MTAA WA KATI : Nimeanza kuupenda wimbo wa Ole At The Wheel

Tuesday April 23 2019

 

By Said Pendeza

Ole at the wheel. Huu wimbo uliimbwa sana na mashabiki wa Manchester United kati ya Desemba hadi Februari.

Hakuna kilichokuwa kikiwazuia wasiimbe wimbo huo.

Ulikuwa wimbo wa kumtukuza kocha wao mpya, Ole Gunnar Solskjaer.

Nyakati zilikuwa tamu. Kama kwenye penzi jipya tu, si kitu cha kushangaza kusikia neno kwanini hatukujuana mapema. Basi hivyo ndivyo nililivyokuwa penzi la Ole na mashabiki wa Man United. Walimwimbia nyimbo zote na yeye akawatoa mahali walipo na kuwapeleka walipokuwa wanapahitaji. Pale kwenye Top Four. Matumaini yakarudi upya na Ole akaonekana mwokozi wao.

Wapiga debe wakapiga sana kulifanya daladala la Ole kupata abiria, kwamba safari yao itakuwa salama kwa sababu yeye ndiye dereva, ameshika usukani. Ole at the wheel.

Akaja kuwavuruga hadi mabosi wa United alipowatupa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wababe wa Ufaransa, Paris Saint-Germain na Kylian Mbappe wao uwanjani.

Advertisement

Matokeo ya 2-0 Old Trafford yalifuta ndoto. Lakini, Ole alikwenda kupindua meza Paris, aliposhinda 3-1 na kuifikisha Man United robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Bosi kubwa Ed Woodward naye akakubali kupanda basi la Ole akiamini ni dereva mzuri, safari yake atafika salama. Wakampa mkataba wa kuwa kocha wa kudumu, kwasababu kule nyuma alikokuwa akifanya yake, alikuwa kocha wa muda tu, tena waliyekuwa wamemkopa kutoka Molde. Ole akapewa kazi ya kudumu Old Trafford.

Wengi waliamini ni uamuzi sahihi, wachache bado waliona Mauricio Pochettino aliyekuwa akitajwatajwa huko nyuma hiyo kazi ndiyo ingemfaa zaidi. Yakapita ya kupita. Ole akaanza maisha yake Old Trafford kama kocha mkuu.

Maisha yalianza vyema, akashinda mechi ya kwanza. Baada ya hapo, hadi kufikia sasa, Ole ameshinda mechi mbili kati ya nane. Amefungwa na Arsenal hapo, ndio walioanza kumtia gundu. Akafungwa na Wolves kwa kugeuzwageuzwa, Barcelona mara mbili na hapo juzi Everton nao wamejipigia.

Tena Everton wameweka rekodi kabisa wakishinda 4-0 matokeo ambayo haijawahi kukumbana nayo kwenye ligi miaka ya karibu. Man United inaonekana kurudi nyuma kwa kasi ya ajabu sana.

Imefungwa mfululizo ugenini, ikienda inachapwa tu mara tano sasa. Mechi ya marudiano na Barca, makosa yalikuwa mengi wakachapwa 3-0, kisha Ole akawaambia wachezaji wake hawajitumi na kupiga mkwara kwamba kuna watu wataondoka mwisho wa msimu.

Kidonda cha Nou Camp hakijapona, amekumbana na maumivu mengine Goodison Park. Sasa ni dhahiri Top Four inaelekea kuwashinda Man United na hilo likitokea hawatakuwapo kwenye michuano ya Ulaya msimu ujao. Kama hawatakuwapo basi watajiweka kwenye hatari ya kuwakosa wachezaji inayowataka kuwasajili, lakini pia wanaweza wakapoteza wachezaji wao muhimu kama Paul Pogba na David De Gea.

Kitu kinachowaumiza zaidi mashabiki wa Man United ni ule wimbo sasa kutumiwa na wapinzani kama kejeli. Kwa sasa mashabiki wa upinzani ndiyo wanaoimba wimbo wa Ole At The Wheel. Kwa vipigo hivyo vya siku za karibuni dereva Ole anakwenda kuwaua.

Kesho Jumatano wanacheza na Man City. Man City inayotaka ubingwa. Man United iliyotoka kupigwa mabao 7-0 katika mechi mbili zilizopita. Hapo unaweza kutabiri kinachokwenda kutokea na hautaonekana we mchawi.

Sijui kama Man United walifanya haraka kumuamini Ole au ni upepo mbaya tu unapita OT. Ni kitu kinazua maswali mengi. Man United imebadili makocha wanne sasa, lakini matokeo hayana tofauti. Shida nini wachezaji au makocha wanaoletwa wabovu? Inafikirisha japo hapo kwa wachezaji kuna uzito mkubwa. Phil Jones na Chris Smalling kwa mfano sio wachezaji wa kuchezea Man United bana kama mchezaji Gylfi Sigurdsson anachezea Everton.

Mpira wa siku hizi unahitaji watu siyo Jesse Lingard.

Advertisement