MKEKA WAKO : Arsenal itachezea kichapo kwa Manchester City

Muktasari:

Arsenal na Manchester City ambazo ni miongoni mwa klabu vigogo za England zinafukuzia ushindi ili kufufua hadhi zao.

Macho ya wapenzi ya soka la England wikiendi hii yataelekezwa zaidi kwenye Uwanja wa Emirates wakati Arsenal itakapovaana na Manchester City.

Arsenal ikiwa chini ya kocha wa muda, Freddy Ljungberg itakuwa imepania kufanya vizuri katika mchezo huu ili kujiweka pazuri baada ya kusuasua katika siku za karibuni.

Kuyumba kwa Arsenal kuliilazimisha timu hiyo kumtimua kocha wake wa kihispania, Unai Emery.

Ljungberg anakabiliwa na kibarua kizito cha kurudisha ari ya timu hiyo kwani ni muhimu ukizingatia inakabiliana na timu inayotisha ya Manchester City.

Ili kurudisha matumaini yao, Arsenal itakuwa inamtegemea mfungaji wake hatari Pierre-Emerick Aubameyang, ambaye bila shaka atachungwa sana na mabeki wa Manchester City.

Manchester City nao wataingia wakiwa na maumivu kwenye mchezo huu kwani ni wikiendi iliyopita walijikuta wakipigwa mabao 2-1 na wapinzani wao wa jadi Manchester United tena kwenye uwanja wao wa Etihad.

Arsenal na Manchester City ambazo ni miongoni mwa klabu vigogo za England zinafukuzia ushindi ili kufufua hadhi zao..

Manchester City inayotetea taji lao la ubingwa ipo kwenye nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu wakati Arsenal ipo kwenye nafasi ya tisa.

Arsenal inaweza kujipa moyo kwenye mchezo huu angalau kwani Manchester City inamtegemea Gabriel Jesus pekee katika kupachika mabao. Hali hiyo imetokana na straika wao mwingine, Sergio Aguero kuwa majeruhi wakati Raheem Sterling yupo katika wakati mgumu kutokana na mabao kumkimbia.

Hali ni tete zaidi kwa City kutokana na kuyumba kwa beki yao katika siku za karibuni, ambapo imeshindwa kuzuia mabao katika mechi 10 zilizopita.

Hata hivyo, Manchester City inakabiliana na timu inayofanana nayo likija suala zima la beki kuyumba.

Arsenal itajipa moyo inaweza kupata ushindi kwenye mchezo huu baada ya kuiliza West Ham mabao 3-1, Jumatatu iliyopita.

Ingawa kuna watu wengine watasema kuwa walikutana na West Ham, ambao pia wana tatizo la beki.

Ushindi huu angalau uliisaidia Arsenal kukamata nafasi ya tisa, ikiwa pointi saba nyuma ya timu zinazoshika nafasi nne za juu.

Ingawa pia ina pointi saba juu ya timu ambazo zipo kwenye hatari ya kushuka daraja.

Arsenal ina rekodi ya kufunga mara kibao ingawa pia inakabiliwa na tatizo la kuruhusu sana kufungwa mabao. Kuna uwezekano Manchester City wakatumia udhaifu huo tena wa beki ya Arsenal na kuweza kuondoka na ushindi katika mchezo huu.

Arsenal itaingia katika mchezo huu ikiwa na rekodi ya kushinda mechi moja katika tisa za ligi.

Pia Arsenal haijaweza kupata ushindi katika mechi tano za ligi ilizocheza nyumbani.

Manchester City imepoteza mechi moja tu katika mechi tisa za ligi za ugenini ilizocheza hivi karibuni.

Manchester City sasa ili kufufua matumaini yao ya kutwaa ubingwa wanapaswa kushinda mechi za ligi.

Mechi hii dhidi ya Arsenal inawapa nafasi nzuri ya kupata pointi ukizingatia wana rekodi nzuri na mechi za ugenini.

Kutokana na hali hiyo, ninawapa nafasi kubwa zaidi Manchester City kuibuka na ushindi katika mchezo huo wa keshokutwa.