MTAA WA KATI : Liverpool kuondoa gundu la ubingwa Aprili 14?

Tuesday March 26 2019

 

By Said Pendeza

PALE juu kwenye kilele cha msimamo wa Ligi Kuu England pamebadilika tena wikiendi iliyopita.

Liverpool wamewaondosha kileleni Man City baada ya ushindi wao kwa Fulham. Lakini, kwenye nafasi hiyo ni kama mchezo wa kukaa na kutoka.

Liverpool wapo kileleni, lakini wakiwa na mchezo mmoja zaidi ya wapinzani wao hao Man City.

Liverpool wanaongoza na pointi zao 76, mbili zaidi ya Man City. Walitumia vyema fursa waliyoipata wakati Man City walikuwa kwenye shughuli ya kucheza na Swansea City kwenye Kombe la FA.

Kitu muhimu ni kuongoza ligi, kutangulia mechi hilo ni jambo jingine. Wakati mwingine viporo huwa vinachacha.

Hivyo, inachokiomba Liverpool ni matokeo ya sare tu kwa Man City katika mechi yao ya kiporo. Jambo hilo linazidisha utamu kwenye ligi hiyo kwamba huenda vita yake ikaendelea hadi mechi ya mwisho Mei 12, kwa sababu inavyoonekana hakuna timu inayoonekana kufanya mchezo wa kupoteza pointi.

Lakini, kinachoelezwa ni kwamba Jumapili ya Aprili 14 itakuwa siku pekee ya kutambua mbio za ubingwa wa ligi hiyo zitakavyokuwa. Siku hiyo pengine ndio itakuwa mwisho wa kumaliza kitendawili cha kutambua bingwa wa msimu huu ni nani.

Siku hiyo, Man City watakuwa na mechi ngumu ugenini kwa Crystal Palace huko Selhurst Park. Lakini, siku hiyo hiyo, Liverpool nao watakuwa na mechi ngumu zaidi, kuwakabili Chelsea wanaofukuzia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Mechi hiyo itapigwa Anfield. Mechi hiyo inarudisha kumbukumbu za msimu wa 2013/14. Liverpool walikosa ubingwa na kuwapa nafasi Man City baada ya kupoteza 2-0 na Chelsea, ambapo Gerrard alianguka kumfanya Demba Ba kwenda kufunga kirahisi.

Mechi ile ilikuwa Aprili 27 na hii inakuja Aprili tena. Hilo linawakabili Liverpool. Lakini, Man City nao wana kibarua cha kwenda kuwakabili Palace waliopo kwenye ubora wao. Kipindi kile Man City waliwafunga hao hao Palace.

Hivyo, historia kama vile inaweza kwenda kujirudia hapa. Wakati ule Man City ilishinda 2-0 shukrani kwa mabao ya Edin Dzeko na Yaya Toure.

Baada ya hapo, Man City hawakutazama nyuma, lakini Liverpool wakaja kufanya uzembe wakipoteza uongozi wao wa mabao 3-0 na kutoka sare ya 3-3 na Palace.

Hivyo, Aprili 14 mwaka huu itakuwa siku muhimu kwa vigogo hao wawili, Man City na Liverpool kutambua hatima yao kwenye mbio hizo za ubingwa wa Ligi Kuu England.

Kabla ya kufika siku hiyo, Man City wao watakuwa na mechi nyepesi dhidi ya Fulham na Cardiff City. Liverpool wao kabla ya kuwakabili Chelsea, watakuwa na mechi dhidi ya Tottenham na Southampton uwanjani St Mary’s. Mambo ni magumu.

Liverpool wao watakuwa na kazi ya kuwakabili FC Porto. Jambo kubwa ni hiyo Aprili 14 inayoonekana kwamba ndio itakayoweka mambo hadharani kuhusu mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Gundu la Aprili kwa Liverpool litajirudia au safari hii watafanya kweli na kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England. Tusubiri.

Advertisement