MKEKA WAKO : Liverpool itapeta kwa Brighton kama kawaida

Muktasari:

Liverpool ndio inaongoza Ligi Kuu England ikiwa na pointi 37 wakati nafasi ya pili ipo Leicester City ikiwa imejikusanyia pointi 29.

Liverpool ina nafasi ya kuendeleza wimbi lake la ushindi wakati itakapoivaa Brighton kwenye mechi ya Ligi Kuu England kesho Jumamosi.

Mechi hiyo Liverpool wanaipiga nyumbani kwenye uwanja wao wa Anfield, ambapo ni fursa njema kwao kuendelea kuchanja mbuga kwenye mechi za ligi ni wazi nawapa nafasi ya kutoa dozi ya mabao mengi katika mchezo huu bila ya ubishi.

Liverpool ndio inaongoza Ligi Kuu England ikiwa na pointi 37 wakati nafasi ya pili ipo Leicester City ikiwa imejikusanyia pointi 29.

Manchester City inayotetea taji lake ipo kwenye nafasi ya tatu ikiwa na pointi 28.

Brighton kwa upande wao nao watakuwa wanasaka kujitutumua kupanda ngazi ya msimamo wa ligi kutokana na kuwa na pointi 15 kwenye nafasi ya 12.

Sio siri kuwa Liverpool wako moto kwa hivi sasa kwa hiyo hakuna cha kuwazuia kuwaliza Brighton.

Ingawa ni kweli kuwa Liverpool wamekuwa wanashinda kwa tabu mechi zao huku mara ya mwisho wakipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Crystal Palace.

Liverpool wamekuwa wana bahati na maamuzi ya video za waamuzi (VAR), ambapo ngekewa hiyo iliendelea kwenye mechi dhidi ya Palace, wikiendi iliyopita.

Mfano James Tomkins aliifungia Palace bao la kichwa katika kipindi cha kwanza cha mchezo dhidi ya Liverpool lakini bao hilo lilikataliwa.

Sadio Mane alipachika bao la kwanza la Liverpool katika dakika ya 49 lakini Wilfried Zaha aliisawazishia Palace lakini na baadae Roberto Firmino akapachika bao la ushindi la Liverpool.

Liverpool ilishinda kwa shida mchezo huo huku kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp akidai kuwa uchovu ndio umekuwa unachangia timu yake kucheza chini ya kiwango.

Klopp bila shaka sasa ataongoza kikosi chake kuhakikisha timu yake inapata ushindi mnono katika mchezo huu.

Habari njema kwa Liverpool ni kuwa Brighton wana rekodi mbovu sana linapokuja suala la mechi za ugenini.

Katika siku za karibuni hawajaweza kushinda mechi sita mfululizo za ugenini jambo ambalo linafanya watu wengi waamini kuwa Liverpool ina nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi mkubwa katika mchezo huo.

Kikosi cha Liverpool katika mchezo huu kinatazamiwa kuundwa na Alisson, Van Dijk, Lovren, Robertson, Alexander-Arnold, Fabinho, Wijnaldum, Henderson, Oxlade-Chamberlain, Firmino, Mane.

Brighton katika siku za karibuni ni kama imepotea kwani kuna wakati ilikuwa inatisha kutokana na kushinda mechi tatu kati ya nne lakini siku za karibuni imekuwa kama ipo taabani.

Katika mechi za karibuni, Brighton ilipigwa mabao 3-1 na Manchester United na pia ilikula kichapo cha mabao 2-0 kwa Leicester.

Hata hivyo, kocha wa Brighton, Graham Potter amejizolea sifa kwa kuifanya timu hiyo kucheza soka la kushambulia zaidi tofauti na ilipokuwa chini ya mtangulizi wake Chris Hughton.

Ingawa wana rekodi mbovu ya mechi za ugenini kwani wameambulia pointi moja na mabao mawili tu kwenye mechi zaoi ugenini.

Katika mchezo huu, kikosi cha Brighton kinatazamiwa kuwa na Ryan, Duffy, Webster, Montoya, Burn, Stephens, Mooy, March, Propper, Maupay, Trossard.