JAMVI LA KISPOTI : Msolla anatakiwa kufahamu haya kwanza Yanga

Thursday May 9 2019

 

By Khatimu Naheka

HATIMAYE Yanga imefanikiwa kupata uongozi kamili wa klabu yao kupitia uchaguzi wao mkuu uliofanyika Jumapili Mei 5 mwaka huu.

Kupitia uchaguzi huo Yanga sasa itakuwa chini ya uongozi wa mwenyekiti Dk Mshindo Msolla atakayesaidiwa na makamu wake Fredrick Mwakalebela pamoja na wajumbe wao nane wa kamati ya utendaji.

Hii ina maana kwamba sasa akili ya wanachama na mashabiki wa timu itakuwa inawaangalia viongozi hao katika kuendana na sera sahihi walizokuwa wanazitoa majukwaani wakati wa kuomba ridhaa.

Hata hivyo, uongozi huo hautakuwa na tija yoyote endapo Msolla na viongozi wenzake hawatatulia na kuyafanyia kazi mambo kadhaa ndani ya klabu yao.

Uongozi wa Msolla unatakiwa kuanza kuunda upya sekretarieti ya klabu hiyo itakayoweza kuhimili majukumu ya taasisi hiyo.

Yanga imeyumba kwa miaka kadhaa katika mambo ya kiofisi ya utendaji wa kila siku.

Yanga haikuwa klabu ya kufikia hatua ya kuchelewa ndege kwa kushindwa kusoma vyema tiketi za ndege lakini kwa miaka ya karibuni limetokea.

Klabu hiyo imepigwa faini nyingi ambazo katika hizo zipo nyingi ambazo zimetokana na upungufu katika usimamizi kutoka kwa maofisa wa taasisi hiyo.

Kifupi Yanga imekuwa ikiishi kiujanjaujanja katika sekretarieti yao kutokana na waliokuwa wanaendesha mfumo wa huo kuwa na ubora mdogo.

Waliokuwa wakichagua watu husika katika eneo hilo hawakuwa na utulivu mkubwa na kuisababishia klabu kuyumba kwa kiasi kikubwa.

Kuna mambo ambayo yamekuwa yakitokea na wanachama na mashabiki kulalamika, lakini kiini chake ni kukosa usimamizi mzuri wa kutoka katika sekretarieti.

Msolla na wenzake wanatakiwa kutulia kwa kwanza kutafuta katibu mkuu ambaye atakuwa injini yao wakati huo ambao wao watakuwa wanatafuta maendeleo ya klabu yao nje ya nyumba.

Kutafuta mtu huyu hakutakiwi kufanyika kwa kigezo cha kushibana na mtu, urafiki au alinisaidia sehemu flani bali anatakiwa mtu mwenye ubora mkubwa na mwenye weledi.

Taasisi nyingi za soka zimetumba nchini kwa kushindwa kufanya maamuzi haya sahihi katika eneo hilo kwa kutangulia kuchagua marafiki na sio watendaji wanaotakiwa wenye weledi.

Wakimaliza kutafuta mtu huyo, kazi hiyo inatakiwa kuendelea katika maeneo mengine ambayo taasisi hiyo inatakiwa kuyajaza.

Uongozi wa Msolla umebeba dhamana kubwa pengine kuliko tawala zilizopita kulingana na nyakati tunazoishi.

Yanga kuweza kuingia katika mfumo mzuri wa mabadiliko, Msolla na wasaidizi wake wanatakiwa kuwa katika utulivu mkubwa katika kusimamia mchakato husika ufanikiwe kuondoa changamoto zote.

Kama Yanga itakuwa inayumba katika utendaji wa kila siku, hakutakuwa na wepesi katika kuanzisha mfumo mpya wa uendeshaji wa klabu hiyo.

Bahati kubwa ambayo Msolla anaweza kuitumia ni uwepo wa Mwakalebela katika utawala wake ambaye kama akili yake naye itakuwa katika afya kubwa inaweza kuisaidia klabu hiyo kuwa na watu muafaka katika ofisi zao.

Kama uongozi wa Msolla utayumba kuanzia katika sekretarieti hili litazalisha mambo mengi ya hovyo katika utawala wake.

Advertisement