, Stand United na Simba ambayo Yanga iliibuka na ushindi michezo miwili na suluhu mchezo mmoja dhidi ya Simba. Ni Beno ndiye aliyekuwa anaibuka shujaa kwenye michezo hiyo.

Lakini, kwa muda mrefu kipa huyo tegemezi amekuwa nje ya timu kwa mtazamo wa mgomo baridi ambao, anautimiza kwa kuwa ana madai mengi kuanzia pesa ya usajili, posho na mishahara isiyopungua miezi mitatu.

Beno ameamua kutumia njia hiyo ambayo bila shaka ni njia inayomsogeza karibu kabisa na ujenzi wa uhasama, si tu kutoka kwa wanachama, wapenzi na mashabiki wa Yanga bali unakwenda hadi kwa viongozi na baadhi ya wachezaji wa timu.

Kakolanya ni mfanyakazi ya mpira wa miguu na anastahili kulipwa kila kitu kwa ufupi hiyo ni haki yake.

Anafanya kazi mwisho wake anatakiwa kulipwa ili maisha yake yawe na furaha huku akiithamini kazi anayoifanya. Beno anayo familia inayomtegemea kwa kiasi kikubwa na soka ndio kazi yake.

Beno ana madai sahihi ambayo viongozi wa Yanga wanastahili kuyakabili na kumsaidia ili aweze kurudi kundini ingawa bado kuna ukakasi wa madai yake kutofanyiwa kazi na viongozi, huku akiamua kugoma wakati wenzake ambao, nao inasemekana wanayo madai yanayofanana na yake.

Ukakasi huu unakuja kutokana na kuwa hii si mara ya kwanza kwa Kakolanya kugoma akishinikiza kulipwa madai yake , njia hii amekuwa akiitumia kila anapotaka kulipwa ingawa wachezaji wengine hawafanyi hivi.

Kwa muda huu wote wa mgogoro wa Beno na uongozi kumekuwa na maneno mengi yanayosemwa kuwa nyuma ya hili.

Moja ni Beno kufikia hali hii ni uwepo wa meneja wake, ambaye ni mdau mkubwa wa Simba akiwa na nafasi kubwa ndani ya klabu hiyo, kwa mtazamo wa kawaida tu unaweza kusema huu ni mchanganyo wa kifikra ‘Conflict of interest’ kuwa hawezi kuona jema linafanywa na mteja wake hasa pale timu zao hizi mbili zinapokutana, ingawa kwenye hili Beno alishafanya kazi yake.

Kitu cha pili kinachotajwa kuzunguka kadhia hii ni kuwa Beno alikuwa anategemea kuondoka ndani ya Yanga na kujiunga na klabu nyingine zikitajwa Simba na Azam za hapa Tanzania. Hata hivyo, kadri siku zinavyokwenda mambo yanayosemwa yanaonekana kuyeyuka kirahisi na kumuacha Beno akiendelea kudai madai yake kwa utaratibu huo huo aliouzoea.

Nataka nimkumbushe Beno kuwa njia aliyopitia ishawahi kufanywa na Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samata ambaye alijiunga na Simba msimu wa 2010/2011 na baada ya kusaini kandarasi hiyo ambapo ndani ya mkataba aliahidiwa kupewa pesa na gari kitu ambacho hakikutimizwa. Simba walimpa pesa lakini hawakumpa gari kitu kilichomfanya Samata kugoma kujiunga na klabu hiyo akishinikiza kuwa alipewe gari kwanza, mgogoro huo ulichukua nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari na kuwafanya viongozi wa Simba kutokuwa na maelewano mazuri dhidi ya mchezaji huyo.

Samatta aliendelea kugoma akikaa nyumbani huku wenzake wakicheza haikuonekana suluhu yoyote zaidi ya wadau wakubwa wa soka kumwambia Samatta arudi kwenye timu akacheze.

Nakumbuka Kocha maarufu nchini, Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’ alimuandikia makala kali Samatta kupitia gazeti moja akimwambia: ‘Mbwana Samatta Rudi ukacheze Soka hapo Simba ni mahali pa kupita tu hayo magari utayakuta mengi sana baadaye, rudi kipaji chako ni kikubwa zaidi ya hiyo gari’.

Bila shaka alijiuliza sana baada ya kusoma makala hiyo, nasikia alimpigia simu, Kenny huku akilia, haikumchukua muda kwani ndani ya msimu huo huo Samata alikutana na zali kubwa hasa baada ya kufanya kazi ya ziada kwenye mchezo wao dhidi ya TP Mazembe ambayo ndio iliyomfanya hasa awe hapa alipo, sijui kama angeendelea kugoma kwa kukaa nje ya timu leo angekuwa wapi!