MTAA WA KATI : Ozil ni ferrari, lakini Emery anamfanya kama lori

Tuesday February 5 2019

 

By Said Pendeza

AKUFUKUZAE hakwambii toka. Hiki ndicho kitu unachoweza kusema kuhusu maisha ya Mesut Ozil na kocha wake Unai Emery.

Kitu ambacho Unai Emery amebakiza kwa Ozil ni kumwambia tu, ondoka kwenye timu yangu. Asikwambie mtu, hakuna mtu mwenye wakati mgumu kwa sasa kama Mjerumani huyo.

Unadhani ni wakati gani Ozil ataweza kumwonyesha kocha wake anastahili kupata nafasi?

Huko nyuma, stori za Emery zilikuwa Ozil ni mgonjwa. Kisha kikafika kipindi cha kuweka wazi Ozil hawezi kucheza mechi zenye upinzani mkali. Lakini, kwa sasa Mjerumani huyo anaishia kukaa kwenye benchi tu kwenye mechi ngumu za kuwakabili vigogo wa Top Six.

Maisha chini ya Arsene Wenger, Arsenal isingecheza mechi kubwa bila ya huduma ya Ozil, alikosa pale tu alipokuwa mgonjwa kweli.

Si kwa ugonjwa wa uongo kama anavyofanya Emery kwa sasa kuwatuliza mashabiki. Kitu kingine kibaya mashabiki wa Arsenal bado wanaamini katika uamuzi wa Emery, licha ya kwenye mechi kadhaa ambazo alimnyima nafasi staa huyo, Arsenal imeshindwa kupata matokeo.

Kuna msemo unaosema, Tembo hata akonde vipi, hawezi kuwa kama paka. Sawa, pengine Ozil ameshuka kiwango chake kwa sasa, lakini si kwa kiwango ambacho mipira yake itashindwa kuleta madhara kwenye mechi.

Kabla ya kuwakabili Arsenal, kiungo wa Man City, Ilkay Gundogan aliwaambia wenzake kamwe wasimdharau Ozil, atawafanya vibaya.

Lakini, hilo likiwa kwenye akili ya Gundogan kuwataka wenzake wawe fiti ndani ya uwanja kumkabili Ozil, Kocha Emery wala hakumwona kama mchezaji huyo anastahili kupata nafasi kwenye kikosi chake. Aliishia tu kwenye benchi huko Etihad na Arsenal imechapwa Bao Tatu. Ozil amekuwa si mtu wa mechi kubwa tena. Utashangaa kwa jeuri ya Emery.

Kwenye kikosi chake hakuna mchezaji anayeweza kuibadili nusu nafasi kuwa nafasi kamili kama awezavyo Ozil, lakini bado hataki kumpa nafasi.

Sijui, lakini pengine huo ni uamuzi ambao kama Wenger angekuwa na uwezo wa kupaza sauti, basi angesema kitu. Wenger anafahamu vyema uwezo wa ubongo wa Ozil kile unachoweza kufanya kwenye mpira. Ndio maana kwenye dirisha la Januari mwaka jana, alikubali kwa haraka sana kumwaachia Alexis Sanchez aondoke, lakini akambakiza Ozil na kumpa mshahara mkubwa. Aliamini katika huduma ya mchezaji huyo. Sijui Emery anatumia akili ya aina gani, ila naamini atakuwa anatumia ile akili aliyokuwa akiitumia Jose Mourinho kwa Paul Pogba.

Mourinho alimtaka Pogba akabe. Huo sio utamaduni wake na ukimtaka acheze hivyo, utashangaa kwanini Man United walilipa pesa nyingi kunasa saini yake.

Lakini, ukimtaka Ozil pia akabe, apigane vikumbo uwanjani, utashangaa kwanini Wenger aliamua kumlipa Pauni 350,000 kwa wiki. Ozil anahitaji uhuru ndani ya uwanja kama anavyotaka Pogba. Tazama kwa sasa Pogba kile anachofanya huko Old Trafford baada ya kuja Ole Gunnar Solskjaer.

Ameachwa huru, hatakiwi kukaba na kazi hiyo wameachiwa wenye uwezo nayo, Ander Herrera na Nemanja Matic. Emery angempa Ozil uhuru wake. Lakini, Emery anashindwa kuelewa kwamba Ozil ni ferrari, hupaswi kuendeesha kama lori. Bado naamini katika uwezo wa Ozil hata kama Emery atapingana na hilo.

Sijui ila sidhani kama Alex Iwobi ubongo wake unafanya kazi kama Ozil. Hilo halina kificho. Unamhitaji Iwobi mara 10 kwenye boksi akafanya jambo matata moja, lakini utamhitaji Ozil kwenye boksi mara mbili tu, anakufanyia kitu kizuri. Jambo unalopaswa kulifanya ni kumwaamini.

Wakati Arsenal inamsajili Henrikh Mkhitaryan, kisha Aubameyang na hapo Alexandre Lacazette tayari alikuwa kwenye kikosi chao, watu walikuwa wakiwaza itakuwaje hiyo fowadi ya Arsenal utakapokabiliana nao.

Lakini, Emery ameshindwa kuja kuleta matumizi sahihi ya wachezaji hao, anawapa nafuu wapinzani wake na sasa timu ipo nafasi ya sita kwenye msimamo huko.

Advertisement