NI wakati wa Simba kuijua katiba yao

Muktasari:

  • Kamati ya Uchaguzi ya Simba ambayo ipo chini ya Mwenyekiti Bonface Lyamwike ilitoa mwongozo wa jinsi uchaguzi huo utakavyokuwa ambao kikatiba ulipaswa ufanyike Julai mwezi ambao ulikuwa muda mwafaka wa kufikia kikomo kwa viongozi waliopo madarakani.

UCHAGUZI Mkuu wa klabu ya Simba unatarajiwa kufanyika Novemba 3 mwaka huu.

Tayari fomu za kugombea nafasi mbalimbali ikiwemo ya mwenyekiti na wajumbe zimeanza kutolewa klabuni pale Mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam.

Kamati ya Uchaguzi ya Simba ambayo ipo chini ya Mwenyekiti Bonface Lyamwike ilitoa mwongozo wa jinsi uchaguzi huo utakavyokuwa ambao kikatiba ulipaswa ufanyike Julai mwezi ambao ulikuwa muda mwafaka wa kufikia kikomo kwa viongozi waliopo madarakani.

Kwa kufuata Katiba ya Simba hivi sasa klabu hiyo inaongozwa na Kamati ya Muda kwani tayari Rais Evans Aveva na Makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’ pamoja na wajumbe wao, muda wao wa kuiongoza Simba ulikwisha ingawa viongozi hao wakubwa nafasi zao zilikuwa zinakaimiwa na Salim Abdallah ‘Try Again’ na Idd Kajuna.

Klabu ya Simba sasa inaendeshwa kwa mfumo wa kampunu baada ya mwekezaji Mfanyabishara maarufu nchini, Mohamed Dewji ‘Mo’ kupita kwenye mchakato huo kwa kuwekeza Sh 20 bilioni ingawa hajakabidhiwa rasmi klabu hiyo hadi leo hii.

Kwa mujibu wa Katiba ya Simba ambayo itatumika kwenye uchaguzi huu ni ile ya 2018, inapaswa wachaguliwe wajumbe sita ambao wataingia moja kwa moja kwenye Bodi ya Wakurugenzi ambao sasa watachaguliwa kwenye uchaguzi huo wa Novemba 3.

Wanachama wa Simba wanapaswa kuwa makini katika uchaguzi wao kwa kuchagua wajumbe ambao watawawakilisha vyema kwenye vikao vya maamuzi mbalimbali ya klabu yao ili kuepuka kujutia hapo baadaye kama hawatachagua wajumbe sahihi kwa masilahi yao na klabu.

Simba ni klabu kubwa, hivyo inapaswa kuendeshwa na watu makini wenye uelewa mpana wa kuchanganua mambo ya sasa na yajayo.

Hivyo uchaguzi huu ufanywe kwa busara ya hali ya juu na usiwe uchaguzi wa mihemko ama kushwawishiwa na wagombea pengine wenye fedha za kuwarubuni wanachama ambao hawana uelewa mkubwa na katiba yao.

Kuwa na kiongozi bora ndiyo mwanzo wa kupata mafanikio makubwa ndani ya klabu ama sehemu yoyote ile lakini kama wanachama watakosea na kupata bora viongozi, basi hilo litakuwa ndilo anguko la mafanikio wanayoyalilia.

Kwa muda mrefu Simba imekuwa kitaka kuingia katika anza la timu kubwa barani Afrika kama vile TP Mazembe, Etoile du Sahel, Al Ahly, Zamaleki na hata Enyimba kwa kuzitaja chache, huu sasa ndio mwelekeo sahihi kama wanachama wa klabu hiyo wataweza kutumia fursa ya kuwachagua viongozi wa wenye mwono wa mbali.

Tunatarajia, wanachama wanawajua wenzao wanaoweza kuwaongoza kwa ufasaha na kuachana na wababaishaji.

Muda bado upo wa kufanya maamuzi sahihi na siyo ya kukurupuka ndani ya uchaguzi wa Simba. Hata kama kuna wagombea watawashawishi wanachama kuwachagua, basi lazima mwanachama wajiulize huyo anayewashawishi ana uwezo gani wa kuleta maendeleo ndani ya Simba.

Wanachama wanapaswa kupitia katiba yao kwa umakini ili kujua nini wanakwenda kukifanya mbele yao.