MTAA WA KATI : Mane anavyonufaika kwa kivuli cha Salah, Firmino

Muktasari:

  • Tangu mwaka huu uanze, Mane amekuwa mmoja kati ya wachezaji waliofunga mabao mengi kwenye Ligi Kuu England. Amefunga mabao tisa. Ni kitu kisichopingika kwa sasa huduma yake imekuwa muhimu kwelikweli huko Liverpool kuliko ya mwingine yeyote yule.

HIVI ndivyo maisha yanavyokwenda kasi. Sadio Mane ndio jina linalotamba huko Liverpool kwa sasa. Mohamed Salah amepoteza yale makali yake. Msimu uliopita muda kama huu, huko Liverpool kila kitu kilikuwa Mo Salah.

Kwa wakati huu, Mane ndiye mtu muhimu huko Liverpool. Anatajwa kila kona kutokana na mabao yake.

Juzi Liverpool ilipambana kupata matokeo muhimu dhidi ya Fulham. Ni Mane aliyefanya mambo yake kufanikisha hilo.

Tangu mwaka huu uanze, Mane amekuwa mmoja kati ya wachezaji waliofunga mabao mengi kwenye Ligi Kuu England. Amefunga mabao tisa. Ni kitu kisichopingika kwa sasa huduma yake imekuwa muhimu kwelikweli huko Liverpool kuliko ya mwingine yeyote yule.

Yupo kwenye ubora wake kabisa. Mechi 11 mabao 11 katika mechi za karibuni alizocheza kwenye michuano yote. Dhidi ya Fulham, matokeo ambayo Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp na timu yake waliyahitaji zaidi kurudi kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo, Mane alifunga moja na kusababisha penalti ya ushindi iliyopigwa na James Milner.

Kwa wakati huu unapokabiliana na Liverpool mtu unayepaswa kumchunga ni Mane. Kitu ambacho Liverpool ilifaidika kwa kipindi cha karibuni ni kwamba kwenye mechi zao zote, wapinzani wamekuwa wakiwatolea macho ni Mo Salah na Roberto Firmino.

Mane amekuwa na faida moja hafikiriwi. Lakini, sasa ataanza kufikiriwa. Kwa sababu ndiye mtu hatari kuliko wenzake wote. Kivuli cha Mo Salah na Firmino kilimbeba Mane, timu pinzani ndani ya uwanja zinakuwa hazina hesabu naye, hapo ndipo anapowajeruhi. Hilo limejionyesha kwenye mechi za karibuni.

Mo Salah amekuwa akiwekewa ulinzi mkali sana, sambamba na Firmino. Mane amekuwa akipewa unafuu na ndio maana hadi sasa ameshafunga mabao 17 kwenye Ligi Kuu England, mengi kuwahi kufungwa na Msenegali yeyote kwenye ligi hiyo ndani ya msimu mmoja.

Wapinzani wanakuwa wanawaza vile Salah anavyokimbia haraka na kufunga. Wanawaza vile Firmino anavyohamisha mipira na kupiga pasi za mabao. Mane anakuja kupewa uzito mdogo kwenye orodha ya wachezaji hatari. Wapinzani waliking’amua hilo, basi Kocha Klopp atakuwa kwenye wakati mgumu.

Jambo hilo ndilo linalowatia watu shaka kwamba huenda wasishindwe kuzimalizia mbio za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu. Mo Salah amekuwa rahisi sana kumdhibiti. Kutegemea mabao kutoka kwa mtu mmoja si jambo zuri. Ujanja mwingine anaoufanya Mane ni ile staili yake ya kucheza mbali na goli.

Anashambulia akitokea pembeni. Anacheza kutokea pembeni na kukimbilia golini katikati kwa haraka sana. Kimsingi ukimtazama, Mane anakuwa pembeni, lakini anapopata mpira kwa haraka sana anakimbia kwenye eneo la hatari.

Jambo hilo linamfanya awe amegusa mpira mara nyingi ndani ya boksi la wapinzani kuliko ilivyokuwa misimu uliopita. Amelionyesha hilo hata kwenye mechi dhidi ya Fulham. Mo Salah ndiye aliyekuwa akicheza ndani ya boksi, lakini mpira aliogusa kwenye eneo hilo amemzidi Mane kwa kiwango kidogo sana. Hivyo ndivyo ilivyo kwenye tafsiri ya wakati.

Kwa wakati huu, mchezaji anayembeba Klopp ni Sadio Mane. Alimbeba Klopp kwenye mechi dhidi ya Bayern Munich na amefanya hivyo kwenye mechi kadhaa zilizopita. Hakika ndiye silaha mpya ya Liverpool kwa wakati huu.