MTU WA PWANI : Stars inahitaji zaidi akili ya Ndayiragije CHAN

Friday February 21 2020

Stars inahitaji zaidi akili ya Ndayiragije CHAN,CHAN 2020,Mbwana Samatta,Aston Villa ,Ligi Kuu England ,Ligi Kuu,

 

By Charles Abel

RAFIKI yangu Etienne Ndayiragije sidhani kama analala usingizi kwa raha ndani ya kipindi hiki cha kuanzia mwezi huu hadi mwezi wa nne.

Mbele yake ana vibarua viwili vigumu ambavyo atakabiliana navyo akiwa anakiongoza kikosi cha Taifa Stars ambacho yeye ni kocha mkuu. Kibarua cha kwanza ni mechi mbili za kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2021 dhidi ya Tunisia ambazo zitachezwa kati ya Machi 23 hadi Machi 31.

Mchezo wa kwanza utachezwa huko Tunisia na ndani ya muda wa wiki moja tu timu hizo zitarudiana jijini Dar es Salaam ikiwa ni michezo ya Kundi J ambalo linashirikisha pia timu za Libya na Guinea ya Ikweta.

Simuonei huruma sana Ndayiragije kwa mtihani huu wa kwanza kwa Stars wa kuwania kufuzu Afcon kwa sababu atacheza na Tunisia huku akiwa na kikosi kilichosheheni nyota wanaocheza soka la kulipwa ndani na nje ya nchi.

Uwepo wa nahodha, Mbwana Samatta anayechezea Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu England na pacha wake Saimon Msuva anayetamba kule Morocco katika Klabu ya Difaa El Jadida inayoshiriki Ligi Kuu.

Kwa bahati nzuri, Thomas Ulimwengu ameanza kufumania nyavu muda mfupi tu baada ya kujiunga na TP Mazembe lakini pia Ndayiragije anayo machaguo mengine kwa wachezaji wanaocheza nje ya nchi kama vile Farid Musa, Maka Edward, Yahya Zayd, Abdi Banda, Salum Chuku na David Kissu ‘Mapigano’.

Advertisement

Na kikosi hiki tayari kina muunganiko unaoeleweka hivyo hapana shaka hakitampa wakati mgumu Etienne kukiandaa kwa ajili ya mechi hizo na huenda kikaishangaza Tunisia kwa kuvuna ushindi ama pointi muhimu katika pindi kitakapokuwa ugenini na kwenye mchezo wa nyumbani.

Wasiwasi na shaka zaidi juu ya Stars upo pale kitakapokabiliwa na jukumu la kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (Chan) ambazo zitafanyika Cameroon kuanzia Aprili 4 hadi 25 zikishirikisha jumla ya timu za taifa 16. Katika mashindano hayo, Taifa Stars imepangwa Kundi D pamoja na timu za Zambia, Guinea na Namibia.

Hapa ni mahali ambapo Ndayiragije anapaswa kutuliza zaidi akili na kichwa chake ili Stars iweze kufanya vizuri vinginevyo tunaweza kujikuta tukiishia hatua ya makundi katika fainali hizo.

Kwanza ni kwa sababu hatakuwa na muda wa kutosha wa kuiandaa Stars kwa ajili ya mashindano hayo na kuna ulazima kwake kutumia maandalizi ya mchezo dhidi ya Tunisia wa kuwania kufuzu Afcon, kuiandaa timu kwa ajili ya mashindano ya Chan.

Hii ni kwa sababu, mara tu baada ya mchezo wa marudiano dhidi ya Tunisia, Stars italazimika kupanda ndege kuelekea Cameroon kwani mashindano ya Chan yatakuwa yamebakiza siku tatu tu kabla ya kuanza kwake.

Lakini changamoto nyingine inayomkabili Etienne Ndayiragije ni kukosa mwendelezo wa ubora kwa baadhi ya wachezaji ambao walitegemewa kuibeba Stars katika mashindano hayo, kutokuwa na uzoefu wa kutosha kwa nyota wengi wanaotamba katika ligi kwa sasa na pia hata majeraha kwa wachezaji kadhaa muhimu.

Mshambuliaji tegemeo wa Stars katika wale wanaocheza ligi ya nyumbani, Ditram Nchimbi sasa anachezeshwa nafasi ya pembeni katika kikosi cha Yanga jambo ambalo limepunguza makali yake ya kufumania nyavu, John Bocco anahaha kurudisha makali yake ya kufunga baada ya kutoka katika majeruhi lakini pia Kelvin Yondani naye amepungua ubora wake ule uliozoeleka.

Ni kama ilivyo kwa Erasto Nyoni ambaye bado hajarudi katika fomu yake iliyozoeleka wakati huo kina Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Abdulaziz Makame wakipoteza nafasi katika kikosi cha kwanza cha Yanga.

Nahodha msaidizi Juma Kaseja bado hajawa fiti baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti lake huku Miraji Athuman, Mzamiru Yassin na Salum Kimenya nao wakiwa ni majeruhi jambo linalomlazimu awatazame wachezaji wengine ambao wengi hawajawahi kupata fursa ya kuchezea Stars. Kina Lucas Kikoti, Reliants Lusajo, Paul Nonga, Daruwesh Saliboko, Kelvin Sabato, Yusuf Mhilu, Zawadi Mauya, Sadallah Lipangile, Sixtus Sabilo, Pato Ngonyani, Abdallah Ame, Baraka Majogoro na Mateo Antony wamekuwa moto wa kuotea mbali katika ligi ingawa hawana uzoefu wa kucheza mechi za kiushindani wakiwa na jezi ya Stars. Hapa Ndayiragije ana kibarua kingine kigumu cha kuwajenga kisaikolojia nyota hao ili hata akienda nao, wasiwe katika presha kubwa na waifanye vyema kazi kama alivyofanikiwa kwa beki Bakari Mwamnyeto.

Nina imani Stars chini ya Ndayiragije haitaenda kuwa mshiriki tu katika fainali za Chan ingawa nitakuwa tayari kupokea matokeo yoyote ambayo itapata.

Advertisement