MTAA WA KATI : Sarri ni maombi tu kukwepa rungu la Abramovich

Muktasari:

  • Kama sio sasa, basi baadaye, Maurizio Sarri atapokea tu meseji kwenye simu yake kutoka kwa Abramovich. Sarri mwenyewe ameshaanza kuishi kwa wasiwasi.

BILA shaka Roman Abramovich atakua anaangalia salio kwenye simu yake kama linatosha kutuma meseji. Bila shaka hilo atalifanya siku za hivi karibuni.

Kama sio sasa, basi baadaye, Maurizio Sarri atapokea tu meseji kwenye simu yake kutoka kwa Abramovich. Sarri mwenyewe ameshaanza kuishi kwa wasiwasi.

Hilo ni kawaida, hasa ukifanya kazi na Abramovich, ambaye suala la kukuondoka kocha na kuleta mwingine halijawahi kuwa gumu kwake.

Ninachokiona, Sarri anaelekea kwenye mlango uliandikwa ‘exit’ huko Stamford Bridge. Unakumbuka, wakati anafungwa na Arsenal, Sarri alidai anadhani wachezaji wake ni ngumu kuhamasika.

Kwa maana hana kitu cha kuwafanya wakapata hamasa na kushinda mechi. Tangu wakati huo, Chelsea kupata ushindi kimekuwa kitu nadra kuliko kupoteza. Mechi tatu za karibuni walizocheza ugenini, zote wamepoteza.

Mbaya zaidi wameshindwa kupata bao hata moja, huku wao wakiruhusu wavu wao kuguswa mara 12. Juzi Jumapili Chelsea imekwenda kucheza na Man City na kilichowakuta huko ni aibu.

Wamepigwa Sita Bila. Ndani ya uwanja, Chelsea ilionekana kuwa timu mbovu kuliko yoyote ile iliyowahi kutokea. Mabeki wa Chelsea walivyokuwa wakipitisha mipira ilikuwa kazi nyepesi kuliko hata chujio kupitisha maji.

Sergio Aguero hakuwa na kazi ngumu kufunga mara tatu. Alifanya hivyo huku akitasamu. Hakupata purukushani. Achana na hilo, cheki namna walivyofungwa bao la pili, ni kama vile Sarri aliwaokota tu wachezaji na kuwapeleka uwanjani.

Hawakuwa kabisa mchezoni. Hayo ni matokeo ya kufikirisha. Sekunde chache tu, kila kitu kimebadilika.

Sarri anahitaji kuvuta sigara zake vizuri. Kama kuna inayomlevya, basi aachane nayo mapema. Abramovich hajawahi kupata shida kufukuza mtu kazi, yeye huwa hataki kuteseka.

Chelsea mechi zake tano zijazo ni mtihani mzito kwa Sarri. Kama atavuka hapo salama, basi Abramovich bila shaka atafuta ile meseji yake iliyopo kwenye drafti, ‘you’re fired’. Hapo maisha yatakuwa salama kwa Sarri na atamaliza msimu akiwa bado Stamford Bridge.

Mechi hizo, kwanza, Chelsea itacheza ugenini kwa Malmo kwenye Europa League. Baada ya hapo itacheza na Manchester United kwenye Kombe la FA, kisha Malmo tena, halafu Manchester City kwenye fainali ya Kombe la Ligi na baada ya hapo watakuja kucheza na Tottenham.

Ratiba ngumu kabisa kwa Sarri. Kwasababu ndani yake kuna mashindano manne tofauti. Kwenye Ligi Kuu England, timu ipo nafasi ya sita, hivyo piga ua lazima wapambane wasipoteze mechi yao na Spurs ili wasijiweke mbali zaidi na Top Four.

Lakini, kuna Europa League pia, watahitaji kuwaondoa Malmo, wakishindwa, basi Sarri hawezi kupona. Kwa sababu kama hakuna nafasi kwenye ligi, njia pekee ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao ni kubeba Europa League.

Kutakuwa na mechi nyingine ya Kombe la FA dhidi ya Man United na fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Man City.

Akipoteza mechi hizo zote ina maana hakutakuwa na taji lolote Stamford Bridge msimu huu. Hapo itakuwa imethibitika rasmi kwamba Sarri ni chaguo baya zaidi kuwahi kutokea Chelsea.

Antonio Conte aliondoka Chelsea akiwaachia taji la Kombe la FA. Msimu wake wa kwanza aliwapa ubingwa wa Ligi Kuu England. Sarri staili yake ya soka analotaka kucheza haifanyi kazi kwenye Ligi Kuu England. Kung’ang’ania anachoking’ang’ania na ugumu wake wa kubadilika, umemfanya amfanye N’Golo Kante kuwa mchezaji wa kawaida sana.

Amefanya Chelsea kuwa na beki nyepesi kwa sababu hakuna beki wa kuilinda beki hiyo. Kung’ang’ania kutumia Jorginho mbele ya mabeki wa kati ni kujitengenezea bomu la makusudi.

Jorginho hakabi. Jorginho ni mzuri timu inapokuwa na umiliki wa mpira. Inapocheza dhidi ya timu inayoficha mpira kama Man City, inakuwa mtihani.

Lakini, ukirudi nyuma katika yale maneno yake kwamba wachezaji wa Chelsea hawahamasiki tena, hiyo ina maana Sarri ameshajiandaa kufeli. Ameshakubali yaishe.

Sasa ni wakali wa kina Eden Hazard tu kumbeba. Kinyume cha hilo, basi Abramovich atafanya kile ambacho ni kawaida yake kufanya kwa makocha waliopata nafasi ya kuinoa timu hiyo yenye maskani yake Stamford Bridge. Lakini, huu ni mwanzo tu, msimu ujao huenda ukawa mgumu zaidi kwa Chelsea kwa sababu Eden Hazard haonekani kama ataendelea kubaki baada ya magumu haya ya msimu huu kupita.

Ndoto zake kwenda kuichezea Real Madrid na hilo linakwenda kutokea mwisho wa msimu.