MTAA WA KATI : Man United haijulikani lini mwisho wa shida zao

Muktasari:

  • Man United imeshindwa kuandikisha ushindi mbele ya timu ambayo imepoteza mechi zake 22 kati ya 24 zilizopita. Lakini, pengine wakati mchezo huo unafanyika kulikuwa na timu zinazofanana tu viwango.

HAKUNA kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Hilo ndilo linalowahusu Man United. Lakini, hilo sio tatizo kubwa linalowakabili, kwa hali ilivyo kwa sasa hawaonekani kama mambo yatatumia ndani ya miaka ya karibuni.

Shida haijulikani ni wachezaji au makocha? Hakuna mashaka wachezaji wataletwa kwenye dirisha lijalo la usajili wakati Ole Gunnar Solskjaer atakapohitaji kukijenga upya kikosi chake, lakini suala la wachezaji kuletwa limeshafanyika sana huko nyuma na mambo yamegoma kukaa sawa.

David Moyes, Louis van Gaal na Jose Mourinho wote walipewa pesa za kusajili, zaidi ya Pauni 600 milioni zimetumika tangu alipoondoka Sir Alex Ferguson. Lakini, hakuna nafuu, mara ya nne katika miaka sita tangu Ferguson alipoondoka, Man United inamaliza ligi nje ya Top Four.

Hilo ndilo walilostahili. Kwenye mchezo wao dhidi ya Huddersfield hawakuonekana kabisa kuwa na nia ya kutaka kushinda mchezo huo ili walau kuendelea kwenye mambambo ya kuwamo kwenye Top Four.

Man United imeshindwa kuandikisha ushindi mbele ya timu ambayo imepoteza mechi zake 22 kati ya 24 zilizopita. Lakini, pengine wakati mchezo huo unafanyika kulikuwa na timu zinazofanana tu viwango.

Sawa Huddersfield wameshuka daraja, lakini kwa mwendo ambao Man United ilikuwa ikienda nao, ulikuwa unatishia kwelikweli. Kushinda mechi mbili kati ya 11 za karibuni, hicho si kiwango cha kuvunia kabisa kwa Man United.

Hali ni mbaya na haionekani itakwisha lini. Maisha yamegeuka kwa haraka sana. Siku zimekwenda kasi sana kwa kocha Ole. Mechi zake 11 za mwanzo, alishinda 10 na kutoka sare moja tu.

Kwa wakati huo, Arsenal, Chelsea na hata Tottenham wote walionekana wataachia tu zile nafasi zao wanazoshika kwenye msimamo wa ligi.

Ilifika wakati Man United hadi waliingia kwenye ile Top Four na kuonekana kama mambo yangemalizika hivyo. Kufumba na kufumbua, mechi 11 za karibuni, Ole ameshinda mara mbili tu, sare mbili na vingine vyote vichapo. Man United imefungwa na timu kama Wolves mara mbili. Imefungwa na Everton 4-0. Wamefungwa na Watford na West Ham.

Ni aibu.

Kitu kibaya, kwenye mechi hizo hakuna hata moja ambayo hawajaruhusu wavu wao kuguswa. Huo ni mwendo wa ovyo zaidi kuwahi kuutembea kwenye maisha yake ya kisoka tangu miaka ya sabini huko.

Kama utakuwa umeitazama Man United kwenye mchezo wao na Huddersfield basi bila shaka utakuwa na matatizo milioni moja yanayohitaji kupatiwa utatuzi kwenye kikosi hicho. Man United imemegukameguka.

Huwaoni kuwa na mpango wa kutafuta goli, kuwa na mpango wa kuzuia wasifungwe.

Alexis Sanchez amekosa maajabu. Paul Pogba amekuwa wa aina ileile licha ya kugongesha mwamba mara mbili. Marcus Rashford amepoteza shabaha yake ya goli, naye anahitaji nafasi nyingi kufunga mara moja.

Hayo ndio mengi yanayoigharimu timu hiyo. Imekosa huduma ya wale wafungaji hatari kama alivyokuwa Robin van Persie kwenye kikosi chao.

Kwenye ligi ya kisasa, unahitaji kuitumia vyema kila nafasi inayopata kwa sababu hutazamii kuona zikipatikana nyingi ndani ya mchezo mmoja. Hayo ndio maisha magumu yanayoikabili Man United kwa sasa. Yanahitajika mabadiliko makubwa.