TASWIRA YA MLANGABOY : Kuziacha Simba, Yanga zitawale ni kuua soka

Friday February 14 2020

Kuziacha Simba, Yanga zitawale ni kuua soka, Ligi Kuu Tanzania Bara,Mwadui FC na JKT Tanzania,Simba,Ligi Kuu ya Tanzania Bara,

 

By Andrew Kingamkono

MCHAKAMCHAKA wa Ligi Kuu Tanzania Bara umeendelea kushika kasi kila kona nchini huku timu nyingine zikisaka ubingwa, nyingine zainapigania kukwepa janga la kushuka daraja katika ingwe hii ya lala salama.

Katika mzunguko huu wa pili tayari mashabiki wameshuhudia Simba ikiongoza ikiwa na pointi 53, baada ya mechi 21, ikifutiwa na Azam (pointi 44) na Yanga ikiwa ya tatu na pointi 38.

Pamoja na kushuhudia Simba ikiongoza katika ligi hiyo bado hatujaona ushindani kwa timu shiriki kiasi cha kuacha vijana hao wa Msimbazi kuongoza ligi kwa tofauti kubwa ya pointi.

Hakuna ubishi kwa Simba kushinda mechi zote, kwa sababu ni timu nzuri na imejiandaa msimu huu kuhakikisha inaweka rekodi nzuri ikiwa imefungwa mechi mbili tu dhidi ya Mwadui FC na JKT Tanzania na sare mbili.

Ukiangalia hali inavyokwenda sasa unaona kabisa ligi yetu bado haina ushindani wa maana huku suala Simba na Yanga kuendelea kutesa milele likizidi kukua katika soka letu.

Naamini timu nyingine zinaweza zikiamua kwa nia moja kuifanya ligi yetu kuwa bora na yenye ushindani mkali, lakini kwanza zinaogopa timu kubwa na kujiona kuwa hawaziwezi. Pili zinajishusha mno na kuona ligi sio yao bali ni ya Simba na Yanga na tatu kuna mambo mengine yanafanyika nyuma ya pazi ambayo wengi wanayajua.

Advertisement

Ligi yetu bado inahitaji ushindani mkali kwa timu zote na kuondoa dhana za Usimba na Uyanga kila mara kwani hali ndio inaangamiza soka letu.

Tunajua timu za ‘Big Four’ England ziko juu zaidi ya wengine, lakini ukiangalia sasa hakuna aliyejihakikishia nafasi kwani kila timu inakomaa na inataka kuingia katika kundi hilo ndio maana hushangai kuona timu kubwa kama Manchester United, Arsenal zikiwa katika nafasi za chini katika msimamo wa ligi hiyo yote inatokana na ushindani na timu zote kujituma uwanjani kwani zinajua nafasi hizo hazina mwenyewe.

Kila timu itambue kuwa imepata nafasi ya kushiriki ligi na ni lazima ionyeshe uwezo ili mashabiki wapate ladha ya ligi hiyo.

Kila timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara ijue timu ya Taifa bora inatokana na ligi bora yenye mchanganyiko wa wachezaji bora ili soka letu liende mbele zaidi kimataifa.

Mfano wa Ligi Kuu ya Uganda, ni ligi yenye ushindani na wachezaji wake wengi wanapata fursa ya kutoka nje ya nchi na kwenda kutafuta changamoto nyingine.

Kwa kipindi hiki ambacho tunajianda na mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN 2020 Cameroon) ni fursa kwa wachezaji wa klabu ndogo kuonyesha uwezo wao ili kumshawishi kocha kuwachukua.

Lakini kuziachia Simba na Yanga zishinde kila mechi kiulaini hakuwasaidii katika michuano ya kimataifa wanayokwenda kushiriki na ndio maana kila mara wanaishia raundi za awali na kutolewa.

Klabu zote za Ligi Kuu zinapocheza kwa ushindani katika kila mechi achana na hii ya kuzikamia Simba, Yanga na Azam kunasaidia kukuza soka la nchini hii kwa ujumla.

Nafikiri wakati wa timu zote kuamka na kupambana hadi mwisho kuhakikisha bingwa wa ligi anapatikana kihalali na kiuwezo uwanjani na kuifanya Ligi Kuu kuwa na ushindani mkubwa.

Pia, waamuzi wetu waache kuziogopa timu kubwa na kutoa uamuzi tata yasiyo na mpango eti kwa sababu ya kuhofia viongozi fulani au watapata kitu fulani kutoka kwa timu hizo.

Wachezeshe kwa kufuata sheria na kuipa haki kila timu inayoshiriki ligi hiyo ili bingwa apatikane kwa haki, waige mazuri ya wenzao wa nje wanaochezesha ligi dhidi ya timu kubwa.

Kitu kingine kwa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kuhakikisha ligi inajiuza kwa kuwa na thamani kubwa mbele ya jamii.

Ni wakati huu ambao TFF wanatakiwa kutafuta wadhamini ambao wa kuwekeza pesa kwenye ligi ili timu ziweze kuishi katika mazingira sawa na Simba na Yanga.

Sio kwa TFF peke yao hata klabu nazo zinapaswa kusaka wadhamani binafsi ili kuweza kupata fedha za kuzisaidia kuleta ushindani dhidi ya timu hizo vigogo.

Fedha hizi zinaweza kuzisaidia timu kuwalipa mishahara muzuri wachezaji wao na kuweza kuwapa lishe na kuwaweka katika mazingira mazuri ya kambi.

Mfano mzuri ni kwa timu kama Namungo FC, ina udhamini mkubwa kutoka kwa CRDB, SportPesa ukiondoa pesa za udhamini wa Vodacom ambao unatolewa kwa timu zote. Ni haki sasa wachezaji wa Namungo kushindana na timu kubwa za Simba na Yanga na kuzipa changamoto ya kutosha.

Hata hivyo, binafsi namini mzunguko huu tutashuhudi ushindani mkubwa kwa timu zote na kuhakikisha tunapata bingwa wa ukweli na hata zile timu zitakazoshuka wakubali wenyewe kweli tulipambana lakini bahati mbaya tumeshuka daraja.

Advertisement