MAONI YA MHARIRI: Kwa uamuzi huu, Simbu, RT wana mzigo wa lawama

Muktasari:

  • Inaelezwa mabosi wa RT wamekubaliana kutomjumuisha Simbu kwenda Australia

MASHABIKI wa Riadha nchini bado wamepigwa na butwaa baada ya kusikia mwanariadha tegemeo wa timu ya taifa ya mchezo huo, Alphonce Simbu hatashiriki Michezo ya Madola itakayofanyika mwakani nchini Australia.

Jina la Simbu halijajumuishwa kwenye michuano hiyo ya pili kwa ukubwa duniani baada ya Olimpiki na inayofanyika kila baada ya miaka minne kwa sababu tu ya kuingilia na ratiba ya Mbio za London Marathon 2018.

Inaelezwa mabosi wa RT wamekubaliana kutomjumuisha Simbu kwenda Australia ili kuitikia mwaliko wa London Marathon ambao yatafanyika siku chache kabla ya Madola itakayofanyika Aprili mwakani.

Yapo madai Simbu ametaka akakimbie London Marathon kuliko Madola, ikielezwa inatokana na mbio hizo binafsi kuwa na fedha nyingi kuliko Madola ambako mwanariadha wanaambulia medali na posho kidogo. Mwanaspoti haitaki kuamini Simbu ndiye aliyefanya maamuzi ya kukacha mashindano ya Madola na kwenda London Marathon, lakini pia hawezi kukwepa lawama hizi anazoelekezwa sasa kwa kitendo cha kuonekana sio mzalendo.

Tunaamini lipo shinikizo nyuma ya maamuzi yake naye ameshindwa kukataa, lakini bado alipaswa kujitokeza hadharani na kuweka msimamo wake, kwamba sio mapenzi yake yaliyomsukuma kupelekwa London badala ya Madola.

Kukaa kwake kimya kunamfanya achukuliwe kama mtu asiye na uzalendo na pengine labda ameangalia fedha zaidi kuliko uzalendo kwa nchi yake, jambo ambalo Mwanasspoti hatutaki kuamini moja kwa moja.

Kwa nini hatutaki kuamini? Ni kwa vile Simbu ni askari hivyo suala la uzalendo kwake ni kama mhimili, ila ni wazi kuna kitu kilichopo nyuma yake na ndio maana amekuwa mkimya kuweka bayana kilichomtatiza hata ikawa hivyo.

Ili kuweza kukata mzizi wa fitina ni lazima ajitokeze sasa na kuweka bayana kukatwa kwa jina lake kwa mashindano ya Madola hakukutokana na mapenzi yake ili Watanzania wamsamehe, vinginevyo wataendelea kumhukumu. Pia kwa walioshinikiza mwanariadha huyo akakimbie mbio za London badala ya Madola ni wazi wameshindwa kujipima na kuona Simbu ni tegemeo katika kuleta heshima kwenye mashindano hayo makubwa.

Ni muda mrefu Tanzania ilikuwa ikichechemea kwenye riadha duniani, lakini ujio wa Simbu na wenzake kadhaa kama Emmanuel Giniki kumesaidia kuamsha ari kwa riadha Tanzania na ilikuwa nafasi nyingine ya kutetemesha kimataifa.

Simbu ameibeba Tanzania katika Mashindano ya Dunia ya Riadha yaliyofanyika London hivi karibuni na kila mtu alikuwa na hamu ya kuona akienda Australia kutuletea medali kama alivyojitahidi kupambana kwenye Olimpiki 2016 na kumaliza nafasi ya tano nchini Brazili.

Hivyo matarajio ya Watanzania walio wengi yaliwekwa kwa mwanariadha huyo na wenzake ili kuendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania na hata kauli za kumsakama zinazooka kila upande zinatokana na sababu hiyo kuu. Ndio maana tunadhani pande zote mbili, yaani Simbu na RT hawawezi kukwepa mzigo wa lawama kwa sababu, suala hili lilikuwa ndani ya uwezo wao na kulikuwa na nafasi kwao ya kupima ama kusoma alama za nyakati mapema.

Hakuna anayefurahia baada ya kubaini kuwa tumepoteza nafasi ya kubeba medali katika Madola, ikizingatiwa kuwa kwa sasa Simbu ndiye kama mboni ya jicho la Watanzania katika riadha. Mafanikio yake ya muda mfupi akianza kwa kunyakua medali ya dhahabu katika Mumbai Marathon kisha kumaliza nafasi ya tano katika Olimpiki na kunyakua medali ya Shaba mbio za dunia imechochea watu kumfuatilia zaidi.

Ingawa maamuzi yameshafanyika kwa sasa, lakini ni wazi jambo lolote ambalo litaitokea timu ya Tanzania nchini Australia ikafanya vibaya bila kuambulia medali, vidole vya lawama vitaelekezwa kwao na wajiandae kubeba mzigo huo. Kama walivyoshangazwa viongozi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) na nyota wa zamani wa riadha walioitikisa dunia katika mchezo wa riadha, vivyo hivyo ndivyo Watanzania wapenda michezo na hasa riadha walivyotikiswa.

Kwani hakuna aliyetegemea kama Simbu na RT waliamua kuchukua maamuzi hayo magumu ambayo yameleta mshtuko kwa wapenda riadha waliokuwa na matumaini makubwa na mwanariadha.