Kwa mbeleko hizi, lazima tuchemshe kimataifa

Sunday September 23 2018

Kuna mambo hutokea Tanzania tu na kwingineko ni nadra kuyasikia au kuyaona. Ni Tanzania tu ambako klabu inaweza kuomba kuahirishiwa mechi zao ili iende kwenye bonanza na ratiba kupanguka kwa ajili ya mechi za ndondo!

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imetangaza kuzifuta mechi zijazo za katikati ya wiki zinazozihusu Simba na Yanga, ili kuzipa nafasi ya maandalizi ya mchezo wao wa wikiendi ijayo.

Ajabu kabisa! Ratiba iliyopangwa na kuridhiwa na klabu zote 20 kupanguliwa kwa sababu klabu moja kubwa inataka kujiandaa na mechi yao. Hizi mbeleko za TFF na Bodi ya Ligi (TPLB) zinazozibeba klabu kubwa hazisaidii afya ya soka letu. Zinalemaza klabu zetu ndio maana zimekuwa zikiachwa mbali na wapinzani wao katika anga za kimataifa.

Kwa mfano Simba ilipangwa icheze jana Jumamosi, lakini mechi imesogezwa hadi leo Jumapili dhidi ya Mwadui. Yanga iliyokuwa ianze msimu kwa kuvaana na Mtibwa Sugar mjini Morogoro, mechi yao ilihamishwa Dar kimbeleko mbeleko.

Bahati mbaya ni kwamba TFF na TPLB wanaziangalia klabu kubwa na kuzibeba licha ya kuwa na uwezo na kuzisahau klabu ndogo zenye kutatizwa na hali mbaya ya ukata.

Biashara iliyokuwa ianze safari kuja Dar ili kuvaana na Simba, kisha kuifuata Mtibwa Sugar mjini Morogoro, sasa italazimika kutenga bajeti ya safari mbili bila kupenda. Hasara hizi kwa klabu ndogo za kuahirishiwa mechi ili kuzibeba Simba, Yanga na nyingine kuwa zinaharibu soka letu.

TFF na TPLB kwanini walipanga hizi mechi za mwisho za Simba na Yanga kabla ya kukutana kwao? Hawakujua au ni kwa vile mbeleko ipo mikononi mwao na wanaitumia watakavyo.

Ni vigumu! Klabu zetu kwenda sambamba na Al Ahly, Zamalek, TP Mazembe au Mamelodi wakati zimezoea kubewa kwa kila jambo ambalo halina muhimu wa kulifanya hivyo kwenye soka.

Advertisement