MTAA WA KATI : Inapokuwa ngumu kuwa Karim Benzema

Tuesday November 19 2019

Inapokuwa -ngumu -Karim -Benzema-La Liga-Los Blancos -Ufaransa-

 

By Said Pendeza

KWENYE La Liga msimu huu, amefunga mabao mengi kuliko wote. Ndiye kinara na mabao yake tisa. Ameasisti pia mara tatu, jambo linalomfanya awe amehusika kwenye mabao 12 kwenye La Liga hadi sasa. Kwa ujumla wake, Los Blancos imefunga mabao 25, hiyo ina manaa mabao 12 yametokana na staa huyo na mengine 13 ndo wamehusika wengine.

Huyu ni Karim Benzema. Sio namba tisa halisi, lakini hiyo ndiyo namba anayovaa kwenye jezi yake. Sio mfungaji mahiri, lakini ameshawahi kubeba Pichichi, tuzo anayopewa kinara wa mabao kwenye La Liga.

Ni staa mkubwa Ufaransa, lakini hachezei timu yake ya taifa. Sio kwa kupenda, bali kwa kulazimishwa. Jumamosi iliyopita, hakukuwa na mechi za ligi.

Kulikuwa na mechi za kimataifa, kitu ambacho Benzema kimekuwa kitu kisichomhusu. Benzema ameibuka na kuzungumzia kukosekana kwenye soka la kimataifa. Ufaransa wamemfungia kabisa milango mchezaji huyo, tena kwa sababu zisizokuwa za kimpira.

Ingekuwa kitu rahisi tu kwa Benzema kuamua zake kutulia tu wikiendi na kula starehe zake nyingine. Lakini, inamuuma kwa sabau wachezaji wenzake wote mastaa huko kwenye La Liga, wote wamekuwa bize kwenye timu zao za taifa. Wanakwenda kutumikia mataifa yao.

Bila ya shaka kitu hicho kinamuuma sana Benzema na hana namna zaidi ya kubaki tu akiomboleza. Kuna watu waliapa kuhusu yeye ushiriki wake kwenye kikosi cha Les Bleus.

Advertisement

Mwishoni mwa wiki mwenyewe alizungumzia uwezekano wa kulichezea taifa nyingine ya taifa, pengine inaweza kuwa Algeria kwenye asili yake. Ngumu kwa sasa.

Kikawaida, Benzema anaweza kuamua kuachana na uraia wake wa Ufaransa na kuwa raia wa taifa jingine analotaka yeye.

Lakini, kwenye ishu ya mpira, suala lake linakuwa gumu kwa sababu sheria za Fifa ziko wazi, mchezaji hawezi kuchezea zaidi ya nchi moja kwenye soka la kimataifa kama atakuwa amecheza mechi za kimashindano. Benzema amefanya hivyo akiwa na Les Bleus.

Kitu ambacho Benzema aombe kitokee ni rais wa shirikisho la mpira la Ufaransa, Noel Le Graet kutengua kauli yake.

Mtu huyo ndiye aliyefunga ukurasa wa Benzema kuichezea timu yake ya taifa na hakucheza tangu kesi yake ile dhidi ya mchezaji mwenzake, Valbuena mwaka 2015. Inakuwa ngumu kwa Benzema kwa sasa kwa sababu Ufaransa wanafanya vizuri. Mwaka jana tu hapo walifanya kweli Russia walipobeba taji la Kombe la Dunia.

Ufaransa ilibeba ubingwa na mafowadi Antoine Griezmann, Kylian Mbappe na Olivier Giroud. Watatu bado wapo kwenye ubora wao na wamekuwa chaguo la Didier Deschamps.

Utawaambia nini mashabiki wa Ufaransa kuhusu Benzema kama timu inafanya vizuri na washambuliaji waliopo. Ni ngumu na hicho ndicho kinachomuumiza Benzema.

Wengine wanamwona kwanza sio namba tisa, hivyo nafasi yake anayocheza kuna watu wengi sana wa wake ambao wanasubiri tu kwenye benchi huko Les Bleus.

Lakini, yote kwa yote Benzema atabaki kuwa Benzema. Real Madrid wanatambua thamani yake na ndio maana anabaki kuwa mtu muhimu kwenye kikosi chao. Anawasawaidia jambo kwamba anaweza kukosa bao la wazi akafunga ambalo wengine hawakulitegemea.

Real Madrid wanachoomba wao hasira hizo za kukosa soka la kimataifa zisimharibu staa wao. Ukweli ni kwamba Benzema hawezi kuwa na mapenzi na wikiendi hizi za mechi za kimataifa. Anamisi soka. Uwezo anao, dhamira anayo katika kuichezea timu, lakini shida yeye ni Karim Benzema na rais wa soka la Ufaransa, amesema hawezi kuichezea tena Les Bleus.

Advertisement