TASWIRA YA MLANGABOY : Mapato ya mlangoni yamewadumaza viongozi wa klabu

Friday November 15 2019

By Andrew Kingamkono

TIMU ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ leo Ijumaa Novemba 15, 2019 itarusha karata yake ya kwanza dhidi ya Equatorial Guinea katika kusaka tiketi ya kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika Afcon 2021 Cameroon.

Katika mashindano hayo Tanzania ipo kundi J moja na Equatorial Guinea, Libya na Tunisia. Baada ya mechi ya leo Taifa Stars itasafiri hadi Tunisia kucheza dhidi ya Libya. Libya imechagua Tunisia kuwa ndiyo nyumbani kwake kutokana na machafuko yanayoendelea katika nchi yao kwa sasa.

Hakuna ubishi kila Mtanzania ndoto yake ni kuona Taifa Stars inaanza vizuri mashindano hayo na kujihakikishia nafasi ya kufuzu kwa fainali hizo za Cameroon 2021.

Kubwa kwangu ni kuwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi Ijumaa kuanzia saa 9 Alasiri ili inapofika saa 1:00 usiku Uwanja wa Taifa uwe umejaa kila kona.

Ni matazamio ya mashabiki na wapenzi wa soka katika Tanzania Stars itaingia uwanjani kwa nia ya kusaka ushindi mnono wa mechi ya nyumbani ili kujiweka vizuri.

Mashabiki na wapenzi wa soka wajitokeza kwa wingi na kuipa hamasa Stars, na kuonyesha uzalendo wa kushangilia mwanzo mwisho kama ilivyokuwa katika mchezo dhidi ya Uganda pale timu ilipofuzu kwa Afcon 2019.

Advertisement

Pamoja na kuwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi, pia namuomba IGP, Simon Sirro pamoja na Kamanda Lazaro Mambosasa kuwapanga vijana wao vizuri nje ya uwanja kulinda usalama wa mali za watu, kwani kumekuwa na matukio uporaji vitu hasa wanapotoka katika michezo hii ya usiku.

Tukiyacha hayo ya Taifa Stars, wiki hii Taswira inataka kuzungumzia suala la maendeleo ya klabu zetu nyingi za Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa katika hali mbaya ya kifedha.

Maisha ya wachezaji wetu na suala la mishahara yao katika klabu nyingi bado ipo chini jambo ambalo kwa sehemu moja linapoteza utamu wa ligi yetu.

Hakuna ubishi maendeleo ya klabu yoyote ya soka popote duniani yanategemeana na jinsi inavyojiendesha kisasa pamoja na utaratibu waliojiwekea miongoni mwao na kujitangaza zaidi.

Soka ni mchezo unaohitaji uwekezaji mkubwa wa fedha na kuwa na viongozi thabiti ili klabu iweze kuendesha kutokana na vyanzo mbalimbali ndani na nje ya klabu husika pamoja na biashara ambazo zinatokana na kazi zake ukilinganisha na ukubwa wa timu yenyewe.

Uuzaji kama wa skafu, jezi, kofia, raba na vitu vingine vyenye nembo ya timu hizo ni sehemu kubwa ya kujipatia mapato kutokana na kuwepo mashabiki wanaopenda timu hiyo.

Katika dunia ya sasa klabu zimekuwa zikipata fedha kupitia haki za matangazo ya televisheni kwa kuuza vipindi vyao.

Ni jambo zuri kuona kampuni kubwa pamoja na watu binafsi wakijitokeza kwa nia ya kuzisaidia klabu hizi lakini kwa upande mwingine misaada hii haijitoshelezi hata kidogo kutokana na ukubwa wa timu zenyewe.

Klabu zetu hazipaswi kutegemea misaada inayotoka kwa wadhamini pekee pamoja na mapato ya milangoni kama wenyewe walivyojizoesha, bali ni wakati wa timu hizi kujiendesha zenyewe.

Uwezo wa timu kujiendesha zenyewe ni mkubwa endapo viongozi watakuja na mipango thabiti iliyokuwa bora na ushawishi wa wadhamini kuwekeza fedha zao na kuona jinsi zitakavyotumika na kuleta tija kwa pande zote mbili. Naamini klabu hizi kwa kushirikiana Bodi ya Ligi zina uwezo wa kukaa na kutafuta ni jinsi gani wanaweza kujiendesha bila kutegemea mapato ya milangoni kama ambavyo zinavyofanya sasa.

Kampuni zina uwezo mkubwa wa kuziendesha klabu hizi zaidi ya hapo zilipo na kutokana na timu hizi kuvaa jezi zenye nembo ya kampuni hizi ni dhahiri bado uwezekano wa kuzilipa zaidi ya hapo inawezekana. Tatizo kubwa ambalo nimeliona katika udhamini wa klabu nyingi kumekuwa na janjajanja nyingi sana ndiyo maana unaweza kuona timu ina wadhamini lukuki lakini hali yao hailingani na uwekezaji.

Kuna ripoti ya uchunguzi iliyofanywa barani Afrika na kuonyesha fedha nyingi za udhamini zinazoingiza katika klabu za soka haziwafikii walengwa ndio moja ya sababu ya mpira wa barani humu kukwama.

Viongozi wenye dhamana ya kusimamia klabu wanapiga dili chafu na wadhamini fedha zinazotangazwa siyo zinazoenda kuingia katika maendeleo ya timu na mchezo wenyewe.

Ndiyo maana leo utaona timu kama Yanga, Singida United na nyingine za Ligi Kuu pamoja na kuwa na wadhamini wengi bado zinashindwa kugharamia uendeshaji jambo linazozifanya zimekuwa ombaomba. Wakati umefika kwa klabu kuacha kutegemea mapato ya milangoni kujiendesha ni lazima kuwe na mipango bora na uwazi ya matumizi ya fedha za udhamini ili kupata tija kwa mchezo wenyewe.

Advertisement