Muda wa Yanga, Simba kuthibitisha ukongwe wao

Muktasari:

  • Mhariri anaeleza namna timu za Simba na Yanga zilivyokuwa kongwe na kupata mashabiki wengi Nchini na kuwataka kuonyesha ukongwe wao kwa kucheza soka safi na lenye viwango bora.
  • Mashabiki wa timu hizo wametakiwa kuachana na uhuni wanaoufanya kila wanapokutana ambao hauna maana yoyote katika soka la sasa.

MASHABIKI wa soka na Watanzania walio wengi kwa sasa wameweka kando mambo mengine, kutokana na kumezwa na pambano la watani wa jadi nchini.

Jumapili hii Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana tena katika pambano la Ligi Kuu Bara likiwa ni pambano la 101 tangu zianze kukutana katika ligi hiyo 1965.

Timu hizo ndizo zilizoshika itikadi na kuwagawa Watanzania katika makundi mawili tofauti ambayo huzishabikia timu hizo. Ipo dhana kwamba kama mtu sio shabiki wa Yanga basi lazima awe Simba na kinyume chake.

Tangu wiki hii ianze gumzo kubwa ni mchezo huo wa kwanza katika msimu huu wa 2018-2019.

Watu wa kada na rika mbalimbali wamekuwa wakijadiliana na kupigana vijembe na kutaniana mitaani kwa sababu ya pambano hilo la watani wa jadi.

Hii ni kuonyesha namna gani soka la Tanzania lilivyoshikiliwa na klabu hizo kongwe zilizoasisiwa katikati ya miaka ya 1930.

Ukubwa wa pambano la Simba na Yanga haliwachanganyi mashabiki na wanachama wao tu, bali hata makocha, viongozi na wachezaji presha yao huwa kubwa katika kuelekea mchezo huo na hupumua baada ya kumalizika kwa mchezo huo. Faraja huja pale timu mojawapio inapopata matokeo mazuri dhidi ya mpinzani wake, huku wale ambao hupata matokeo mabaya kuna wakati hupatwa na dhahama isiyotarajiwa.

Mechi ya Simba na Yanga ndio inayofukuzisha kazi makocha, kuwang’oa viongozi madarakani na hata kuwatia lawama wachezaji wa timu hizo pale mambo yanapoenda kombo. Sio mara moja au mbili, mambo hayo yamekuwa yakishuhudiwa ndani ya klabu hizo, baada ya timu moja kufanya vibaya mbele ya mpinzani wake.

Kwa uzito huo huo ambao mashabiki wa klabu hizo na watanzania kwa ujumla hubeba kuelekea kwenye mchezo huo, ndivyo ambavyo timu hizo zinapaswa kubeba na kuhakikisha unajitofautisha na mechi nyingine.

Mashabiki wataenda Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuliangalia pambano la kipekee, kubwa na lenye msisimko wa aina yake. Mchezo huo hauwezi kulingana na ule wa Simba dhidi Stand United ama Yanga dhidi ya Ruvu Shooting.

Hivyo wachezaji wanapaswa kuwaonyesha watazamaji watakaomiminika uwanjani hapo vitu vya tofauti, soka lenye ufundi na ustaarabu ili kuthibitisha ukubwa na upekee wa mchezo huo.

Japo mara kadhaa mipambano ya aina hii imekuwa ikitoa taswira tofauti na matarajio ya wengi kwa maana ya timu kucheza ovyo kutokana na kukamiana, japo Mwanaspoti linaamini mambo hayo Jumapili hii hayatakuwepo.

Vikosi vyote vinavyoundwa na nyota mbalimbali wa kitaifa na kimataifa vitashuka uwanjani kuonyesha ubora na thamani yao mbele ya mashabiki.

Mambo ya kihuni na upuuzi aslani hatutarajii yatokee, ili thamani ya viingilio vitakavyolipwa na watazamani watakaoenda uwanjani vilingane na burudani watakayooshewa bila kujali matokeo ya dakika 90.

Kubwa ambalo Mwanaspoti linasisitiza ni kwamba waamuzi waliopewa jukumu la kuchezesha pambano hilo walitendee haki na mwishowe watu watoke uwanjani wakiwa na nyuso za bashasha hata kama timu moja itapoteza mchezo.

Tunaamini waamuzi waliopewa kazi hiyo ni wenye weledi wanaozifahamu vema sheria za soka na kujua ukubwa wa pambano hilo, hivyo wafanye yaliyosahihi kwa mujibu wa sheria na kuepuka kuchezesha kwa shinikizo toka nje ya uwanja.

Muhimu zaidi kwa mashabiki wa klabu hizo na watu wengine watakaoenda uwanjani kushuhudia mchezo huo, ni lazima wawe wastaarabu na kuzishangilia timu zao kiungwana sambamba na kujiepusha na matendo yasiyokubalika.

Ule uhuni wa kutumia viti kama silaha za kupigana, vitendo vingine vinavyokera na kutokea mara kwa mara na kusababisha kuharibu sifa ya mchezo wa soka, lazima yaachwe majumbani na watu waende Taifa kucheki na kufurahia burudani.

Michezo ni furaha, soka ni burudani na Simba na Yanga ni timu kubwa na kongwe na wajibu wao kuthibitisha kuwa hata pambano lao kweli ni la kipekee.