MAONI: Huu ndio wakati mwafaka wa Yanga kujikomboa na matatizo

Saturday June 9 2018

 

KATIKA maisha kuna nyakati ambapo mtu hupitia kwenye mitihani mizito inayoweza hata kumfanya akate tamaa.

Nyakati ambazo wengi huzipenda ni zile za raha. Ni nyakati ambazo maisha yanakuwa mazuri na hata kama huna nguvu huwezi kuonewa na yeyote yule.

Mtu huweza kutembea kibabe na kila mtu akiamini kuwa ana nguvu sana kumbe, hata mbwa koko akikukomalia anaweza kukukimbiza na kukutoa kijasho.

Ni kipindi cha tambo nyingi na maneno ya jeuri na kejeli.

Bahati mbaya kipindi hiki huwa hakidumu kwa muda mrefu. Raha hukatika kwa nukta chache kama kiasi cha kupepesa macho.

Baada ya hapo huja kile kipindi cha pili cha dhiki, ni kigumu ambacho mtu unakosa fedha na kufedheheka.

Ukiwa katika kipindi hiki kibaya katika maisha kila mtu atakukimbia na kukuona kuwa hufai.

Hata wale ambao ulikuwa ukitumia nao katika kipindi kile cha raha watakudharau na kamwe hutaamini kile unachokisikia kutoka kwao.

Kesho Jumapili mabingwa wa kihistoria wa soka nchini, Yanga watafanya mkutano wao mkuu katika bwalo la maofisa wa Polisi pale Oysterbay, jijini Dar es Salaam.

Yanga inafanya mkutano ikiwa katika kipindi cha pili cha maisha ya mwanadamu. Baada ya awali kutesa na kuwa na maisha mazuri chini ya ufadhili na uongozi wa mfanyabishara mashuhuri nchini , Yusuf Manji.

Lakini sasa mashabiki na wanachama wa Yanga wanalia kwa kadhia mbalimbali ambazo wamekuwa wakizipitia baada ya Manji kuachia ngazi Mei mwaka jana.

Klabu yao imepoteza kila kile kilichokuwa kizuri na imefikia hatua hata ya kushindwa kufanya usajili wa wachezaji wanaowataka na kusubiri wale wasiotakiwa na wapinzani wao wa jadi, Simba na Azam FC.

Hakuna kinachopendeza ndani ya Yanga kwa sasa ambayo imefikia hatua ya kushindwa kulipa hata mishahara ya wachezaji wake.

Baadhi ya wachezaji wamefikia hatua ya kuweka migomo baridi kwa sababu ya kukosa pesa. Aliyekuwa kocha wake mkuu, George Lwandamini alilazimika kuikacha timu hiyo na kukimbilia kwao Zambia baada ya kuona ukata ukiendelea kumtesa ndani ya klabu hiyo.

Yanga imekuwa haitishi tena uwanjani kwani imefungwa na timu ambazo hazikuwa hata na hadhi ya kushindana nayo wakati ilipokuwa imetawaliwa na neema mwaka mmoja na nusu uliopita.

Kipindi kama hiki kilishawahi kupitiwa na wapinzani wao wa jadi, Simba na kuwafanya kukosa ubingwa wa Ligi Kuu kwa miaka mitano mfululuzo.

Leo hii Simba imebeba ubingwa wa Ligi Kuu ikiwa chini ya Bilionea Mohamed Dewji ‘MO’ ambaye ameleta mafanikio hayo Msimbazi.

Wakati Simba ilipokuwa katika hali hiyo ya dhiki, Yanga ilikuwa inacheka na kuinyanyasa kwa kutoa kebehi na ilikuwa ikiinyang’anya wachezaji kadiri ilivyojisikia. Leo kibao kimebadilika na Simba ndio inayowacheka watani zao.

Yote kwa yote, Yanga wanakwenda kufanya mkutano wao mkuu ili kubadilisha mustakabali wa maisha ya baadaye ya klabu yao.

Lakini wakati lengo likiwa ni hilo, kabla ya mkutano huoo, tayari kuna figisufigisu za wanachana na mashabiki wa Yanga zikionyesha klabu hiyo imepoteza umoja wake uliokuwapo miaka ya nyuma.

Tofauti kubwa ya baadhi ya wanachana ni mfumo gani utumike kuindesha klabu hiyo.

Wapo wanaoshangilia kuhusu habari za kurudi kwa Manji na wengine wakionekana kuponda mtazamo huo.

Wanaopinga wanasema haiwezekani klabu hiyo kuendeshwa na mtu mmoja. Huku wakitaka mfumo wa hisa utumike kwa watu wengi wenye uwezo kuweza kuingoza klabu hiyo yenye maskani yake katika Mitaa ya Twiga na Jangwani.

Mwanaspoti tunasema wanachama wa Yanga wote wanapaswa kuwa kitu kimoja na kufanya uamuzi wenye busara kwa ajili ya klabu yao.

Kila mmoja ameona jinsi klabu ilivyokuwa ikipoteza umaarufu wake sidhani kama wanataka kurudi tena katika hali hiyo. Huu ni muda mwafaka kuweka silaha chini na kuijenga Yanga.

Yote kwa yote, Mwanaspoti tunahimiza umoja wa wana Yanga wote katika kuiletea mafanikio klabu yao kwa kuwa umoja ni nguvu.

Advertisement