Kiwango cha wachezaji wa Azam FC kinasikitisha

Thursday January 10 2019

 

By Mwanahiba Richard

Mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanaendelea kisiwani Unguja na fainali yake itachezwa Jumapili kisiwani Pemba kwenye Uwanja wa Gombani.

Ni mashindano ya 13 tangu kuanzishwa kwake na Azam FC ndiyo inaongozwa kwa kubeba ubingwa mara nyingi.

Simba ni timu inayofuatiwa kutwaa ubingwa huo na imebeba mara mbili na sasa timu hizo mbili zimetinga hatua ya nusu fainali.

Yanga haina bahati na mashindano haya, kwani kwa miaka miwili mfululizo imekuwa ikitolewa hatua za mwanzo na tayari leo Alhamisi itaanza safari yake ya kurejea jijini Dar es Salaam na wanaonekana kutojali mashindano haya hawachukulii wala kuyapa uzito kama ilivyo kwa timu zingine.

Msimu huu imeleta wachezaji wengi vijana ambao wametoka timu yao ya vijana huku kikosi kizima kikibaki Dar es Salaam na hayo ndiyo yalikuwa maamuzi ya kocha wao mkuu, Mwinyi Zahera.

Zahera aliweka msimamo wake wa kutoleta kikosi kizima akisema mashindano haya hayana umuhimu sana kwake kama ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA. Hakuna aliyempinga tofauti na miaka ya nyuma Yanga iligomea mashindano hayo na kulazimika kulipa faini ya Sh10 milioni.

Mashindano haya huwa yanashirikisha hata timu kutoka nje ya nchi ya Tanzania lakini msimu huu hakuna timu iliyoshiriki kutoka nchi jirani. Mashindano hayo ambayo yalishirikisha timu tisa zilizopangwa makundi mawili zimetolewa timu tano na kubaki nne ambazo ni Simba, KMK, Azam na mshindi kati ya mechi za jana za kundi B.

Waandaaji wa mashindano hayo wametumia pesa nyingi sana ingawa viwango vilivyoonyeshwa na timu shiriki huenda haziendani na gharama zinazotumika.

Achilia mbali na Simba iliyoleta kikosi kizima hatua ya makundi, Azam pia ilikuwa na kikosi chao chote ila kiwango walichokionyesha ni afadhali ya Yanga walioleta wachezaji asilimia kubwa kutoka timu ya vijana.

Azam ambao ndio mabingwa watetezi wa mashindano hayo, wachezaji wake hawaonyeshi nia na uchungu wa kile wanachokipata kutoka kwa mabosi wao ukizingatia ndiyo timu pekee inayoishi hoteli ya hadhi ya juu kabisa kisiwani Unguja inayomilikiwa na Bhakresa.

Azam pamoja na kushinda baadhi ya mechi walikutana na changamoto kubwa kutoka timu za hapa visiwani walizocheza nazo achilia mbali Yanga ya makinda.

Kama uwezo wao wa hapa ndiyo watakaokwenda nao kwenye ligi basi wamiliki wa timu hiyo watarajie kuona mengi tu yakitokea ikiwemo kuukosa ubingwa wa ligi na Kombe la FA.

Hakuna kinachokosekana ndani ya klabu ya Azam ambayo ndiyo inayoongoza kwa utajiri kwenye ligi kuu Bara, wachezaji hulipwa vizuri na hawana shida ya kifedha kama timu zingine ambazo hazina udhamini hata mmoja lakini faida wanayorudisha kwa mabosi wao ni ndogo mno tena inayozua hofu na maswali.

Zingekuwa timu zingine basi moja kwa moja ingesemekana kwamba wachezaji wanacheza chini ya kiwango pengine wanaingia uwanjani bila kula ama wana msongo wa mawazo kwa kukosa mishahara.

Je wanasumbuliwa na majeruhi napo jibu linakuwa hapana, kwani hata kama wana majeruhi lakini si kwa kiwango kikubwa namna hiyo, au labda wameshindwa kuelewa vyema mbinu za kocha wao Hans Pluijm.

Nyie wachezaji wa Azam oneeni huruma uwekezaji wa mabosi wenu kwa kujitambua kuwa hiyo ni kazi yenu, mjitume na kama tatizo lipo benchi la ufundi basi pia lifanyiwe kazi.

Advertisement