MTAA WA KATI : Kisa ni pesa za burebure zinazopatikana England

Muktasari:

  • Anatajwa pia Laurent Blanc. Haishii hapo, majina ni mengi. Jose Enrique. Max Allegri. Carlo Ancelotti ameshakuja na anatajwa kwamba atakuja tena. Claudio Ranieri amerudi. Hivyo ndivyo Ligi Kuu England inavyovutia makocha bora kabisa duniani.

JOSE Mourinho ameondoka. Antonio Conte amekwenda. Lakini, usishangae ukiwaona wamerudi tena kwenye Ligi Kuu England baada ya miaka michache baadaye. Zinedine Zidane anatajwa.

Anatajwa pia Laurent Blanc. Haishii hapo, majina ni mengi. Jose Enrique. Max Allegri. Carlo Ancelotti ameshakuja na anatajwa kwamba atakuja tena. Claudio Ranieri amerudi. Hivyo ndivyo Ligi Kuu England inavyovutia makocha bora kabisa duniani.

Makocha wote mahiri hata wale wasio mahiri sana, majina yao yanahusishwa na Ligi Kuu England. Orodha ni ndefu. Mfano mdogo tu, Julen Lopetegui baada ya kufutwa kazi kwenye kikosi cha La Roja, kisha kwenye chama la Los Blancos, kilichofuatia, jina lake kutajwa likihusishwa na Ligi Kuu England.

Si kitu cha kushangaza tena. Kuna wakati karibu makocha wote bora duniani walikuwa kwenye Ligi Kuu England.

Pep Guardiola alikuwa na bado yuko Man City. Jurgen Klopp yupo Liverpool. Arsene Wenger alikuwa Arsenal, Conte Chelsea na Mourinho alikuwa Man United. Rafa Benitez yupo Newcastle United. Mauricio Pochettino anafanya kazi yake pale Tottenham.

Hao ni makocha wote bora. Conte ameondoka amekuja Maurizio Sarri. Mourinho ameondoka amekuja Ole Gunnar Solskjaer. Benitez ametulizana Newcastle United na Ranieri amerudi kufanya kazi Fulham. Kitu gani kinawafanya makocha bora kabisa duniani kufurika England?

Wenger kaondoka, Unai Emery ametua Arsenal, akitokea PSG. Vipaji vya wachezaji? Hapana. Kama ni hivyo, kwanini wasiende kujazana kwenye La Liga. Kwenye Ligue 1 kwa sasa kuna vipaji vingi sana.

Kylian Mbappe na Neymar wanacheza kwenye ligi hiyo. Hata klabu za Ligi Kuu England zinasumbua akili kwa sasa kwenda kusajili Ufaransa. Kwa maana hiyo ishu sio vipaji. Sababu kubwa hapo ni pesa.

Ligi Kuu England inalipa. Inalipa vizuri kuanzia wachezaji hadi makocha. Jambo hilo linawafanya makocha wengi kufikiria kwenda kufanyakazi kwenye ligi hiyo. Conte anasubiri ofa ya kutoka England. Mourinho anazugazuga tu huko, lakini jina lake karibuni tu, lilihusishwa na kurudi Chelsea kwa mara ya tatu.

Utamu wa kwenye Ligi Kuu England, hata kama ukifutwa kazi, akaunti yako inanona vyema. Utakumbana na aibu tu ya kufutwa kazi, lakini familia yako mambo yao yatakuwa mazuri. Kocha Mourinho amefutwa kazi Man United hivi karibuni, lakini kwenye akaunti yake imeingizwa Pauni 15 milioni.

Kwenye Serie A huwezi kulipwa fidia kama hiyo. Huwezi unaweza kuipata England tu.

Bundesliga na hata kwenye Ligue 1, hutarajii kukutana na fidia ya pesa ndefu hivyo. Shida ni kwamba hata mikataba utakayosaini huko, mshahara wake unakuwa wa kawaida tu. Lakini, England, Louis van Gaal alikuja akachota pesa kaondoka zake.

Luiz Felipe Scolari amekuja, amechota pesa ameondoka. Imetokea hivyo kwa makocha kibao wakiwamoAndre Villas-Boas, Ancelotti na Conte. Wakali hao wamebeba zaidi ya Pauni 100 milioni kupitia fidia tu walizolipwa kwa kufutwa kazi katika klabu za Ligi Kuu England.

Kuna mtu asiyependa pesa za nje nje kiasi hicho? Solskjaer inawezekana anafahamu wazi kabisa hana ubavu wa kuwa kocha wa kudumu kwenye kikosi cha Man United.

Lakini hawezi kukataa ofa hiyo kama itawekwa mezani kwake, kwa sababu anafahamu baada ya muda, akifukuzwa, kuna mkwanja mrefu utaingia kwenye akaunti yake. Hana cha kupoteza.

David Moyes anaishi maisha matamu kwa sasa. Amefanya kazi miezi isiyozidi 10 pale Man United, ameondoka na pesa ndefu. Hivyo ndivyo pesa zinavyowafanya makocha wa maana kuwa wengi kwenye Ligi Kuu England. Si kwa wageni tu, hata kwa wazawa wenyewe. Sam Allardyce amepiga pesa nyingi sana kwa kukubali kazi, kisha anafukuzwa ndani ya muda mfupi, mfuko wake unanona. Fidia ya kuvunja mikataba.

Hicho ndicho kinachowafanya makocha wengi kuja England, kwa sababu wanafahamu pesa yake watakayovuna ni ndefu.

Ndio maana miaka michache baadaye, utamwona Zidane kwenye Ligi Kuu England na pengine utamwona tena Jose Mourinho kwenye moja ya timu vigogo zinazolipa pesa ndefu za fidia zinapovunja mikataba.

Pengine kwa klabu za Ligi Kuu England kujiondoa kwenye hilo, zianzishe utaratibu wa kusaini mikataba inayowabana makocha wanapofungwa idadi fulani ya mechi, wanaposhindwa kupata matokeo kwenye mechi za aina fulani, basi mikataba yao itakuwa imevunjika rasmi na wataondoka, tena kwa kuzilipa klabu fidia kwa sababu wanalipwa pesa nyingi na wanasajiliwa wachezaji wanaowataka. Mourinho asingerudi England.