NINAVYOJUA : Chozi la Mwinyi Zahera ni kengele kwa waamuzi

Muktasari:

  • Katika hilo hakuna suluhisho zaidi ya kufukuzwa kwa kuvunjiwa mkataba na kulipwa stahiki zao.
  • Zipo sababu zinazosababisha timu kutofanya vizuri ambazo ni maandalizi mabaya, usajili usio sahihi na pamoja na ukata.

MAKOCHA ni wahanga wa matokeo mabaya yanazoziandama timu na kushindwa kufikia malengo.

Katika hilo hakuna suluhisho zaidi ya kufukuzwa kwa kuvunjiwa mkataba na kulipwa stahiki zao.

Zipo sababu zinazosababisha timu kutofanya vizuri ambazo ni maandalizi mabaya, usajili usio sahihi na pamoja na ukata.

Lakini matokeo mabaya pia yanaweza kusababishwa na waamuzi wanaobadili kazi nzuri ya kocha kwa ndani ya dakika 90 tu. Waamuzi wanaweza kuharibu kila kitu, mipango ya timu falsafa ya mwalimu na malengo ya timu kwa makusudi au kwa kutojua.

Hali hii imewafanya makocha kwa miaka mingi kuwa wahanga wa uchezeshaji mbaya wa waamuzi. Na zaidi wamekuwa wakiendelea kuwa wanyonge mbele ya waamuzi.

Waamuzi ndio wameshika makali ya kufanya lolote kama ni kumtoa kocha uwanjani na kuandika ripoti inayoweza kuwashawishi wasimamizi wa mpira kutoa mamuzi juu yake, kusimamishwa au kulipa faini. Mbaya zaidi kocha anakuwa ameshapoteza mchezo na zaidi anaweza kupoteza kazi yake.

Msimu huu tunaona kitu tofauti kuliko misimu iliyopita. Msimu umeghubikwa na hali ngumu ya uchumi. Timu nyingi haziwezi kujiendesha, nyingi zikishindwa kuwalipa mishahara wachezaji na hata kusafiri.

Hali hii kwa klabu zetu imesababisha hata waamuzi nao kuwa na hali mbaya. Kwa sababu ule ukarimu uliokuwa ukifanywa na klabu kwa waamuzi kila wanakokwenda haupo tena. Mfano waamuzi siku zote wamekuwa wakipokelewa na timu mwenyeji na kupewa chakula, malazi na mambo mengine.

Klabu zilifanya hivyo ili kuwapunguzia makali ya maisha na kuwafanya kuchezesha kwa upendeleo kwa mwenyeji. Ama timu zenye uwezo wa kifedha na ziliwatumia fedha hizo kuwaghiribu baadhi ya waamuzi waliokuwa wakizipendelea waziwazi hivyo kuifanya ligi kukosa ushindani.

Lakini sasa timu nyingi zinapitia kipindi kigumu na hazina muda wa kuwakirimu waamuzi tena ili watoe upendeleo kwao.

Sasa waamuzi wanachezesha kwa uwezo, ujuzi, ufundi na timu bora ndiyo inayoshinda. Hakuna ule usemi wa timu hii imenunua mechi sasa ni uwezo tu wa kushinda viwanjani.

Uchezashaji wa waamuzi ukiwa bora, bila shaka tutegemee wawakilishi bora kimataifa. Msimu huu unaweza kuturudisha nyuma hadi mwishoni mwa miaka ya 80 au 90 hadi mwanzoni mwa 2000 ambako wawakilishi wetu walifanya vizuri kimataifa.

Mwaka 1993, Simba ilifika fainali ya Kombe la Caf (sasa Kombe Shirikisho) huku Yanga ikichukua Ubingwa wa Afrika Mashariki na kati 1995, 1996. Simba nayo ilichukua ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1998.

Mwaka 2003 Simba ilitinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hii ilitokana na uchezeshaji uliokuwa bora miaka hiyo.

Hali hii inaweza kutokea msimu huu kwa waamuzi ambapo pengine kwa namna moja au nyingine walikuwa wakighiribiwa kwa pesa zilizowafanya wachezeshe vibaya. Msimu huu hawapati na wapo huru kutuletea timu bingwa ya nchi ambayo bila shaka itapatikana kihalali kabisa. Hata hivyo, wapo waamuzi wachache bado wana mawazo ya kuchezesha kwa mazoea. Wanaingia viwanjani kuweka mizania sawa pasipo na ulazima. Wanajua Azam na Yanga bado hazijapoteza michezo, hivyo baadhi wanataka nazo zipoteze kwa lazima.

Hili ndilo lililomtoa machozi Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera mara baada ya mchezo dhidi ya Tanzania Prisons. Ni wazi Kocha Zahera anajua ligi nzuri ni ile inayoifanya timu bora kuibuka na ushinda ndani ya dakika 90 au kushindwa kwa haki na si kwa kulazimisha.

Kocha huyu anajua hata kwao, timu zinapata ubingwa kwa haki hata kama ni kwa ucheshaji wa makosa lakini sio mengi. Ndio maana timu zao zinapopata uwakilishi wa nchi hufanya vizuri kwenye michuano mikubwa barani Afrika.

Zahera anasikitika kwa nini mwamuzi ashindwe kuwa mkweli na kuchezesha kwa minajiri asiyoijua. Anasikitika kuliona soka letu linaharibiwa na waamuzi kwa makusudi.

Kocha Zahera hajazoea hali hii ikikithiri ni lazima ashangae kwa hiki kinachotokea.

Chozi la Mwinyi Zahera halikuwa la furaha kama wengine wanavyofikiria ni chozi lenye uchungu likiwataka waamuzi wa Tanzania kubadilika. Si vizuri waamuzi wakawaingiza makocha hata hawa wa kigeni kwenye mawazo ya kuwa huwa wanazipendelea baadhi ya timu kwa makusudi.