MTAA WA KATI : Mkimchukulia poa Solskjaer atawaumbua!

Tuesday January 29 2019

 

By Said Pendeza

MANENO mawili tu, usimchukulia poa Ole Gunnar Solskjaer. Man United yake wakati ilipokuwa ikiishinda Cardiff City, likaibuka suala la kusema kwamba anapiga vibonde. Likaja suala la kwamba atakapocheza dhidi ya vigogo, watu watafahamu kiwango cha timu yake.

Mara huko na huko, ikaja mechi ya Tottenham Hotspur. Wengi waliamini hapo ndipo patakapokuwa mwisho wa fungate ya kocha huyo. Lakini dakika 90 zilipomalizika, Ole aliondoka Wembley na pointi zote tatu.

Sawa, mwisho wa mechi kipa wake, David De Gea, ndiye aliyekuwa akisifiwa kwa kiwango chake, lakini kwa namna ambavyo alipanga kikosi chake na mtindo alioutumia kwenye mechi hiyo, ilitosha kumpa Ole sifa zake.

Kwanza, Ole aliwataka wachezaji wake kucheza kwa nidhamu kubwa. Lakini, kingine aliwataka mabeki wake wa pembeni na timu yake kwa jumla kuondoka kwenye eneo la nyuma, kulifanya goli lao kuwa mbali na wapinzani. Mwanzoni ilionekana kama Ole amewakamata tu wachezaji wa Man United kisaikolojia, lakini kwa namna alivyokuwa na mbinu hizo kwenye mechi hiyo ya Spurs, ilionyesha wazi kuna kitu kingine cha ziada kutoka kwa kocha huyo.

Ole aliwatambua mabeki wa Spurs wana uwezo mkubwa sana wa kupiga pasi. Kitu ambacho amekifanya, alimwaanzisha kiungo Jesse Lingard kucheza kama namba 9 bandia. Lingard ana kasi na anakaba, hivyo kumchezesha kwenye eneo hilo, liliwavuruga Spurs na lilimvuruga zaidi kocha mwenzake, Mauricio Pochettino. Lingard aliwabugudhi mabeki wa Spurs kila walipokuwa na mipira. Aliwakalia kooni.

Kitu kingine alihakikisha Christian Eriksen na Dele Alli hawapati muda mwingi wa kuwa na mpira. Mabeki wake wa pembeni, Luke Shaw na Ashley Young walisogea mbele zaidi kubinya mianya yote ambayo Spurs ingeweza kutumia kuleta matatizo kwa kipa wao De Gea.

Sawa kuna mipira iliyopita na kumkukuta De Dea, lakini mfumo aliotumia Ole ulikuwa na msaada mkubwa kwenye matokeo hayo.Ikaja mechi dhidi ya Arsenal. Kigongo kingine cha ugenini.

Kwa msimu huu, Arsenal imekuwa na rekodi nzuri inapocheza dhidi ya timu za kwenye Top Six. Imeonekana kuwa na ujuzi mzuri wa kuzicheza mechi ngumu chini ya kocha wao, Unai Emery. Lakini Ole alimzidi kimbinu mpinzani wake.

Kitu cha kwanza, Ole alitumia washambuliaji wenye kasi kwenye fowadi yake, akimpanga Alexis Sanchez, Lingard na Romelu Lukaku. Kitu alichokuja kumvuruga kabisa mpinzani wake Ole licha ya kwamba alikuwa na namba 9 wa asili, Lomelu Lukaku, lakini hakumchezesha kwenye eneo hilo. Alimtumia Lingard kucheza namba 9 bandia. Alichofanya akamchukua Lukaku akamtumia pembeni upande wa kulia na Alexis Sanchez alikuwa upande mwingine.

Ole aliisoma Arsenal mabeki wake wa pembeni wanapanda sana mbele kushambulia, hasa huo upande wa kulia, hivyo alimweka Lukaku kwenye eneo hilo kukomesha hilo. Hiyo ni mbinu iliyofanikiwa.

Kisha alifahamu wazi mabeki wengi wa Arsenal hawana kasi, hivyo alitumia washambuliaji wake wenye kasi kuwafanya wanapokuwa na mpira na kufanya mashambulizi, basi wafanye kwa haraka kuwafanya Arsenal kuwa wachache kwenye eneo lao. Hilo ndilo lililofanyika.

Mabao yote yaliyofungwa dhidi ya Arsenal kwenye mechi hiyo, yalitokana na ushapu wa fowadi ya Man United ambayo iliwafanya Arsenal mabeki wao kushindwa kwenda na kasi na matokeo yake kujikuta wakiwa wachache katika eneo lao la kulinda. Walifungwa bao la kwanza, bao la pili na la tatu kwa staili hiyo hiyo.

Ole alisema hakupata shida sana kwenye mechi hiyo alichofanya ni kuisoma tu video ya miaka 10 iliyopita, wakati Arsenal ilipofungwa pia 3-1 na Man United ikiwa na Cristiano Ronaldo, Wayne Rooney na Ji-sung Park walipofanya mashambulizi ya kushtukiza kupata matokeo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kwa staili ile ile ya mashambulizi ya kushtukiza, Ole alitumia tena mbinu zilezile akapata matokeo.

Kimtazamo unaliona hili ni jambo la kawaida, lakini Arsenal inapaswa kujitazama sana. Ina maana bado inacheza kwa staili ileile katika kipindi cha miaka 10. Ina maana staili ya uchezaji wa kocha wake wa zamani Arsene Wenger na Unai Emery zinafanana au?
Inapaswa kubadili na inahitaji kuwa na mabeki walioshapu kwenye ulinzi wao kukwepa kupoteza mechi kwa staili hiyo.

Lakini hilo lilimeonyesha pia Ole ana kitu cha ziada kwenye mbinu zake za ufundishaji na si kwamba anashinda tu kwa kuhamasisha.

Jambo ni moja tu, msichukulie poa Ole, atawasumbua!

Advertisement