NINAVYOJUA : Mapro Simba watabadili mawazo ya Mo Dewji

Thursday February 14 2019

 

By Joseph Kanakamfumu

Juzi ya Jumanne tarehe 12, Simba iliutumia vizuri sana Uwanja wa Taifa kujiongezea pointi kwenye akiba yake na kufikia pointi sita, baada ya kuifunga timu ngumu ya Al Ahly kwenye mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba ilipata ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na nyota wa timu hiyo Meddie Kagere na kuipeleka hadi nafasi ya pili ikiwaacha AS Vita na JS Saoura lkwenye nafasi ya tatu na nne kwenye kundi D.

Licha ya kupoteza michezo miwili mfululizo dhidi ya AS Vita na Al Ahly kwa kufungwa mabao matano kila mchezo, bado haijaifanya Simba kuteteleka katika kuwania nafasi ya juu ndani ya kundi hilo.

Achana na ushindi walioupata, kiwango bora walichoonyesha Simba siku hiyo, kiliwafanya Al Ahly washindwe kabisa kutengeneza mipango yao kutoka nyuma na kuwafanya wachezaji wa Al Ahly wabadili mbinu kabisa.

Al Ahly badala ya kucheza kwa pasi nyingi fupi fupi na mipango mingi iliwabidi kuanza kutumia pasi ndefu za juu kitu ambacho siyo kawaida kwao.

Simba walijituma sana na kuwabana wachezaji wa Al Ahly wasiweze kusogea kwenye eneo lao kwa kuziba nafasi zilizokuwa zikitengenezwa huku washambuliaji wao watatu Kagere, John Boko na Emanuel Okwi.

Okwi alifanya kazi ya ziada ya kurudi nyuma kuchukua mipira na kuwaacha washambuliaji wawili juu waliosaidia kuwazuia walinzi wa Al Ahly wasipande mbele kirahisi.

Kushuka kwa Okwi kuchukua mipira kulisaidia sana kuongeza idadi ya viungo waliokuwa watatu na kulifanya eneo hilo kuwa na wanne pamoja na Jonas Mkude, James Kotei na Clotous Chama, hivyo kutengeneza muunganiko mzuri sana katikati.

Hali hii iliwapa nafasi ya kupumua walinzi wa Simba ambao hawakuwa na kazi kubwa ya kumkaba Junior Ajeyi aliyeachwa peke yake mbele na kwa matumizi ya mipira mirefu ya juu iliyokuwa ikichukuliwa kirahisi na kina Pascal Wawa na Juurko Murshid kulimfanya Aishi Manula asiwe na wasiwasi golini.

Al Ahly walishindwa kabisa kuonyesha kile walichokifanya Misri ambacho wengi walikitarajia na kuonyesha ni klabu kubwa yenye mingi ndani ya uwanja.

Juzi Simba walikuwa bora sana na usingeweza kuona makosa ya mchezaji mmoja mmoja kuanzia beki, viungo, hadi washambuliaji kwani walicheza pamoja ‘Team Work’ ya hali ya juu na kujitolea kwa hali ya juu na hamasa ilionekana.

Ni kutokana na kiwango hiki bora walichokionyesha Simba ndicho kinachoweza kuibadili kauli ya muwekezaji mkuu wa timu hiyo, Mohamed Dewji ambayo aliisema siku chache kabla ya mchezo huo wa juzi kuna uwezekano mkubwa kikosi hiki kubadilishwa na kubakizwa wachezaji wachache wanaonekana kujituma uwanjani na wanaonekana kucheza kwa nidhamu kubwa.

Alisema hao ni wale wenye uwezo mkubwa wa kucheza michuano hii mikubwa barani Afrika, hii ilitoa onyo kuwa wachezaji wengi watakaokumbwa na kadhia hii ni wale wanaotoka nje ya nchi. Ukiwaangalia wachezaji kumi wa kigeni wa Simba wapo wengi wanaonekana kuelea tu ndani ya kikosi hicho, ndio maana MO Dewji alisema angalau anaona wachezaji wa kigeni wasiozidi watano ndio wanaoweza kubaki Simba.

Bila shaka hili la matokeo mabaya mfululizo lilimfanya tajiri huyu kujiuliza sana umuhimu wa kuwa na wachezaji 10 wa kigeni wanaonekana kutokuwa na kazi na zaidi kuongeza gharama isiyo na sababu.

Matokeo mabaya ndiyo yalisababisha tajiri huyo kuongea hayo, ingawa hili kwangu naweza kusema linasaidiwa sana na mipango ya kocha mkuu ambaye anaweza kuwafanya wachezaji wa kawaida kuonekana bora.

Hata hivyo, kwa kiwango cha juzi walichokionyesha Simba bila shaka Mo itabidi abadili mawazo na kufikiria upya juu ya kauli yake ya kuwafyekelea mbali wachezaji wengi wa kigeni.

Ukiangalia ndani ya kikosi cha Simba kilichoanza unawaona wachezaji saba au wanane wakiwa ndio nguzo kubwa ya timu ukiwaacha Haruna Niyonzima, Nicolas Gyan na Asante Kwasi aliyetoka baada ya kuumia waliobaki wote walianza na kuifanya Simba kwa asilimia kubwa kubebwa na wachezaji wa kigeni.

Advertisement