MKEKA WAKO : Man City watapata pointi tatu safi kwa West Ham

Friday February 7 2020

Man City watapata pointi tatu safi kwa West Ham,mechi za Ligi Kuu England,La Liga,Bundesliga,

 

By Samson Mfalila

KWA mara ya kwanza kutakuwa na mapumziko ya mechi za Ligi Kuu England ingawa yatakuwa tofauti na yanavyofanywa kwenye ligi za soka za nchi nyingine.

Ligi Kuu England imekuwa haina mapumziko na hasa kwa kuzingatia kuna utamaduni wao wa kuwepo kwa mechi zinazochezwa katika Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko wa utaratibu huo kuwachosha wachezaji wa England kiasi cha kufanya klabu za huko kutofanya vizuri katika mashindano ya klabu barani Ulaya.

Kwani kumekuwa na manung’uniko kuwa wachezaji wa timu za England wanacheza mechi nyingi sana, mfano zile za Ligi Kuu England, Kombe la FA, Kombe la Carabao, michuano ya Ulaya na mechi za timu za taifa.

Pengine hali hiyo inachangia kwa mastaa kuumia mara nyingine kutokana na ugumu wa ratiba za mashindano hayo,

Pia, kuna wadau wamekuwa wanalalamikia hali hiyo kwa kiasi kikubwa imesababisha England kutofanya vizuri katika mashindano makubwa ya soka kama yale ya Ulaya na Kombe la Dunia.

Advertisement

Wadau wamekuwa wakidai hali hiyo inatokana na wachezaji wa taifa hilo kucheza mechi nyingi kiasi cha kuwachosha wachezaji. Tumezoea kuona kwenye ligi kama zile za La Liga, Bundesliga na Serie A timu zikipewa mapumziko ya wiki mbili kwenye kipindi cha siku za Krismasi na Mwaka Mpya.

Mechi hizo husimama muda mfupi kabla ya Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya na baadaye kipute kuendelea baada ya mambo hayo kumalizika.

England sasa wamekuja na utaratibu tofauti wa kidogo wa mapumziko kwani mechi zao za ligi hazitasimama kabisa.

Kitu ambacho kitafanyika ni kuwa timu zitapata nafasi ya kupumzika wikiendi moja.

Kutakuwa kuna mechi chache zitakazochezwa ingawa zimepangwa kufanyika katika muda tofauti tofauti.

Kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo ni kuwa timu nane zitacheza mechi zao kesho na keshokutwa wakati timu nyingine 12 zitacheza mechi zao wikiendi ijayo.

Burnley, Bournemouth, Manchester City, Sheffield United na Wolves, ambazo zitacheza wikiendi hii zitapata nafasi ya kupumzika siku 13.

Wakati timu ambazo zitapata nafasi ya kupumzika kwa muda mrefu zaidi ni Manchester United na Chelsea ambazo angalau zitapumzika kwa siku 16 kwenye ratiba zao.

Kitendo cha kuwepo kwa mapumziko haya ya mechi za Ligi Kuu England ni mapinduzi makubwa kwenye soka la England.

Kutokana na ukweli kuwa kwa miaka mingi kumekuwa na upinzani mkubwa likija suala zima la kuwepo kwa mapumziko ya mechi za Ligi Kuu England.

Angalau mapumziko haya kwa kiasi kikubwa yanaweza kuzisaidia timu za England likija suala la zima la mastaa hao kupumzika.

Klabu saba za England zinacheza katika mashindano ya Ulaya nazo ni Arsenal, Chelsea, Liverpool, Manchester City, Manchester United, Tottenham na Wolves.

Timu hizo zinakipiga katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi ya Europa baadaye mwezi huu.

Wikiendi hii sasa timu nane zitacheza, ambapo Everton inaikaribisha Crystal Palace kesho na mechi nyingine Brighton itaikabili Watford.

Katika mechi zitakazopigwa keshokutwa Jumapili, Sheffield United itapambana na Bournemouth na Manchester City itavaana na West Ham.

Mechi kali zaidi inatazamiwa kuwa kwenye Uwanja wa Etihad ni wazi wenyeji Manchester City watapania kurejesha fomu yao baada ya kuonja kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Tottenham Hotspur.

Bila shaka watataka kupoza presha ya mashabiki wao wakati watakapovaana na West Ham. Kipigo cha Manchester City kilishangaza wengi na hasa timu hiyo ilivyobanwa kwa kipindi kirefu na Spurs.

Kipigo kile kilizua maswali na watu kuanza kuhoji hatma ya kocha wa timu hiyo, Pep Guardiola.

Kuna watu wameanza kujiuliza pengine kocha huyu amepoteza makali yake.

Hata hivyo, mchezo huu kwa ujumla wake hautakuwa rahisi kutokana na rekodi nzuri ya West Ham linapokuja suala zima la kucheza mechi za ugenini.

Jambo la ajabu ni kuwa West Ham inafanya vizuri zaidi katika mechi zao za ugenini kuliko vile inavyocheza nyumbani.

Hata hivyo, pamoja na hali hiyo ninawapa nafasi kubwa zaidi Manchester City kushinda mchezo huu.

Advertisement